Thursday, February 9, 2012

Wavulana wapeta matokeo kidato cha nne


BARAZA la Mtihani la Taifa(Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa asilimia 53.59 ya wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Hata hivyo, wakati asilimia hiyo ambayo ni sawa na wanafunzi 180,216 wakifurahia matokeo hayo, wenzao 3,301 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu ikiwamo mfanano usio wa kawaida wa majibu. Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako alisema wasichana waliofaulu ni 90,885 sawa na asilimia 48.25 na wavulana ni 134,241 sawa na asilimia 57.51.

“Mwaka  2010 watahiniwa waliofaulu walikuwa 223,085 sawa na asilimia 50.74, hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.63,” alifafanua  Dk  Ndalichako. Wanafunzi 10 bora Dk Ndalichako aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa kuwa ni Moses Andrew Swai kutoka shule ya Feza Boys,  Rosalyn  Tandau kutoka Marian Girls, Mboni Mumba kutoka St Francis Girls na  Sepiso Mwamelo kutoka St Francis Girls. Wengine na shule zao kwenye mabano ni  Uwella Rubuga (Marian Girls), Hellen Mpanduji (St Mary’s Mazinde Juu), Daniel Wallace Maugo (St Joseph Millennium), Benjamin Tilubuzya, (Thomas More Machrina), Simon Mbangalukela (St. Joseph Millennium) na Nimrod Rutatora (Feza Boys).

Wasichana 10 bora
 Kwa upande wa wasichana kumi bora, Dk Ndalichako aliwataja na shule walizotoka kwenye mabano kuwa ni Rosalyn (Marian Girls), Mboni  (St Francis Girls),  Sepiso Mwamelo (St Francis Girls),  Uwella Rubuga (Marian Girls) na Hellen Mpanduji (St Mary’s Mazinde Juu). Wengine ni Lisa Chille (St Francis Girls Mbeya), Elizabeth Ng’imba (St Francis Girls Mbeya), Doris Noah (Kandoto Sayansi Girls),  Herieth Machunda  (St Francis Girls Mbeya) na Daisy Mugenyi (Kifungilo Girls Tanga).

Wavulana 10 bora
Wavulana kumi waliofanya vizuri zaidi katika mtihani humo ni Moses Andrew Swai (Feza Boys), Daniel Maugo (St Joseph Millennium), Benjamini Tilubuzya, (Thomas More Machrina), Simon Mbangalukela (St. Joseph Millenium) na Nimrod Rutatora (Feza Boys). Wengine ni Simon Mnyele (Feza Boys), Paschal Madukwa (Nyegezi Seminary), Henry Stanlay (St Joseph Millenium), Fransisco Kibasa (Mzumbe) na Tumain Charles (Iliboru).
Shule 10 bora 
Matokeo hayo yanaonyesha shule kumi bora zenye zaidi ya watahiniwa 40 kuwa ni St. Francis Girls ya Mbeya, Feza Boys, St Joseph Millenium,  Marian Girls,  Don Bosco Seminary, Kasima Seminary,  St. Mary’s Mazinde Juu,  Canossa, Mzumbe na Kihaba.

Matokeo hayo yanaonyesha pia  shule 10 bora zenye watahiniwa chini ya 40 kuwa ni Thomas  More Machrina, Feza Girls, Dungunyi Seminary,  Maua Seminary,  Rubya Seminary, St Joseph Kilocha Seminary, Sengerema Seminary,  Lumumba,  Queen of Apostles- Ushirombo na Bihawana Junior Seminary.
Shule 10 za mwisho
Shule kumi za mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 40 ni Bwebwera, Pande Daraja, Mufindi, Zirai, Kasokala, Tongoni, Mofu, Mziwa, Maneromango na Kibuta. Na shule kumi za mwisho zenye watahiniwa chini ya 40 ni Ndongosi, St Luke, Igingwa, Kining’inila, Ndaoya,  Kilangali, Kikulyungu, Usunga, Mto bubu day na  Miguruwe. Waliofutiwa matokeo Dk Ndalichako alifafanua zaidi kuwa watahiniwa 3,301  waliobainika kufanya udanganyifu wamefutiwa matokeo na hawataruhusiwa kufanya mtihani wowote wa Necta kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.

