Monday, February 20, 2012

Majambazi wateka wafiwa, wampekua maiti

MAJAMBAZI wamevamia na kuteka gari lililokuwa likimsafirisha maiti kutoka Mpanda mkoani Rukwa kwenda mkoani Mara na kumpekua maiti wakitafuta fedha na vitu vya thamani.

Utekaji huo ulifanyika Ijumaa iliyopita saa saba usiku katika eneo la Mtakuja Manispaa ya Tabora wakati wafiwa wakisafirisha mwili wa mtumishi wa Halmashauri ya Mpanda kwenda Musoma kwa maziko.

Akisimulia mkasa huo jana, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Moshi Musa Chang'a alisema baada ya gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser mali ya halmashauri hiyo kufika Mtakuja, walikuta mawe yamepangwa barabarani na liliposimama, ghafla kundi la majambazi lilitokea porini likiwa na mapanga na marungu na kuteka gari hilo.

Alisema baada ya kuteka gari hilo, waliwapekua waombolezaji waliokuwa wakisindikiza msiba na kuwapora zaidi ya Sh milioni mbili na simu za mkononi.

Chang'a alisema majambazi hao kabla ya kupora fedha hizo, waliwashambulia waombolezaji hao kwa marungu na ubapa wa mapanga na kuwasababishia majeraha madogo.

“Baada ya kumaliza kuwapora waombolezaji hao, ndipo wakaanza kuipekuwa maiti kwa lengo la kupata fedha zaidi au kitu chochote kilichokuwa kimefichwa kwenye jeneza hilo ili wakichukuwe,” alisema Chang’a.

Kwa mujibu wa Chang'a, muombolezaji mmoja alikuwa ameficha simu yake akatoa taarifa kwake na kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda ambao walifikisha taarifa hizo Polisi Tabora waliofika eneo la tukio usiku huo.

Alisema polisi walipofika eneo la Mtakuja, hawakuwakuta majambazi hao na tayari wameanzisha msako wa kuwabaini majambazi hao.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Tabora alisema majambazi hao hawako mbali na eneo la Mtakuja na kuwataka wananchi watoe taarifa Polisi ili wawakamate na kuwafikishwa katika vyombo vya sheria.

Alisema kila mwananchi wa Kata ya Mtakuja ana wajibu wa kushirikiana na Jeshi hilo ili kutokomeza kikundi hicho kinachosumbua watu mara kwa mara hasa nyakati za usiku.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Antony Rutta amekiri kutokea kwa uporaji huo na kuwataka wananchi kuwafichua watu wanaofanya uhalifu huo.

Aliwataka wananchi watoe taarifa hizo kwa siri ili Serikali ichukue hatua madhubuti kupambana na wahalifu hao ikiwemo kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.

No comments:

Post a Comment