Friday, February 3, 2012

Wabunge CCM waisulubu Serikali ya JK


WAUNGANA NA CHADEMA KUKWAMISHA HOJA ZA WAZIRI MKULO NA JAJI WEREMA
Midraji Ibrahim, Dodoma na Boniface Meena, Dar
WABUNGE wa CCM jana waliongoza mashambulizi dhidi ya  Serikali na kufanikisha kuondolewa kwa hoja mbili zilizowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema.Hoja ya kwanza ya Serikali iliwasilishwa asubuhi na Waziri Mkulo ambaye alitaka Bunge liidhinishe punguzo la ushuru wa maji ya kunywa kutoka Sh69 kwa chupa hadi Sh12.

Jana jioni, Jaji Werema aliwasilisha hoja ya mabadiliko ya Sheria Mbalimbali ikiwamo ya Bodi ya Mikopo. Hoja hizo zote ziligonga ukuta na kuondolewa bungeni hadi mkutano ujao.

Mkulo

Akiwasilisha azimio hilo, Mkulo alisema kutokana na ongezeko la ushuru, maji ya chupa yamepanda kwa kiwango kikubwa, hivyo kuwafanya watumiaji wengi ambao ni wananchi wa kawaida kushindwa kumudu bei na kutumia maji ambayo siyo salama na kuhatarisha maisha yao.

“Ushuru wa bidhaa uliotarajiwa kukusanywa kwa kipindi cha Julai hadi Juni, 2012 kwa kiwango cha Sh69 kwa lita ni Sh15,549.3 milioni. Mapendekezo mapya ya kupunguza ushuru yatakusanya Sh2,704.2 milioni,” alifafanua  Mkulo.

Alisema punguzo hilo litasababisha nakisi ya Sh12,845.1 milioni na kwamba, kuanzia Julai hadi Desemba, mwaka jana tayari wamekusanya Sh6,730 milioni.

“Hivyo, kwa kutumia kiwango kipya cha Sh12 kwa lita, nakisi ya mapato itapungua kutoka Sh8,819.3 milioni hadi Sh7,719.3 milioni,” alisema.

Waziri Mkulo alipendekeza maeneo ya kuziba nakisi hiyo kuwa ni kupunguza posho, fedha zinazotumika kwenye makongamano, ununuzi wa magari, gharama za uendeshaji, ununuzi wa samani, mafunzo ya ndani na nje, safari za ndani na nje na ukarabati wa majengo.

Serikali hivi sasa inatumia Sh360 bilioni kwa ajili ya posho, kati ya fedha hizo, Sh14 bilioni zinahusu wabunge.

Mpango wa miaka mitano wa Serikali unaonyesha kupunguza posho na kutafuta njia bora za kulipana mishahara mizuri.

Wabunge

Hata hivyo, akichangia azimio hilo  Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inaonyesha wamekusanya mapato kwa asilimia 102, lakini makusanyo hayaonekani akidai kutolewa kwa maelezo ya ziada.

“Tuna matatizo ya madaktari, wanafunzi, tuna matatizo chungu nzima, fedha tulizoidhinisha kwenye bajeti hazipelekwi kwenye halmashauri, haituingii akilini,” alisema.

“ Kama una mapato ya ziada bado una matatizo, basi unahitaji maelezo ya ziada kuturidhisha,” alisema Hamad.

Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba (CCM), aliwashangaa baadhi ya wabunge kwa kuipongeza Serikali kwa usikivu wa kupeleka amri hiyo, huku akitaka waelezwe hasara iliyopatikana kwa ukaidi wa waziri kabla ya kupitisha.

“Kwanza waziri (Mkulo), angetuambia kwa nini alikaidi ushauri wa kamati na hasara ambayo taifa limepata, wenzangu wamesema ni usikivu, lakini mimi sioni zaidi ya ukaidi, huu siyo mwenendo mzuri. Ushauri wa wabunge unakuwa na nia nzuri,” alisema Dk Tizeba.

Dk Tizeba alishangaa marekebisho hayo kuhusu maji yanayozalishwa nchini pekee, ilhali mvinyo unaozalishwa nchini  unatozwa Sh420 kwa chupa na unaotoka nje Sh122 na kumtaka Waziri Mkulo,  atoe sababu ya mbao za nje kutozwa ushuru kidogo, huku mzigo zikibebeshwa zinazozalishwa nchini.

Alitaka TRA kuacha urasimu na ulegelege kutokana na kutotanua vyanzo vya mapato.

Mbunge wa Kalenga, William Mgimwa (CCM), alihoji iwapo maeneo yaliyopendekezwa kupangwa kwa ajili ya kufidia nakisi hiyo yalikuwa na ziada na kwamba, kama hakuna basi ni matatizo.

“Kama TRA inakusanya asilimia 102 na kuna upungufu wa fedha, basi kuna tatizo na tunahitaji maelezo maana tuna takwimu za makusanyo, lakini hakuna maelezo ya matumizi,” alisema Mgimwa.

