Wednesday, February 15, 2012

Wachina kujenga majengo 7 UDSM

KAMPUNI tatu za China leo zinaanza ujenzi wa majengo saba ya vitivo vya Sayansi na Teknolojia vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani, kwa gharama ya Sh bilioni 28.

Ujenzi huo unafanyika chini ya mradi wa Benki ya Dunia uliotoa jumla ya Sh bilioni 65 kwa chuo hicho.

Fedha nyingine zinatumika kuwasomesha walimu na kununua vifaa vya maabara na maktaba.

Makabidhiano ya ujenzi huo yalifanyika jana chuoni hapo kwa kampuni hizo tatu ambazo ni CRJ Company, Group Six International Company na HAINAN International Company kuoneshwa maeneo ya ujenzi.

Mtaalamu wa Manunuzi wa Mradi wa Benki ya Dunia chuoni hapo, John Kafuku alisema lengo la mradi huo ni kujenga uwezo kwa walimu, kuongeza nafasi za kusomea na vifaa kwa wanafunzi wa sayansi na teknolojia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ujenzi huo, Kafuku alisema utakamilika katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa na majengo yatajengwa kwa urefu wa kuanzia ghorofa mbili hadi nne.

“Ujenzi unafanyika chini ya umiliki wa vitivo mbalimbali ikiwemo elimu, uhandisi, elimu ya sayansi, teknolojia ambavyo vinahusika na sayansi na uhandisi (teknolojia), lengo ni kuongeza uwezo kwa walimu na wanafunzi,” alisema Kafuku.

Akifafanua matumizi ya fedha hizo, mbali na Sh bilioni 28 kutumika kwa ujenzi huo, Sh bilioni 18 zitanunua vifaa na Sh bilioni 17 zitasomesha walimu 117.

Kafuku alisema kati yao, walimu 61 watasomeshwa Shahada ya Uzamivu (PhD) na 59 watasomeshwa Shahada ya Uzamili.

“Tunategemea kesho (leo) ujenzi utaanza kwa kuona makatapila katika maeneo husika, ujenzi wote unafanyika hapa hapa kampasi kuu,” alisema Kafuku.

No comments:

Post a Comment