Saturday, February 4, 2012

Waziri Nahodha apigwa mawe Mbeya


ALIKUWA KATIKA ZIARA YA CHAMA MBEYA, ASHANGAA VIJANA KUMPIGA, AAGIZA POLISI WAWASHUGHULIKIE
Stephano Simbeye, Tunduma.
 WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, jana alionja 'joto ya jiwe' baada ya msafara wake kupigwa mawe alipokuwa kwenye ziara ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya.Tukio hilo la tatu kwa viongozi wa Serikali kushambuliwa mkoani Mbeya, lilitokea eneo la Soko la Tunduma (Kisimani), wilayani Tunduma.

Habari zilieleza kuwa tukio hillo lilitokea wakati Waziri huyo na msafara wake walikuwa wanapita kuelekea ofisi za CCM Kata ya Tunduma ambako alitakiwa kufanya mkutano wa hadhara.

Ilikuaje?

Dalili za machafuko zilianza wakati msafara huo unapita kwa baadhi ya vijana wanaofanya biashara ya kubadilisha fedha sokoni hapo kuanza kujipanga barabarani wakizomea na kupiga miluzi.

Wengi wa vijana hao walisikika wakilaumu kitendo cha Waziri huyo wa Mambo ya Ndani kutumia magari ya Serikali katika msafari wake wa kichama.

"Haya ni matumizi mabaya ya mali za umma," alisikika akisema mmoja wa vijana hao.

Vijana hao walianza kumzomea waziri huyo huku baadhi wakirusha mawe kabla ya kudhibitiwa na polisi waliokuwa wanasaidiana na walinzi wa CCM maarufu kwa jina la Green Guard.

Katika sekeseke hilo vijana wawili walikamatwa na kukabidhiwa katika Kituo cha Polisi cha Tunduma.
 
Hata hivyo, Mkuu wa kituo hicho ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa yeye sio msemaji wa polisi, alikiri kuwapokea vijana hao na kueleza kuwa wanaendelea kuwafanyia mahojiano.

Mmoja wa vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Yusuf Haonga alisema wamechukua hatua hiyo kwa vile Waziri huyo aliwachanganya kwa kutumia magari ya Serikali akiwa kwenye ziara ya chama.

“Hawa wanatuchanganya, inakuwaje wanatumia rasilimali za nchi kwa kazi za chama. Pesa hizo si zingetumika kuhudumia wagonjwa waliolala mahosipitalini badala yake wanazitumia wao,”alisema Haonga.

Haonga alisema kuwa kitendo cha Waziri akiwa mtumishi wa umma kufanya ziara ya kichama kwa magari ya Serikali, kiliwakera na waliamua kumtupia mawe ili kutoa onyo kwa viongozi wengine wa Seriakali.

Hata hivyo, habari zingine zilieleza kuwa vijana waliomrushia mawe Waziri huyo ni wafuasi wa Chadema.

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vijana wakiwa na bendera za chama hicho cha upinzani ambao pia walikuwapo kwenye msafara huo uliomalizikia kwenye mkutano huo wa hadhara.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alipopulizwa kuhusu tukio hilo alihoji "Unataka niseme nini? Mimi niko Dar es Salaam na tukio hilo limefanyika Mbeya."

Aliendelea, "Ndio kwanza unaniambia (mwandishi). Inabidi nijue nini kilitokea na kama kweli ni vijana wa Chadema nijue walikasirishwa na nini."

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu," Sina taarifa."

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo, Abbas Kandoro jana alishindwa kuzungumzia tukio hilo kwa kile alichoeleza kuwa yuko kwenye safari ya kikazi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliohutubiwa na Nahodha, mwenyekiti wa CCM Kata ya Tunduma, Daniel Mwashiuya alisema kuna kikundi cha watu ambacho kimeanza kupoteza amani ya mji wa Tunduma kutekeleza matakwa yao ya kisiasa.

Alisema “mazingira tunayokwenda nayo kwa sasa si mazuri kwa ustawi wa mji wetu hivyo Wanatunduma tujiepushe na kuvunja amani tuliyoizoea ili isije ikapotea,” alisema

Kauli ya Waziri Nahodha

Akihutubia mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo, Waziri Nahodha alisema hajapendezwa tukio hilo na kuhoji, "Kama limefanyika kwangu hali ikoje kwa watu wengine?"

Alisema kamwe hawezi kuacha hali hiyo ya uvunjifu wa amani iendelee na kuiagiza polisi mkoani Mbeya kuchukua hatua haraka dhidi ya kikundi hicho cha watu aliowaita wahuni.

Waziri Nahodha pia amepiga marufuku biashara haramu ya kubadilisha fedha katika eneo hilo.

Alisema mtu anayetaka kuendelea kufanya kazi hiyo itabidi afuate taratibu zinazotakiwa ili aweze kuihalalisha biashara yake.

“Sokoni pana biashara za aina mbalimbali zilizo halali na haramu, lakini nawaagiza polisi chini ya Kamanda wenu wa Mkoa, mkae muangalie namna ya kurejesha amani mahali hapo. Sasa likizo basi,” alisema Nahodha.

Waziri Nahodha alisikitishwa na taarifa za kuendelea kuvunjika kwa amani katika mji wa Tunduma ambapo aliwataka wananchi wa mji huu kuthamini amani iliyojengeka kwa muda mrefu.

Aliwataka wasidhani kwamba amani iliyopo imeshuka kutoka Mbunguni na kwa sababu hiyo wao wenyewe wailinde na kuidumisha kwa kushirikiana na polisi kwa njia ya ulinzi shirikishi.

Historia ya matukio

Hili ni tukio la tatu kwa viongozi wa kitaifa kuzomewa katika mji wa Tunduma ambapo mwaka 2010, mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, alizomewa katika eneo hilo alipokuwa akipita kutokea mkoani Rukwa katika ziara za kampeni za uchaguzi.

Mwaka 2009, Mwenge wa Uhuru ulilazimika kubadili njia ghafla kufuatia dalilili za uvunjifu wa amani.

Tukio jingine ilikuwa ni Oktoba, 2008, ambapo msafara wa Rais Jakaya Kikwete kushambuliwa kwa mawe kwenye kijiji cha Kanga, wilayani Chunya.

Tukio hilo lilitokea katika Kijiji hicho wakati msafara wa Rais ukiwa njiani kuelekea Mbeya mjini ukitokea mji wa Mwakwajuni wilayani Chunya ambako alikuwa amefanya ziara.
Kwa mujibu wa habari hizo magari sita yaliyokuwa kwenye msafara huo yalishambuliwa kwa mawe na baadaye vijana kadhaa walikamatwa.

Ilidaiwa kuwa waliofanya tukio walikuwa wamejipanga pembeni mwa barabara na baada ya magari manne ya mwanzo kupita, likiwamo la Rais Kikwete, ndipo mawe yalianza kuvurumishwa.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa wananchi hao walikasirishwa na  kitendo cha kushindwa kumwona Rais Kikwete baada ya kumsubiri kwa muda mrefu ili awahutubia na kusikiliza kero zao.

No comments:

Post a Comment