Wengine waliochangia hoja hiyo ni Henry Shekifu (Lushoto), Leticia Nyerere (Chadema-Viti Maalumu) na Zaria Madabida (CCM-Viti Maalumu).

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge, Mkulo aliwasihi wabunge kutokwamisha hoja hiyo na kwamba, tayari maeneo mengine yamepunguziwa kasma.

Baada ya Mkullo kujibu hoja, alisimama Dk Tizeba kwa kutumia kanuni ya 58, akitaka kutopitisha amri hiyo na kuitaka Serikali kwenda kuifanyia marekebisho mbalimbali.

“Punguzo hilo halitamsaidia mlaji wa kawaida zaidi ya wenye viwanda kama waziri alivyokiri ameandikiwa na wenye viwanda… kwa hiyo itanufaisha wenyewe,” alisema Dk Tizeba.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikataa matumizi ya kanuni hiyo kwa madai ilikuwa haihusiani na hoja hiyo na kuamua kutumia kanuni ya 69 (2), inayompa mamlaka Spika kuhoji wabunge wanaokubali na wanaokataa.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya kutumia kanuni hiyo, waliokataa hoja walishinda huku Ndugai akiitaka Serikali kwenda kujipanga upya.

Jaji Werema
Kwa upande wa Werema hoja yake ya Muswada wa Marekebisho  ya Sheria 17 ikiwamo ya Bodi ya Mikopo, iligonga mwamba baada ya wabunge kutaka uondolewe kwanza upungufu uliomo katika sheria hizo.

Hoja hiyo ilianza kukataliwa na mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile aliyesema wao kama Kamati ya Huduma za Jamii, wanapinga moja kwa moja muswada huo kwa kuwa kamati yao haikuhusishwa.

Alisema kwanza, Rasimu ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ambayo iko katika marekebisho hayo, italeta mgogoro zaidi kwenye vyuo vikuu nchini.

"Sheria hii inaleta ubaguzi kati ya watoto maskini na matajiri, hivyo mjadala huu uahirishwe hadi utakapopangwa upya. Naomba wenzangu mniunge mkono ili ijadiliwe katika kikao cha mwezi wa nne," alisema Dk Ndugulile na kisha kuungwa mkono na wabunge.

Wakati Ndugai akitafakari hilo alimtaka mbunge wa Viti Maalumu CCM, Angela Kairuki kuendelea kuchangia na alipomaliza, mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa alijaribu kuokoa jahazi kwa kutaka hoja ya Dk Ndugulile iondolewe ili waendelee  kujadili muswada huo.

Kitendo hicho kilimfanya mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) kumtaka Naibu Spika atoe mwongozo wa hoja ya kwanza iliyoungwa mkono na wabunge wengine.

Baada ya hapo alisimama Kaimu Mnadhimu wa Serikali, Dk Mary Nagu ambaye aliwaomba wabunge waiunge mkono hoja hiyo na kuwataka mawaziri wenzake kufanya hivyo, lakini pia jaribio hilo liligonga mwamba.

Kitendo hicho kilimlazimu Jaji Werema kusimama na kuwaeleza wabunge kuwa inawezekana suala la Bodi ya Mikopo likaondolewa lakini, kwa kuwa wabunge ndiyo wenye uamuzi wa kutunga sheria, waamue wao.

"Bado sijafukuzwa ujaji, huu ni mhimili muhimu sana, lakini kwa kauli zenu na tabia zenu tukienda hivi tunaweza kuuharibu. Nimekaa kwenye ujaji muda mrefu sijaona, najua kuna upepo unaendelea nje na ndani ya Bunge," alisema Jaji Werema na kuongeza: "…tuko tayari kupokea uamuzi wowote utakaotolewa unaoruhusiwa na kanuni," alisema Jaji Werema akiwa tayari kupokea mwongozo wa Spika.

Hata hivyo, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisimama na kumweleza Naibu Spika kuwa hoja iliyoko mbele ni moja ya kutokukubaliwa kujadiliwa kwa muswada huo hivyo aitolee uamuzi kama kanuni inavyotaka.

"Hoja ya Ndugulile ni ya marekebisho mbalimbali na ndiyo hoja pekee iliyoko kwenye mjadala. Kama hoja ina mashiko unatakiwa uwaulize wabunge waamue. Hoja iondolewe kwa mujibu wa Kanuni ya 90  inayotaka iondolewe yote," alisema Lissu.

Baada ya hoja ya Lissu, Ndugai alisimama na kueleza kuwa kanuni hiyo inataka mbunge anapotaka ifanyike hivyo ataje iahirishwe mpaka lini na kwa sababu gani kitu ambacho alieleza kuwa Dk Ndugulile alikitimiza.

"Kutokana na hilo nitawahoji wanaokubali waseme ndiyo na wasiokubali waseme siyo," alisema Ndugai.

Wabunge waliokubaliana na Dk Ndugulile walikuwa wengi hivyo Ndugai aliahirisha hoja hiyo hadi mkutano ujao wa Bunge  hapo Aprili.

No comments:

Post a Comment