Monday, February 13, 2012

Wapinzani wamtaka Pinda aachie ngazi


VYAMA vya siasa vya upinzani, vimemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ajiuzulu kwa maelezo kuwa vitisho vyake kuhusu matumizi ya vyombo vya dola  katika kushughulikia mgomo wa madaktari nchini, vilichochea maafa.Matakwa hayo ya vyama vya upinzani, yamekuja siku kadhaa baada ya Pinda kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa kufuatia mgomo huo uliomalizika wiki Alhamisi iliyopita.


Akitangaza hatua huyo, Waziri Mkuu alisema inalenga katika kutoa nafasi kwa vyombo vya dola kuwachunguza maofisa hao kwa tuhuma zinazowakabili.

Tuhuma hizo ni pamoja na kuingiza nchini vifaa duni vya kupimia virusi vya Ukimwi kutoka Korea kusini, utata katika zabuni ya kampuni inayofanya usafi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na zabuni za sare za madaktari na wauguzi katika hospitali hiyo.

Lakini jana, wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya Chadema, CUF, SAU, CCK, na TLP walisema, haitoshi kuwasimamisha Nyoni na Dk Mtasiwa pekee na kwamba kuna haja kwa Waziri Mkuu naye ajiuzulu.
Walisema Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa katika kulishughulikia mgomo huo  na kusababisha uchukue muda mrefu na matokeo maafa kwa watu wasiokuwa na hatia.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema  kilichotokea katika sakata hilo kinaonyesha jinsi namna Serikali ilivyo dhaifu na inavyoshindwa kujisimamia.

Alisema pia kushinda kuupatia mgomo huo suluhu ya haraka,  kumeonyesha jinsi Waziri Mkuu alivyoshindwa kuwajibika katika nafasi yake.
Mbowe alisema uongozi wa busara na hekima ulipaswa kuchukua nafasi katika kushughulikia mgomo huo na kwamba kwa msingi huo, hakukuwa na sababu kwa Pinda kutoa vitisho kwa madaktari.

Kiongozi huyo wa Chadema alisema madaktari  walikuwa na hoja  za msingi na kwamba kitendo cha Pinda kuwatishia kiliwakatisha tamaa.
Mbowe alisema si vizuri mambo ya kitaalam kushughulikiwa kisiasa kama ilivyofanywa na Serikali.

Kwa mujibu wa Mbowe, wazoo la kujiuzulu linapaswa pia kufanywa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda ambaye wakati mgogoro unaanza, alikuwa likizo jimboni kwake na ilimchukua wiki nzima kurudi jijini Dar es Salaam kushughulikia mgomo huo.

"Huu ni udhaifu mkubwa wa kiutendaji na mbaya zaidi waziri Pinda kaamua kuwasimamisha kazi katibu mkuu na mganga mkuu baada ya shinikizo la bunge na wala si vingine. Naamini hivi kwa sababu kwake suala hilo lilifika akatumia vitisho kisha akaagiza madaktari wa jeshi kwenda kuchukua nafasi za madaktari wa Muhimbili na mwisho wa siku ikabidi azungumze nao," alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi hao wanaendelea na utamaduni uliozoeleka serikalini wa  kusubiri maafa na baadaye kuchukua hatua.

 Alisema mtindo huo unatokana na tabia ya kulindana iliyoota mizizi katika Serikali ya CCM.
"Kamati ya Bunge ya Huduma za  Jamii, ilisafiri kutoka Dodoma hadi Dar es Saalam na kuzungumza na madaktari, wizara ya fedha na wadau wengine na ikarudi na kukutana na uongozi wa Bunge na baadaye ndio Pinda akachukua hatua za kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu na Mganga wa Mkuu wa Serikali," alisema.
Alisema Pinda anapaswa kujiuzulu kwa sababu busara yake ya  kuwatisha madaktari na kuwapeleka wanajeshi Muhimbili imechangia kuua  baadhi ya wagonjwa.