Dk Ndalichako alisema  kati yao watahiniwa waliofanya mtihani huo walikuwa 426,314, sawa na asilimia 94.67 ya watahiniwa wote waliosajiliwa. “Mwaka 2010 watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 458,114  hivyo, idadi ya watahiniwa imepungua kwa watahiniwa 7,790 sawa na asilimia 1.70,” alisema Dk Ndalichako. Alisema  mwaka jana, watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 349,39 na watahiniwa huku wa kujitegemea wakiwa ni 100,934.  Akifafanua zaidi juu ya matokeo hayo, Mtendaji Mkuu huyo wa Necta alisema watahiniwa 450,324 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambao  wasichana ni 201,799, sawa na asilimia 44.81 na wavulana 248,525, sawa na asilimia 55.19. Alisema  jumla ya watahiniwa wa shule 180,216 sawa na asilimia 53.59 ya waliofanya mtihani wa kidato cha nne wamefaulu, kati yao wasichana wakiwa 69,913 na wavulana 110,303.

Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, waliofaulu ni 44,910  wasichana wakiwa 20,972 na wavulana 23,938.
Waliofutiwa mitihani 
Dk Ndalichako alisema  Necta imefuta matokeo ya watahiniwa 3,03 waliobainika kufanya udanganyifu kati yao,  watahiniwa wa shule ni 3,301 na wawili wakiwa wa maarifa (QT). Akifafanua zaidi juu ya udanganyifu huo alisema , 182 walikamatwa na wasimamizi wakiwa na makaratasi (notes) sita walikamatwa na simu, watatu walikuwa wakifanyiwa mtihani na watu wengine, wanne walisajiliwa kufanya mtihani kwa majina ya watu wengine.

 Dk Ndalichako aliongeza kwamba,  pia   watahiniwa 2,896 karatasi zao za majibu zilikuwa na mfanano usio wa kawaida, 155 karatasi zao za majibu  zilikuwa na miandiko zaidi ya mmoja, 14 kubadilishana karatasi katika chumba cha mtihani, 18 kukamatwa na karatasi za majibu zaidi ya moja, 25 wakiwa  na mfanano usio wa kawaida wa majibu ,  kuwa na vikaratasi  ama kubadilishana vikaratasi. “Mtu mmoja unakuta mitihani  yake ya majibu ina miandiko zaidi ya 10, na jeshi la polisi ndilo lililothibitisha kuwa miandiko ya wanafunzi hawa ilikuwa inatofautiana. Alisema pia kuwa, baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa nane walioandika matusi ya nguoni kwenye karatasi zao za majibu.  “Kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za majibu kinaonyesha utovu wa nidhamu, hivyo pamoja na kuwafutia matokeo ufuatiliaji zaidi unaendelea ili kuona hatua za kuwachukulia,” alisema Dk Ndalichako.

Pia alitoa onyo kali kwa vituo vilivyohusika na udanganyifu huo, huku akisema kwa vilivyobaika vitaandikiwa barua ya kutaka vijieleze kwa nini visifutiwe matokeo. Dk Ndalichako akielezea zaidi juu ya hali hiyo, alisema baadhi ya watahiniwa waliandika nyimbo za  kizazi kipya  (Bongo fleva) kwenye karatasi zao za majibu huku wengine wakichora michoro isiyo eleweka na wachezaji wa mpira. “Mwingine aliandika bongo fleva,  ngoja niwasomee ‘wasahihishaji msinisamehe..., acha utani na girl wangu, najukuja home nakukuta.. nikifeli mtihani naendelea na fani ya muziki,” Dk Ndalichako alisoma moja ya karatasi za majibu za watahiniwa hao huku akiruka baadhi ya maeneo akisema ameandika matusi yasiyoweza kusomeka.
Ubora wa ufaulu kwa jinsi  
Dk Ndalichako  alisema  ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa, jumla ya watahiniwa 33,577 sawa na asilimia 9.98 wamefaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu.

“Wasichana waliofaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu ni 10,313 sawa na asilimia 7.13 na wavulana ni 23,267, sawa na asilimia 12.13,” alisema Dk Ndalichako. Aliongeza kwamba,  waliopata daraja la nne ni 146,639 sawa na asilimia 43.60 ambao wavulana ni  87,039 sawa na asilimia 45.40 na wasichana 59,600, sawa na asilimia 41.22. Dk Ndalichoka aliongeza kwamba,  waliofeli ni 0156,089  sawa na asilimia 46.41, kati yao wavulana wakiwa 81,418 sawa na asilimia 42.47 na wasichana wakiwa 74,667, sawa na asilimia 51.64. mwisho

No comments:

Post a Comment