Wednesday, February 15, 2012

Mabadiliko CCM kuwang'oa mafisadi


KINGUNGE ADAIWA KUPINGA, ASEMA HAYALENGI KUBORESHA MFUMO WA CHAMA
Midraji Ibrahim, Dodoma
SIKU moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitisha mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1977 juu ya namna ya kuwapata wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), imeelezwa kuwa mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwa kitanzi kwa watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho tawala kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Juzi, Nec ya CCM ilibariki mabadiliko muhimu ya katiba ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa ndani ambayo ni pamoja na kuanzisha utaratibu ambao wajumbe wa NEC waliokuwa wanatoka mikoani, sasa watakuwa wanachaguliwa kutoka wilayani na wabunge, wawakilishi na madiwani sasa hawataruhusiwa kushika nyadhifa za chama.

Katika marekebisho hayo, viongozi wakuu wastaafu wakiwamo Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marais wa Zanzibar na makamu wenyeviti wa chama hicho, wameundiwa Baraza la Ushauri na sasa hawatakuwa wajumbe wa NEC.

Hata hivyo, uamuzi huo umepingwa vikali na baadhi ya wajumbe ambao walisema marekebisho hayo hayana tija zaidi ya kutaka kudhoofisha upande mmoja ambao uko kwenye harakati za urais mwaka 2015 na kuutaja kwamba, ni genge la watuhumiwa wa ufisadi.

“Wamejaribu kuondoa wazee wastaafu ili Kamati Kuu isiwe na watu ‘strong’, lakini yote hayo yanalenga kwa mtu siyo mfumo. Chama kinatakiwa kufanya marekebisho yake kwa mfumo siyo mtu... ngoja twende tutaona itakavyokuwa,” alisema mjumbe mmoja wa NEC ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Mjumbe mwingine ambaye pia hakutaja kutambushwa jina lake gazetini alisema uamuzi huo wa kurejesha nafasi hizo wilayani, unalenga kuwazuia baadhi ya watu wasiingie katika vikao hivyo vya uamuzi na kuwazuia watuhumiwa wa ufisadi kuweka watu wao katika wilaya zote nchini hata kama wana fedha.

Alisema hata kama watuhumiwa wa ufisadi wana fedha nyingi, itakuwa vigumu kwao kuweza kupandikiza watu wao katika wilaya zote nchini.

“Kwa hiyo sasa hivi angalau kutakuwa na mkakati wa kuhakikisha mafisadi hawaweki watu wao wengi wilayani. Kwani itakuwa vigumu kumudu kuweka wajumbe wa NEC wilaya zote nchini, lakini pia, wao wenyewe itawawia vigumu kupenya.”

Mwishoni mwa mwaka jana, mpango wa kujivua gamba ndani ya CCM uligonga ukuta katika kikao cha NEC hatua ambayo ilimfanya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kutumia busara na kurejesha utekelezaji wa mpango huo kwenye Kamati Kuu (CC) kwa utekelezaji.

Kingunge apinga
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa, kada mkongwe wa chama hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru, ndiye mjumbe pekee aliyepinga marekebisho hayo, huku akiituhumu sekretarieti kwa kukiuka katiba ya chama hicho.

Kingunge anadaiwa kuwatuhumu Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kwa kuvunja katiba hiyo kutokana na Halmashauri Kuu kutokuwa na uwezo wa kupitisha marekebisho hayo zaidi ya kupendekeza kwa Mkutano Mkuu ambao ndiyo wenye mamlaka hayo.

"Mzee ametueleza wazi kabisa kwamba marekebisho hayo hayana maudhui zaidi ya kumlenga mtu mmoja, aliuza sekretarieti imepata wapi kwamba Halmashauri Kuu ina uwezo wa kufanya marekebisho haya?,” alisema mtoa habari hayo.

Lakini, katika utetezi wake, Sekretarieti ilisema kuna kifungu kinachotoa mamlaka hayo kwa NEC kupitisha marekebisho hayo na kutoa taarifa kwa Mkutano Mkuu. Hata hivyo, Kingunge hakukubaliana na hoja hiyo.

Ilielezwa pia kwamba marekebisho hayo yaliyopitishwa kwa kupigiwa kura na wajumbe kwa kupata theluthi tatu kutoka Tanzania Bara na nyingine tatu kutoka Visiwani, wote walikubali isipokuwa Kingunge pekee.

“Ila tulichojifunza kwa Mzee (Kingunge) ni kwamba lazima utetee unachokiamini hadi mwisho na alimtaka Katibu Mkuu kuandika kuwa amepiga kura ya hapana ili iwe kwenye kumbukumbu,” chanzo chetu kilieleza.

Hata hivyo, Kingunge alipotafutwa jana kwa simu kufafanua msimamo wake hakutaka kuzungumza chochote akisema kwamba alikuwa kikaoni...”Samahani niko kwenye kikao, asante.”

Yapokea taarifa ya Katiba Mpya

Katika hatua nyingine, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema Nec imepokea taarifa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa lakini ikaitaka Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, huku akitaka wanachama wao kujitokeza kutoa maoni pindi tume itakapoundwa.

Nape alisema mjadala ulikuwa iwapo Tume ya Maadili iundwe au la lakini kutokana na katiba kuruhusu kuundwa kwa tume mbalimbali wajumbe walikubaliana iundwe.

Aidha, alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa taarifa ya mgomo wa madaktari na wajumbe waliitaka Serikali kuharakisha makubaliano yaliyofikiwa na iwe inachukua hatua kabla ya migomo kusababisha madhara kama ilivyotokea.

Uchaguzi Mdogo Arumeru
Alisema NEC imetoa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwenye uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki na viti vinane vya udiwani vilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, utaratibu utakaotumika katika nafasi ya ubunge ni ule wa kura za maoni kwenye mkutano mkuu wa jimbo na kwamba Februari 13 hadi 18 wagombea watachukua na kurejesha fomu. Februari 20, mkutano mkuu wa jimbo utapiga kura na kesho yake, kamati ya siasa ya Wilaya ya Arumeru itajadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa ambayo itakutana Februari 24 na kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu ya CCM ambayo itakutana Februari 27.

No comments:

Post a Comment