Thursday, February 2, 2012
Posho za wabunge mjadala kila kona
DK SLAA ATAKA RAIS AZIFUTE, CAG AZISHANGAA, PINDA, MAKINDA WATAKIWA KUJIUZULU
Waandishi Wetu
KITENDO cha Rais Jakaya Kikwete kumruka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Spika wa Bunge, Anne Makinda kuhusu posho za wabunge, kimeibua mjadala mzito nchini, huku wasomi na wanasiasa akiwamo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa wakimtaka mkuu huyo wa nchi azifute na kulivunja Bunge mara moja kuthibitisha msimamo wake. Juzi, ikiwa ni siku moja baada ya Pinda kusema tayari Rais Kikwete amesaini kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) za wabunge kutoka Sh 70,000 hadi Sh200,000 kwa siku, Ikulu ilitoa taarifa ikisema Rais Kikwete hakuwahi kusaini nyongeza hiyo bali alitaka Waziri Mkuu atumie busara katika kupatia suluhu suala hilo. Wakati Ikulu ikitoa taarifa hiyo juzi jioni, tayari mchana wa siku hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema, "Siyo kwamba tutaanza kutoa, tulishaanza kutoa na Rais ameshatoa kibali chake na mbunge atalipwa katika vikao tu, si kila siku na tena baada ya kukaa kwenye vikao na kusaini."
Mgongano huo wa kauli kuhusu posho hizo ulijitokeza tangu Novemba mwaka jana baada ya Mwananchi kuripoti kwa mara ya kwanza kwamba wabunge waliongezewa posho na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah kukanusha, akisema Rais hakuwa ameziidhinisha. Hata hivyo, siku tatu baadaye, Spika Makinda alithibitisha juu ya wabunge kuanza kulipwa viwango hivyo vipya vya posho akisema, Rais Kikwete tayari alishaidhinisha zilipwe kwa wawakilishi hao.
Jana, kwa nyakati tofauti wakizungumzia utata huo watu wa kada mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wanasiasa na wasomi, walielezea mkanganyiko huo kama kitendo cha hatari katika kipindi hiki ambacho nchi inatikiswa na mgomo wa madaktari.
Wanasiasa Katibu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alienda mbali zaidi kwa kusema kutofautiana kwa viongozi hao wa Serikali na Bunge kuhusu suala la posho mpya za wabunge, ni sawa na kutokuwa na Serikali.
Alifafanua kwamba posho hizo ni sawa na bomu ambalo limetegwa na sasa linakaribia kulipuka wakati wowote. “Rais na Waziri Mkuu wanatofautiana kuhusu posho, hivi hapo kuna Serikali kweli? Ndiyo maana tunasema posho hizi ni bomu litakalolipuka wakati wowote,” alionya Dk Slaa. Dk Slaa alisema wabunge hao kulipwa posho ya Sh330,000 huku wakiwa wamekaa kwenye viyoyozi wakati madaktari wanafanya kazi katika mazingira magumu ni laana. “Laana hii, ndiyo inawafanya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wanatofautiana na bado wasubiri sasa bomu litakalolipuka,” alisema Dk Slaa.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema Rais Kikwete anatakiwa kulivunja Bunge kwa kitendo hicho cha taasisi hiyo kujiongezea posho kinyemela. “Kama ingekuwa enzi za Mwalimu Julius Nyerere, kitendo hicho kilichotokea cha kujiongezea posho kingesababisha Bunge kuvunjwa, lakini, kwa Rais wetu mambo yataendelea kama kawaida,” alisema Mtatiro.
Kwa upande wa CCM, kimetoa tamko kikisema huu si wakati wa kupandisha posho na kupongeza hatua ya Rais Kikwete kuweka mambo wazi kwamba hakuzithibitisha. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa huu si muda mwafaka kwa wabunge kujiongezea posho.
CAG abaki mdomo wazi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Ludovick Utouh alisema kuwasilishwa kwa taarifa za mchanganyiko kuhusu posho za wabunge kunachanganya wananchi. Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Utouh alisema wabunge hawawezi kulipana posho bila Rais kuidhinisha.
“Ninachojua mimi ni kwamba, Serikali haiwezi kulipa wabunge bila ya fedha kuidhinishwa na Rais na kwamba hakuna kibali kinachotolewa zaidi yake, kutokana na hali hiyo taarifa zao zinatuchanganya,"alisema Utouh. Viongozi wa dini Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Yuda Thadeus Ruwaichi, alisema kugongana kwa kauli hizo, kunatoa taswira kwamba kuna jambo linafichwa kuhusu suala hilo. “Kugongana kwa hizi kauli kunaonyesha wazi kuwa, kuna kitu kimejificha hapa..., ni vyema ukweli ukaelezwa,” alisema Ruwaichi.
