Saturday, February 4, 2012

Dk Magufuli kutowasamehee makandarasi wazembe


WAZIRI wa Ujenzi Dk John Magufuli ametangaza kiyama kwa wakandarasi wote wanaofanya kazi kwa uzembe na chini ya kiwango kuwa hatakuwa na msalia mtume nao.

Dk Magufuli aliyasema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge Ismail Rage (Tabora Mjini-CCM), ambapo alisema hana kigugumizi wala huruma kwa watu wa aina hiyo.

“Mpaka sasa nimeshafukuza Wakandarasi 2059, hivyo nasema na wengine ambao ni wazembe na wanaofikiria kucheza na kazi basi wakae mkao wa kula, lazima nitawatimua,’’alisema Magufuli.

Katika swali lake Rage alitaka kujua ni kwa nini ujenzi wa barabara za Tabora na Nzega-Tabora,Tabora-Manyoni na Tabora-Urambo unakwenda kwa kusuasua zaidi.

Rage pia aliitaka Serikali kutoa tamko la lini barabara za lami zitakamilika katika mkoa wa Tabora ambao kwa muda mrefu umekosa barabara nzuri.

Waziri alisema kusuasua kwa ujenzi barabara za Tabora kulichangiwa na mambo mengi yakiwamo kuchelewa kwa makandarasi kufanya upembuzi na kuchelewa kupatika kwa fedha kwa wakati.Alisema tatizo hilo hivi sasa limepungua kwa kuwa Serikali imeshapata fedha za kuanzia malipo ya wakandarasi hao ambapo jumla ya Sh 45 zimelipwa.

Alisema kuwa kwa hali hiyo sasa makandarasi hawatakuwa na kisingizio tena cha kuanza kwa kasi ujenzi wa barabara hizo ambazo hadi ujenzi wake utakapokamilika zitagharimu Sh 453 bilioni.

No comments:

Post a Comment