CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Wilaya ya Nachingwea, mkoani
Lindi kimepata pigo la kuondokewa na viongozi wake wawili, akiwemo Mwenyekiti wa Wilaya,
Hassani Mkopi na katibu wake, Saadati Kamalu.
Viongozi ambao wameachia ngazi na kujiunga na CCM kwa madai ya kushindwa kukitumikia
vema chama hicho tangu walivyokabidhiwa madaraka kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Katibu wa muda wa Chadema, Jordani Membe alisema juzi kuwa Mkopi alijiondoa Chadema na kujiunga na CCM mwishoni mwa mwezi uliopita wakati wa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal katika Kijiji cha Chiumbati, Kata ya Naipanga.
“Tukiwa katika mkutano huo katika Kijiji cha Chiumbati, ghafla mwenzetu aliamua kujivua gamba la Chadema na kulivaa lile la CCM kwa kumpatia Dk. Bilal kadi yetu ya Chadema,” alisema Membe.
“Katibu wetu Kamalu amedai ameamua kujiuzulu baada ya kushindwa kukitumikia vema
chama kama alivyokabidhiwa na wanachama wakati wa uchaguzi uliopita,” alisema akinukuu kauli yake.
Kutokana na kujiuzulu kwa Kamalu, Kamati ya Utendaji kwa kushirikiana na Baraza la Wazee wa Chadema waliamua kufanya uteuzi mdogo wa kuziba nafasi hiyo, ambapo Diwani wa Kata ya Nkotokuyana, Likolovero Hassani alichaguliwa nafasi ya uenyekiti, na yeye Membe aliteuliwa kushika nafasi ya ukatibu wa muda.
Membe alisema viongozi hao watashikilia nafasi hizo hadi Uchaguzi Mkuu wa Chadema
utakapofanyika mwaka 2013, badala ya 2014 kutokana na mabadiliko mafupi yaliyofanyika
kwa lengo la kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za vijiji, vitongoji na mitaa.
No comments:
Post a Comment