Alisema kuongeza posho za wabunge katika wakati huu ambapo kuna kada nyingi za utumishi wa umma kama walimu na madaktari wakiwa na hoja ambazo hazijapatiwa majibu, hakuleti taswira nzuri kwa Serikali. “Huku kunaonyesha kwamba, hakuna busara katika kufanya maamuzi ya mambo mazito yanayohusu hatima ya taifa hili. Kuchukua uamuzi kama huu wakati huu ambao watumishi wengi wa umma kama madaktari na walimu wana madai mbalimbali, siyo busara kabisa,” alisisitiza Ruwaichi.
Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Alhad Mussa Salim alisema kauli hizo tata za viongozi si ishara nzuri kwa mustakabali wa taifa. “Mgongano wa kauli za viongozi siyo sura nzuri. Tunashangaa kuona Mtendaji Mkuu akisema tofauti na bosi wake hiki ni kitu cha kushangaza," alisema Salim.
Wasomi Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema kama viongozi hao wa Serikali wanatofautiana kuhusu posho ni ishara kwamba kuna mtikisiko mkubwa wa kiutendaji. Alisema, “Pamoja na kwamba sijafuatilia vizuri viongozi hao kutofautiana katika suala la posho, dalili zinaonyesha kwamba kuna matatizo makubwa katika mihimili hiyo miwili,” alisema Dk Bana. “ Sina tatizo kama wabunge wakiongezewa mishahara yao, lakini kulipwa posho wakiwa kazini ni makosa makubwa,” alisema.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo cha Ushirika Moshi, Akwiline Kinabo aliwataka wabunge na Serikali kusoma alama za nyakati kwani posho hizo za wabunge zimewaudhi wananchi kwa kiwango cha kutisha.
Wanasheria, wanaharakati
Mkurugezi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba alisema utawala wa sheria haupo au umekufa kabisa. " Haiwezekani leo mhimili mmoja useme posho za wabunge zimepitishwa, halafu kesho yake mwingine ukanushe, sasa nchi inakwenda wapi?’’ alihoji Bisimba. Wakili wa kujitegemea, Harold Sungusia alisema tatizo kubwa lipo katika Katiba ya nchi ambayo imeshindwa kuonyesha mgawanyo wa madaraka ulipo katika mihimili yetu mitatu ya dola.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Fordia, Buberwa Kaiza amemtaka Rais Kikwete kufuta posho hizo ili kuthibitisha madai yake kwamba hajazibariki.
“Kauli hizi zinawachanganya wananchi maana haiwezekani Rais atoe msimamo wake halafu kiongozi wa chini yake apinge tamko la Rais, ni dhahiri kwamba Rais anaonekana kushindwa kutekeleza wajibu wake na kusimamia mamlaka yake kwa madaraka aliyonayo,”alisema Kaiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), kimemtaka Rais aeleze ni wapi wabunge wamepata idhini ya kupitisha posho badala ya kusema tu kwamba hajazibariki na kukaa kimya.
“Haiwezekani wabunge wajipitishie posho bila idhini ya Rais, maana hapa Serikali inataka kutuchanganya tu. Waziri Mkuu ni kiongozi wa Serikali, Rais ni kiongozi wa Serikali, lakini kila mmoja anasema lake, hii maana yake nini?" alihoji Mkurugenzi wa shirika hilo, Ananilea Nkya
Mjini Moshi, baadhi ya wakazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro wamemtaka Waziri Mkuu na Spika Makinda wajiuzulu kwa kuwaongezea wabunge posho bila idhini ya Rais. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema Pinda anapaswa kujiuzulu kwa kuwa ameidhalilisha Serikali na Makinda kwa sababu amewasaliti Watanzania maskini.
“Angalau kwa hili Rais ametukuna, lakini bado tunataka Pinda na Makinda wajiuzulu kwa kutoa kauli za kuudhi eti gharama za maisha zimepanda kwa wabunge ndiyo maana posho zipande,”alisema mmoja wa wakazi hao.
Habari hii imeandaliwa na Gedius Rwiza, Patricia Kimelemeta, Fredy Azzah, Raymond Kaminyoge, Shakila Nyerere, Daniel Mwingira, Dar, Moses Mashalla, Arusha na Daniel Mjema, Moshi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment