KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, imepewa jukumu la kuangalia mgogoro
uliopo kati ya madaktari na Serikali kwa lengo la kulishauri Bunge namna ya kumaliza
mgogoro huo na kuhakikisha hali hiyo hairudii.
Pamoja na uamuzi huo, Bunge pia jana kupitia Naibu Spika, Job Ndugai, limetaka madaktari warejee kazini mara moja na kuacha mgomo. Agizo la mgogoro huo kupelekwa katika Kamati hiyo, lilitolewa na Ndugai, wakati akijibu Mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), kabla ya Serikali kuwasilisha kauli yake juu ya mgomo huo.
Mnyika aliomba Mwongozo kwa kuzingatia Kanuni ya 5 ili kauli ya Waziri ijadiliwe na wahusika wawajibishwe. Hoja ya kujadiliwa kwa kauli ya Serikali ilihitaji kwanza kutenguliwa kifungu cha 49 cha Kanuni za Bunge lakini haikuweza baada ya wabunge kutounga mkono hoja ya Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), ambaye alizungumzia haja ya kutumia Kanuni ya 55 (3) na Kabwe Zitto aliyetaka hoja ijadiliwe.
Hata hivyo, kwa kutumia busara zake, Ndugai, aliagiza Kamati ikae na kujadili suala hilo kwa kukutanisha pande zote - madaktari na Serikali, kabla ya kulifikisha katika Bunge kwa ushauri ambao si lazima uwe agizo. Alisema kurejesha suala hilo kwa Kamati ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Magreth Sitta (CCM) na Makamu wake ni mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile (CCM), kulitokana na haja ya kusikiliza pande hizo zenye mgogoro na kufuatilia shauri lingine ambalo halikuwekwa wazi bungeni la wizara kuwa na baadhi ya viongozi wasiowajibika na wenye lugha za kashfa.
Alisema wamesikia upande mmoja na kwa kuwa upande wa pili (madaktari) haukuwapo, ni
vema ukawepo utaratibu wa kuusikiliza pia. Pamoja na kuwa hakuna muda uliopangwa, uamuzi wa Naibu Spika uliungwa mkono na Bunge, kwa kushangiliwa na pande zote. Spika aliitaka Kamati hiyo ifanye kazi haraka na itoe taarifa kuhusu yaliyojiri kwenye mazungumzo
hayo na ushauri wa Bunge kwa pande husika.
Ndugai aliomba pande zinazosigana kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo, ambayo vikao vyake, wabunge wengine wenye nia wanaruhusiwa kuhudhuria. Kamati hiyo inatarajiwa kukutana na Serikali, Chama cha Madaktari, Jumuiya ya Madaktari na madaktari bingwa. Pamoja na kurejesha tamko hilo kwa Kamati hiyo, jana kabla ya kuahirisha kikao cha asubuhi, Ndugai aliwataka madaktari kwa niaba ya wabunge kurejea kazini kusaidia Watanzania wenzao.
“Tunawapenda madaktari, warudi kazini waheshimu viapo vyao,” alisema Ndugai. Awali Bunge lilielezwa hatua zilizofanywa na Serikali katika kutafuta suluhu ya mgomo wa madaktari na kusema kwamba kila masharti mapya yalipojitokeza yalionesha, kwamba madaktari hawataki suluhu. Kauli ya Serikali Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, akiwasilisha bungeni kauli ya Serikali, alisema pamoja na hayo yote, imeundwa Kamati ya kushughulikia tatizo hilo na kutaka wadau wote kuipa maoni.
“Serikali imedhamiria kwa dhati kulitatua tatizo lililopo mbele yetu. Kwa mantiki hiyo, tunawasihi madaktari, wataalamu wengine wa sekta ya afya na wadau wote wa sekta hiyo, kutumia fursa iliyo mbele yetu, kutoa maoni yao kwenye kamati iliyoundwa na Serikali ili kupata namna bora ya kutatua mgogoro uliojitokeza,” alisema Dk Mponda.
Januari 30, Serikali iliunda kamati ya kushughulikia maazimio yaliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu, ili kuyachambua na kutoa maoni na mapendekezo yatakayoisaidia Serikali kumaliza mgogoro wa watumishi wa sekta ya afya. Aidha, Dk. Mponda aliwaeleza wabunge, kwamba Serikali inasikitika kwa athari zilizotokea kwa wananchi kutokana na mgogoro huo.
Hata hivyo, aliliambia Bunge, kwamba huduma zimeanza kutengamaa katika hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) lakini huduma za dharura na wodini katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(MOI) zimedorora kwa kuwa madaktari 21 hawajarudi kazini. “Mipango ya kupeleka madaktari
kutoka jeshini inakamilishwa, ili huduma za wagonjwa wa nje (OPD) zirejeshwe,” alisema
Mponda. Aliongeza kwamba madaktari walio kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye maeneo mengi, wengi bado hawajarudi kazini Muhimbili.
Alilieleza Bunge kuwa, huduma zinatolewa kama kawaida katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, na pia hali ni kama hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza. Alisema, madaktari 81 walio kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi wamerudi kazini, hivyo huduma zinaendelea kama kawaida.
Hali Bugando
Naye Clara Matimo, anaripoti kutoka Mwanza, kwamba uongozi wa Bugando umesema matibabu kwa wagonjwa yanakwenda kama kawaida licha ya baadhi ya vitisho kutoka kwa wafanyakazi wachache wanaoeneza uvumi wa kuwapo mgomo wa madaktari.
Mkurugenzi wa Bugando, Dk Charles Majinge, alisema jana kwamba tangu mgomo wa madaktari uanze katika baadhi ya hospitali za serikali nchini, Bugando bado inaendelea na matibabu na wagonjwa wanapata huduma kama kawaida. "Sisi katika hospitali yetu ya rufaa Bugando, tunafanya kazi kwa maadili zaidi ambayo yanaendana na yale ya kiroho, ukizingatia kuwa hospitali hii inaendeshwa kwa misingi ya dini ya Kanisa Katoliki… tunajali afya zaidi za jamii kuliko kuweka maslahi mbele," alisema Dk. Majinge.
Alitoa ushauri kwa madaktari wengine nchini wanaoendelea na mgomo, kufanya subira wakati Serikali inatafakari namna ya kuboresha maslahi yao, kuliko kuacha wagonjwa wanateseka na baadhi yao kufariki dunia kutokana na mgomo huo wa madaktari. Wanaogoma Aidha, alisema wanaoendelea kugoma katika hospitali hiyo ni wanafunzi ambao wanachukua mafunzo ya udaktari bingwa ambao mara kwa mara wamekuwa wakipiga simu kwa baadhi ya wagonjwa
wanaotaka kutibiwa katika hospitali hiyo, kuwa wasifike kutokana na hospitali kuendelea na
mgomo.
Hata hivyo, uchunguzi wa 'Habarileo' katika baadhi ya wodi pamoja na kufanya mahojiano na baadhi ya madaktari katika hospitali hiyo, ambao walisema wako kwenye mgomo baridi na kwamba wanaofanya kazi katika hospitali hiyo ni wakuu wa vitengo pekee na si madaktari. Baadhi ya wodi wagonjwa waliokuwa wamelazwa, waliondolewa na ndugu zao kwenda kutibiwa katika hospitali zingine za binafsi.
No comments:
Post a Comment