"Udaktari kulingana na kanuni zake kama usipoufanya kwa mwaka mmoja, ni lazima usome tena walau kwa mwaka mmoja kabla ya kutoa huduma, hivyo haina shaka kabisa kuwa wastaafu wa JWTZ waliopelekwa Muhimbili wamechangia vifo vya baadhi ya wagonjwa," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SAU, Paul Kyara alimtaka Pinda awajibike kwa kujiuzulu kwa maelezo kuwa alitumia vitisho badala ya kutafuta muafaka katika kushughulikia mgomo.
"Pinda aliwatisha madaktari badala ya kuangalia jinsi ya kutatua tatizo. Sasa kilichotokea kitachochea migogoro zaidi serikalini," alisema Kyara.
Kyara alielezea wasi wasi wake kuwa huenda Waziri Mkuu hana washauri wazuri na kusisitiza kuwa kimsingi, hakupaswa kutoa kauli ya vitisho kwa madaktari.

Alisema badala yake kiongozi huyo alipaswa kuwatia moyo madaktari na kuonyesha kuhusika kwake katika madai yao kama alivyofanya baadaye.
"Serikali iache siasa katika masuala ya kitaaluma na yale yanayohitaji utaalamu. Lakini haya yanayotokea yanachangiwa na kulindana na kupachikana katika nafasi ambazo kimsingi, waliowekwa hawana uwezo," alisema Kyara.


Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa, aliirushia kombora Idara ya Usalama wa Taifa kwamba imeonyesha udhaifu unaomfanya Waziri Pinda aonekane kuwa hatoshi katika nafasi yake.
“Inaonekana kuna tatizo katika vyombo vya usalama kwa sababu wao walipaswa kuliona jambo hili na kumshauri Waziri Mkuu bila kuegemea upande wowote lakini, hawakufanya hivyo na ndio maana akawa na kauli mbili tofauti katika suala moja," alisema Mnyaa.

Mbunge huyo alisema vyombo hivyo vina wajibu wa kuzuia mambo hayo kabla hayajatokea lakini, hawakufanya hivyo matokeo yake wanamweka Pinda katika wakati mgumu.

Katibu Mkuu wa CCK Renatus Muabhi, alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeonyesha udhaifu mkubwa katika kipindi chote cha mgomo wa madaktari.
 Alisema katika kipindi hicho Rais Kikwete alikuwa nje ya nchi na kwamba hata aliporudi aliona bora aende katika uzinduzi wa tawi la benki mojawapo ya kigeni, badala ya kushughulikia roho za wapiga kura wake.
"Wananchi ndio wamemchagua na matibabu ni sehemu ya haki yao ya kikatiba lakini, Kikwete kawapuuza na kwenda kufungua vitega uchumi vya wawekezaji ambao pia wanalaumiwa kwa kufilisi uchumi wa nchi," alisema Mhabi.
Katibu huyo alisema ni vema Rais Kikwete akawaomba radhi Watanzania katika kile kilichotokea katika mgomo huo, vikiwamo vifo vya wapiga kura.

Alisema vinginevyo awajibike kwa kujiuzulu na waziri mkuu wake, Pinda.
"Kisiasa kifo cha mtu mmoja ni kashfa kubwa sana kwa Serikali iliyopo madarakani kwa hiyovifo vya makumi ya wapiga kura wa chama kilichopo madarakani kutokana na mgogoro wa Serikali na watendaji wake si jambo la kuacha kama lilivyo, waombe radhi au wajiondoe," alisema Mhabi.

Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya vyama vya upinzani, Katibu wa  Itikadi  na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye simu yake iliita na kuikata na kisha kutaka atumiwe ujumbe wa maandishi.

Katibu majibu yake kwa ujumbe aliotumiwa, alisema hayupo katika mazingira mazuri ya kuzungumzia hayo.

"Nipo katika kikao cha NEC siko katika position (nafasi) ya ku-comment (kutoa maoni),” alijibu Nape kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.

Mgomo huo uliodumu kwa zaidi ya wiki mbili unadaiwa kusababisha vifo vya baadhi ya wagonjwa katika hospitali tofauti nchini.

Hata hivyo ulimalizika baada ya Waziri Mkuu, kukutana na madaktari na kuwasimamisha kazi  Dk Mtahsiwa na  Nyoni.

Hatua hiyo ilikuja baada ya madaktari hao kukaidi amri ya Pinda ya kuwataka madaktari kurejea kazini mara moja la sivyo watakuwa wamejifukuzisha kazi na kuendelea na mgomo hadi alipokutana nao na kutangaza kuwasimamisha viongozi hao wa wizara.
Awali Pinda aliwataka madaktari waliokuwa katika mgomo kurudi kazini mara moja na kwamba vinginevyo, watakuwa wamejifuuzisha kazi wenyewe.

No comments:

Post a Comment