ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, amewapongeza madaktari na wauguzi ambao hawakushiriki mgomo, kwa kuwa walifanya kazi ya ki-Mungu kuwahudumia wanyonge.
Amesema hawalaumu waliogoma kwa kuwa walikuwa na hoja ambazo kwao ni za msingi, lakini kwa wale walioendelea na kazi ya kuwahudumia wagonjwa kwa kusema liwalo na liwe, wana moyo wa ki-Mungu na thawabu yao ni kubwa.
Pengo alitoa kauli hiyo jana katika Parokia ya Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam alipokuwa akihubiri katika Misa ya maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani iliyohudhuriwa na wagonjwa zaidi ya 100 kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa MOI), Ocean Road na wa majumbani.
Hata hivyo alisema si kwamba hatambui dhiki walionayo watoa huduma za tiba, lakini aliwaonya kuwa wakati mwingine wanapaswa kuangalia kwanza mapenzi ya Mungu kabla ya maslahi binafsi.
Katika kusisitiza hilo, Pengo alisema, “Ninawapongeza madaktari na manesi ambao hawakugoma, mwongozo kwenu watoa tiba na wengine wote ni kwamba tusiweke maslahi yetu mbele zaidi ya wenye dhiki na uhitaji.” Alisema madaktari walioendelea na kazi japo kwa siri na adha kubwa, walishiriki mwongozo huo wa Mungu na walikuwa na moyo wa Yesu aliyemtakasa mkoma bila kujali sheria za Wayahahudi ambazo zilimkataza Kuhani kumshika mtu mwenye ukoma.
“Yesu alisema liwalo na liwe, akamtakasa mkoma, na walioendelea na kazi walisema vivyo hivyo ili wagonjwa wajisikie Mungu hajawaacha, kila mhudumu wa tiba Mkristo anapaswa kuwa hivyo,” alisisitiza Pengo. Pia alishukuru hali kutengemaa na kurudi kuwa bora zaidi ya awali na kuiomba Serikali iwe na moyo wa huruma kwa kuwasikiliza watumishi wanaofanyakazi katika mazingira magumu, ili hali isijirudie tena.
Aliwataka wagonjwa kutambua kuwa Mungu anawapenda na Kanisa linawajali hivyo wasife moyo bali wamtegemee daima. Misa hiyo ilikuwa maalum kuadhimisha siku hiyo ya kimataifa ambayo hufanyika Februari 11 kila mwaka. Katika misa hiyo pia, wagonjwa wakisimamiwa na madaktari wawili na wauguzi sita, walipakwa Mafuta Matakatifu na kuwekewa mikono na Pengo na mapadri walioshiriki ibada hiyo na baadae walishiriki chakula cha mchana pamoja na Pengo.
Ushuhuda wa mgonjwa
Mgonjwa mmoja kutoka Muhimbili ambaye ni mwenyeji wa Kigoma, Yunus Yusufu (30) alimshukuru Mungu kwa kumalizika kwa mgomo na kuiomba Serikali pamoja na Kanisa kuendelea kuwapatia huduma bila kuchoka.
“Hali ilikuwa mbaya, nimelazwa Kibasila wodi namba 14 tangu Oktoba 30 mwaka jana, wakati wa mgomo tuliteseka sana, tulibaki wagonjwa watatu wodi nzima na wengine walichukuliwa na ndugu zao lakini sisi tulibaki kwa kuwa ndugu wapo mbali, tunawashukuru manesi kwa huduma nzuri wakati wote huo,” alisema Yusufu.
Yusufu alisema, baadhi ya manesi hao wakati mwingine kwa siri walikuwa wakiwauliza aina ya dawa wanazotumia kama zimekwisha na kwenda kuzitafuta na kuwapatia huku wakiwahudumia kwa moyo katika zamu zao jambo lililowatia moyo na kuwapunguzia maumivu. “Kwa kweli manesi walikuwa wanakuja wodini kama kawaida kulingana na zamu zao, walitusaidia maana wengine hatujiwezi kututafutia dawa popote pale, kwa kweli tulimuona Mungu kupitia wao,” alisema Yusufu.
Askofu Shao ataka subira
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao aliwataka wataalamu hao wa tiba kuwa na subira wakati maslahi yao yakijadiliwa na utafutiwa njia sahihi za kuyatatua na Serikali.
Alisema hayo jana alipokuwa akipokea jengo lenye madarasa mawili, maktaba, maabara na vifaa vya kufundishia katika Hospitali ya Machame vilivyotolewa na shirika la huduma za afya kwa jamii la Alegent Health la Marekani. Aliiomba Serikali kutazama upya maslahi ya watumishi katika kada ya afya ili kudhibiti tabia ya baadhi ya madaktari na wauguzi kukimbilia kufanya kazi nje ya nchi.
Akizungumzia jengo hilo, Dk Shao alisema limekamilika baada ya kanisa kwa kushirikiana na marafiki zake kuchangisha zaidi ya Sh milioni 70 na shirika hilo kuongeza kiwango kinacholingana na fedha zilizochangwa. Rais wa shirika hilo, Richard Hachten alisema limegharimu zaidi ya Sh milioni 155 na limejengwa kwa ushirikiano na kanisa hilo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment