Monday, August 22, 2011

Kisa na mkasa na Salim Kikeke

ALITAMANI GEREZA..

Wahalifu hugonga vichwa vya habari wakitoroka gerezani, lakini safari hii, bwana mmoja amezua tafrani baada ya kukutwa akijaribu kuingia jela kwa njia za wizi.
Jela
Gereza..

Bwana huyo, Marvin Ussery alionekana akijaribu kunyata kuingia katika gereza kuu la California, huko Sacramento.

Gazeti la Metro limesema bwana Marvin aliwahi kufungwa jela, lakini katika gereza jingine la New Folsom na kauchiliwa huru mwaka 2009.

Hata hivyo hivi juzi afisa magereza Sajini Tony Quinn alimkuta Marvin akiparamia ukuta wa gereza wenye urefu wa futi saba, ukiwa na senyenge zenye ncha kali, akijaribu kupenya na kuingia gerezani.
Maafisa bado wanajikuna vichwa kujiuliza kwa nini alikuwa anataka kuingia gerezani. Maafisa wanahisi labda alikuwa akitaka kuingia na dawa za kulevya, au kupeleka simu za mkononi gerezani, ingawa hakuna ushahidi wowote kuhusu hilo hadi sasa.

Lakini iwapo nia yake hasa ilikuwa kurejea gerezani, basi, ndoto yake imekuwa kweli, kwani bwana huyo kwa sasa anazuiliwa katika jela ya Sacramento, kwa kosa la kuwepo karibu na gereza, wakati yeye ni mhalifu wa zamani.
Sajini Quinn amesema, bwana huyo aliwaambia kuwa alitaka kurejea gerezani kujikumbusha hali ya gereza.

MWANA MASHITAKI MAMA

Mtoto mmoja mwenye umri wa miaka kumi na moja nchini Ujerumani, amepiga simu polisi kumshtaki mama yake kwa kumfanyisha kazi za nyumbani.
Mama
Mama aitiwa polisi
"Hello, mama yangu ananifanyia kazi za nyumbani kwa nguvu" amesema kijana huyo alipopiga simu polisi.
Mtandao wa news.com umesema kijana huyo aitwaye Leon yuko katika likizo yake baada ya shule kufungwa.

Polisi wamemuuliza ni kazi gani hasa analazimishwa kufanya? "Natakiwa kusafisha kibaraza cha nyumba, nafanya kazi siku nzima" amelalamika kijana huyo.
Mama wa kijana huyo, amewaambia polisi kuwa mtoto wake amekuwa akitishia kumshtaki kwa polisi kwa wiki kadhaa sasa.

"Sasa hivi ameambiwa aokote makaratasi kidogo, ndio akaamua kupiga simu polisi" amesema mama huyo. "yaani yeye hucheza siku nzima, ukimwabia asafishe chumba chake tu, anaanza kusema analazimishwa kazi" amesema mama huyo.
Polisi katika mji wa Aachen lilipotokea sakata hilo wamefunga kesi hiyo.

ELIMU NGUMU..

Wanafunzi wa chuo kikuu nchini Sierra Leone wameshindwa kufanya mitihani yao ya mwisho kutokana na kukosekana kwa karatasi.
eXAM
Wanafunzi wakifanya mtihani... sio wa Sierra Leone lakini..

Mkuu wa chuo hicho, Fourah Bay College, Profesa Thomas Yormah amewaambia wanafunzi wenye hasira wapatao elfu nne kuwa mitihani imeahirishwa hadi wiki ijayo, ambapo karatasi zitawasili.
"Ni aibu kwa jamii yetu" amesema mwanafunzi mmoja akizungumza na BBC. Mwezi Februari, mitihani ya muhula wa kwanza iliahirishwa kwa wiki mbili kwa kuwa madarasa hayakuwa na meza na viti.
Profesa Yormah ameiambia BBC kuwa kulikuwa na tatizo kidoogo katika kuandaa vijitabu vya mitihani, lakini ameahidi kuunda tume ya uchunguzi.

Taarifa kutoka Freetown zinasema nijambo la kawaida kuona wanafunzi wakiwa wamesimama hadi nje ya madarasa huku wakimsikiliza mhadhiri, au mara nyingine masomo huendeshwa nje ya madarasa.Ama kama ni darasani wanafunzi wenye bahati hukalia mabenchi...

MWIZI KUWA MWANARIADHA

Mwizi mmoja nchini Uchina alitoka mbio baada ya kufanya wizi, kiasi kwamba wanariadha wanamtaka mwizi huyo kwa ajili ya mbio fupi.
China
China wanataka kutumia uzoefu wa mwizi kuwa mwanariadha..

Mwizi huyo, Lei Pai, alionekana akikimbia mita mia moja na kumi kwa muda wa sekunde kumi na moja, baada ya kukwapua betri.

Picha za mwizi huyo akikimbia zilionekana katika kamera za ulinzi, maarufu kama CCTV.
"Ukizingatia alikuwa amevaa viatu vya kawaida na kasi aliyokimbia" amesema kocha wa riadha wa jimbo la Zhengzhou. Nadhani atatufaa sana, iwapo akielekezwa jinsi ya kukimbia na akipatiwa vifaa vinavyotakiwa, amesema kocha huyo wa jimbo la Henan.

BENKI YAFUNGWA NA KUFULI MOJA?..

Kisiwa kimoja kidogo katika bahari ya Pasifiki, ambacho kina umaarufu wa kuwa na makanisa mengi, kimepatwa na mshtuko baada ya kutokea wizi katika benki ya kisiwa.
dOLLARS
Haijajulikana kiasi gani kiliibwa..

Kisiwa hicho kiitwacho Aitutaki ni moja ya visiwa tulivu vya visiwa vya Cook, na ndio kwanza kimeshuhudia uhalifu wa kwanza kabisa wa wizi wa benki.
Meya wa kisiwa hicho John Baxter amesema haamini kuwa wizi huo umefanywa na wakazi wa kisiwa hicho. Kisiwa hicho kina wakazi elfu moja na mia nane.
Kamishna wa polisi Maara Tetava amesema kiasi kikubwa cha fedha kimeibiwa, lakini hakusema ni kiasi gani. Aidha pia aligoma kuthibitisha taarifa kuwa benki hiyo hufungwa na kufuli moja tu.

MGONJWA MAHUTUTI.. KUMBE PAKA

Madaktari wa dharura waliitwa katika nyumba moja hapa Uingereza baada ya kuambiwa kuna dharura ya ugonjwa wa moyo, na kukuta mgonjwa mwenyewe ni paka.
pAKA
Sio huyu lakini..

Huduma ya magari ya kubebgea wagonjwa ilipata simu kutoka kwa bwana mmoja na mke wake wakizungumza kwa hofu na majonzi wakisema kiumbe chao chenye umri wa miaka mitano kimepatwa na mshituko wa moyo. Gari la dharura lilipelekwa haraka katika nyumba hiyo, huku madaktari wakidhani ni mtoto mdogo.

Lakini walipofika, walikuta bwana na mke wake huyo wakiwa wamemshkilia paka wao-- ambaye baadaye alikufa.

Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema jinsi walivyoshtushwa na kushangazwa na tukio hilo. "Yaani hatukuamini tulivyokuta ni paka, na sio binaadam".

Na kwa taarifa yako...... Pua yako ina uwezo wa kukumbuka harufu elfu hamsini tofauti.
Tukutane wiki ijayo.... Panapo majaaliwa...

No comments:

Post a Comment