Tuesday, February 21, 2012

Mahakama Kuu yakubali Tanesco kuipinga Dowans


James Magai
MAHAKAMA Kuu Dar es Salaam imerejesha matumaini kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) baada ya kutupilia mbali pingamizi la Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans dhidi ya maombi yake ya kibali cha kukata rufaa.

Tanesco iliwasilisha maombi mahakamani hapo kutaka kibali cha kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya mahakama hiyo iliyoamuru kusajiliwa kwa tuzo ya Dowans ya Sh94 bilioni, iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).

Hata hivyo, Dowans nayo kupitia kwa wakili wake, Kennedy Fungamtama iliweka pingamizi dhidi ya Tanesco ikiiomba mahakama hiyo iinyime kibali hicho cha kukata rufaa kwa madai kuwa haina haki ya kisheria kupinga hukumu hiyo.

Lakini katika uamuzi wake jana, Jaji Dk Fauz Twaib alitupilia mbali pingamizi la Dowans akisema Tanesco inayo haki ya kukata rufaa.

Kwa mujibu wa taratibu za kesi ya migogoro ya kibiashara, kama mshindwa tuzo akitaka kukata rufaa kupinga tuzo iliyotolewa kwa mshinda tuzo, anawajibika kwanza kuomba kibali cha kukata rufaa hiyo kwa mahakama iliyotoa tuzo hiyo.

Hata hivyo, katika uamuzi wake, Jaji Dk Twaib alisema kwa mazingira ya kesi hiyo, Tanesco haikuwa na haja ya kuomba kibali mahakamani hapo ili kukata rufaa hiyo na kwamba ingeweza kutumia utaratibu wa kawaida tu.

Uamuzi huo unatoa matumaini kwa Tanesco kuanza harakati za kuzuia kisheria malipo ya Sh110 bilioni ambayo inapaswa kuilipa Dowans baada ya hukumu ya ICC.

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili anayeitetea Tanesco, Dk Alex Nguluma kutoka Kampuni ya Rex Attorneys alisema kutokana na uamuzi huo sasa watakwenda kukata rufaa moja kwa moja Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo.

Hukumu ya ICC

Novemba 15, 2010 AICC, chini ya Mwenyekiti, Gerald Aksen akisaidiwa na wasuluhishi Swithin Munyantwali na Jonathan Parker, ICC iliiamuru Tanesco iilipe Dowans fidia ya Sh94 bilioni, kwa kuvunja mkataba baina yao kinyume cha sheria.

Kutokana na uamuzi huo, Januari 25, 2011 Dowans iliwasilisha maombi mahakamani hapo ikiomba tuzo yake hiyo isajiliwe ili utaratibu wa ulipwaji wake uwe na nguvu ya kisheria.

Hata hivyo, Tanesco kupitia kwa mawakili wake, Rex Attorneys kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwasilisha pingamizi la usajili wa tuzo hiyo Februari 9, 2011.

Lakini, Septemba 28, 2011, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam aliamua tuzo hiyo ya Dowans ya Sh94 iliyotolewa na ICC isajiliwe na kuwa hukumu halali ya mahakama hiyo.

Katika uamuzi wake, Jaji Mushi alikubaliana na hoja za Dowans na kutupilia mbali pingamizi la Tanesco na kuamuru tuzo hiyo isajiliwe na kuwa hukumu halali ya mahakama hiyo.

Jaji Mushi alisema baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote, alibaini kwamba si sawa kwa mahakama hiyo kuingilia uamuzi wa ICC.

Alisema kwa kufanya hivyo ni kuruhusu kuhoji tena masuala ya kiukweli na ya kisheria ambayo pande husika zenyewe kupitia kwa makubaliano yake ziliyakabidhi kwa ICC kuyachunguza na kuyaamua.

No comments:

Post a Comment