Friday, February 3, 2012

Maharamia wachoma moto boti ya doria

Na Mashaka Mhando, Muheza

MAHARAMIA wanaofanya uvuvi haramu katika mwambao wa Bahari ya Hindi, mkoani Tanga, wameichoma moto boti ya doria inayomilikiwa na Taasisi ya Hifadhi kwenye Bahari ya Silikanti, iliyopo katika Kijiji cha Kigombe, wilayani Muheza.


Uchomaji huo umechangiwa na boti hiyo kufanya doria ya mara kwa ili kuwasaka maharamia wanaofanya uvuvi haramu wa kutumia mabomu na nyavu ndogo zisizoruhusiwa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Mwambi Haji, aliyasema hayo juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Luteni mstaafu, Bi. Chiku Gallawa, aliyekwenda kijijini hapo kupata maelezo ya tukio hilo na kuongeza kuwa, hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa.

Mhifadhi wa Bahari ya Silikanti Bw. Sylevester Kazimoto, alisema mwaaka 2001, walifanya doria 192 katika bahari hiyo na nchi kavu iliyohusisha vyombo vya dola na kuwezesha kukamatwa kwa wavuvi haramu sita.

Alisema pamoja na kuwakamata wavuvi hao, pia walikamata vifaa
vinavyotumia ambavyo ni baruti 29, bunduki 17 za kuulia samaki, mitungi 31 ya kuzamia, makokoro 94, nyavu za utale 11 na samaki wa baruti kilo 124.

Akizungumza katika mkutano na wananchi kwenye ofisi za hifadhi hiyo, Bi. Gallawa alisema kila mmoja wao ana jukumu la kulinda na kuhifadhi rasilimali za bahari.

Aliwataka wataalamu wa hifadhi hiyo, wakishirikiana na Serikali ya kijiji kuandaa mpango wa kuorodhesha wavuvi wote, boti zao na kuziandika namba.

“Suala la uvuvi haramu linapaswa kupigwa vita baada ya kuachwa muda mrefu bila wahusika kuchukuliwa hatua, uvuvi wa aina hii unaharibu mazingira,” alisema Bi. Gallawa.

Hata hivyo, mjumbe wa Serikali ya kijiji hicho Bw. Hassain Bakari, alimtaka Bi. Gallawa kukomesha uvuvi huo kwani kesi nyingi zinazowahusu wahusika wa vitendo hivyo, zinaishia polisi na mahakamani.

Hali hiyo inachangia wavuvi hao kutawala mwambao wa bahari kwa kufanya vitendo hivyo wakiamini hata wakikamatwa kesi zao zitakwisha bila kuchukuliwa hatua.

No comments:

Post a Comment