MZEE wa jijini Mbeya, Sadick Salehe, mkazi wa mtaa wa Ilolo Kata ya Luanda, anashikiliwa na Polisi baada ya wakazi wa mtaa anaoishi kukasirishwa na hatua yake ya kukaa ndani na mwili wa mwanawe kwa siku saba na majirani kujenga hisia za kuwa huenda alimwua.
Hisia za wakazi hao zilikuja baada ya kuoanisha kifo hicho na cha mkewe kilichotokea miaka ya themanini, ambapo mzee huyo alimwua kwa kumkata mapanga na kuficha maiti kwenye uvungu wa kitanda kwa siku nne huku akiendelea kulalia kitanda hicho.
Ilielezwa, kuwa tukio la mauaji ya mkewe, lilikuja kubainika baada ya majirani kubaini zimepita siku nyingi hawamwoni mkewe huyo na walipomwuliza hakuwa na jibu la kuwaridhisha hivyo ikawalazimu waombe uongozi wa mtaa upekue ndani ya nyumba hiyo na ndipo wakakuta mwili huo uvunguni na akashitakiwa na kutumikia kifungo cha miaka minane jela.
Akizungumzia tukio la jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ilolo, Benson Mbwana, alisema juzi akiwa katika mizunguko yake ya kawaida, alipigiwa simu na mkazi wa mtaani hapo ambaye alimjulisha kuwapo tatizo la kushitua nyumbani kwa Mzee Salehe.
Mbwana alisema baada ya kwenda eneo la tukio saa 12 jioni, alimkuta Salehe akiwa na viongozi wa Msikiti wa Soweto, wakijadiliana, na alipouliza akapelekwa katika chumba chenye mwili wa kijana huyo; Salehe Sadiki (38).
Alisema mwili huo ulikuwa umeharibika hali iliyodhihirisha kuwa kijana huyo alifariki dunia muda mrefu na baada ya kumwuliza mzee huyo, akasema aligundua kifo hicho alipoingia katika chumba cha mtoto wake akifuata beseni ili aweke maji.
Jambo lililowashitua wengi ni kuwa eneo la kuzunguka nyumba hiyo lilikuwa na harufu kali hali iliyowafanya wahisi kuwapo mzoga wa mnyama ndani ya nyumba hiyo, lakini wakashindwa kwenda kumhoji mzee huyo, kwa kuwa hakuna jirani ambaye amekuwa akiingia nyumba hiyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa Mtaa alisema pamoja na harufu hiyo kali, bado mzee huyo ambaye yuko kwenye Mfungo wa Ramadhani, siku zote hizo aliendelea kupika na kula karibu na mlango wa chumba chenye maiti bila kujua mtoto wake alipo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti baada ya Mzee Salehe kuulizwa, alisema alionana kwa mara ya mwisho na mtoto wake, ambaye alikuwa kiafya amedhoofu kwa muda mrefu.
Jumatano wiki jana na baada ya hapo hakujua yuko wapi, hivyo akabaki na hisia ya kuwa kijana huyo alikuwa kwa wenzake.
“Tulimwuliza unatambua kuwa kijana wako, alikuwa anaumwa na hakumwona kwa siku
hizo zote, iweje usifungue mlango wa chumba hicho kumwangalia. Akajibu kuwa
walikuwa wakiishi kila mmoja na zake, hivyo hata alipokuwa hamwoni hakushtuka,”
alisema.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya kuona hayo, aliliarifu Jeshi la Polisi na baada ya askari kufika hapo saa mbili usiku walishindwa kuuchukua mwili kwakuwa ulikuwa umeharibika kiasi cha kupasuka na kila kiungo kilichoshikwa kilikuwa kikinyofoka.
Kufuatia hasira ya wakazi wa eneo hilo ililazimu Jeshi la Polisi kuondoka na mzee huyo, hivyo hakushuhudia maziko ya mwanawe huyo jana kwenye makaburi ya Isanga yakiendeshwa na Serikali ya Mtaa wa Ilolo.
Gazeti hili jana lilifika eneo la tukio na kukuta vijana na wakazi wengine wakitoka makaburini kuzika lakini hali katika chumba alimokuwa maiti bado ilikuwa mbaya kutokana na harufu kali.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Anaclet Malindisa, alikiri kumshikilia Sadiki kwa kuhofia usalama wake na kuongeza kuwa mtuhumiwa huyo anaonekana anasumbuliwa na matatizo ya akili.
No comments:
Post a Comment