Safari ya matanuzi ya vigogo yazimwa
- Walikuwa waende Hong Kong kwa ziara ya siku 10
- Waziri Maige, Msekwa waipiga 'stop' dakika za mwisho
- Ingeteketeza mamilioni ya pesa za walipa kodi
- Walipanga kusafiri daraja la kwanza
Habari za uhakika ambazo Raia Mwema limezipata zinasema kwamba hatua yake hiyo imesaidia kuokoa Shilingi milioni 120 ambazo zingeteketea kama ziara hiyo ya siku 10, iliyoelekea kuwa ya kitalii zaidi kuliko ya kujifunza, ingefanyika.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu Waziri huyo kupiga marufuku kusafiri nje menejimenti ya mamlaka hiyo inayoongozwa na Mhifadhi Mkuu, Bernard Murunya kwa mwaka mzima baada ya kubaini kuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kusimamia shughuli za uhifadhi na utalii katika bonde hilo.
Uamuzi huo wa kumwekea “karantini” ya kutokusafiri nje ya nchi Mhifadhi huyo na wenzake kwa mwaka mzima, umekuja baada ya kubainika kuwa katika kipindi cha mwaka moja pekee, watendaji wa mamlaka hiyo na baadhi ya wajumbe wa bodi, wametumia mamilioni ya shilingi kwa safari za nje; huku wananchi wanaoishi ndani ya bonde hilo wakikabiliwa na njaa kali.
Maige alifikia uamuzi huo mgumu wakati alipofanya ziara ya siku mbili ndani ya Mamlaka hiyo kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi pamoja na miradi kadhaa ya maendeleo ambako alipokelewa kwa mabango na wananchi waliokuwa wakiilalamikia menejimentiya NCAA kwa kushindwa kuwahudumia kutokana na watendaji kusafiri kila mara.
Taarifa zilizolifikia Raia Mwema na kuthibitishwa na vyanzo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Pius Msekwa, wiki iliyopita, zilieleza kuwa Mhifadhi huyo alikuwa asafiri na ujumbe wa watu 12 wakiwamo wajumbe wanne wa Bodi, Agost 6, 2011, kwa ndege ya shirika la Emirates kwenda Hong Kong katika kile kinachoitwa kuwa ni “ziara ya kujifunza” shughuli za utalii nchini humo.
Habari zaidi zinawataja waliokuwa wasafiri kuwa ni pamoja na Mjumbe wa Bodi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala na kingozi wa msafara huo, Halima Mamuya. Mamuya alikuwa mbunge wa viti maalumu (CCM) kwa vipindi viwili kati ya mwaka 2000-2005 na 2005-2010 baada ya kushindwa katika kura za maoni.
Wajumbe wengine ni Mbunge wa Bukoba, Deogratius Ntukamazima, Mkurugenzi wa Bodi, Fatma Simba na Mhandisi George Kaidoh, Mhandisi Joseph Mallya na Veronica Ufunguo wa idara ya uhifadhi na utalii.
Wengine ni Mhandisi Ezra Misana, Meneja Utumishi na Raslimali Watu, Ringbert Marcos, Meneja Idara ya Fedha, Shadrack Kyambile, Naibu Meneja Huduma za Sheria, Yusuf Machumu na Meneja Uhusiano, Adam Akyoo.
Taarifa zinasema, hata hivyo, ya kuwa ndoto za ujumbe huo kusafiri nje zilizimwa baada ya Maige kutumiwa taarifa za safari hiyo na baadhi ya wafanyakazi wa ngazi za chini ambao walimtumia ujumbe wa simu (sms) waziri huyo na kumweleza siri ya safari hiyo.
Baada ya kupokea ujumbe huo, inaelezwa kuwa Maige aliwasiliana na baadhi ya watendaji wa Menejimenti ambao walijaribu kujenga hoja kuwa safari hiyo ilikuwa muhimu sana kwa maendeleo ya shughuli za utalii wa mamlaka hiyo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa Waziri Maige alikataa ushawishi huo, na ndipo alipompigia simu Mwenyekiti wa Bodi ya Ngorongoro, Mzee Pius Msekwa ambaye naye alimwagiza Mhifadhi Murunya na kiongozi wa msafara, Halima Mamuya kuvunja na kusitisha safari hiyo.
Akimkariri Waziri Maige, mtoa habari wetu alieleza kuwa Waziri alikuwa amekasirishwa sana na “kiburi” cha watumishi hao kupuuza maagizo yake aliyotoa mwezi uliopita kuwa hawataruhusiwa kusafiri nje ya nchi kwa mwaka mzima hadi watakapojirekebisha hasa katika kutekeleza majukumu ya kazi zao.
Aidha, imeelezwa pia ya kuwa Waziri Maige pia alipinga kuwa ziara za aina hiyo hazina tija kubwa kwa mamlaka hiyo zaidi ya kutafuna posho za mamlaka, kwani kazi ya kutangaza utalii ilitakiwa ifanywe na Bodi ya Utalii nchini (TTB) badala ya mashirika yanayoshughulikia usimamizi wa hifadhi kufanya kazi akitoa mfano wa NCAA na TANAPA.
Watoa taarifa wetu wameeleza pia kwamba kimsingi, Waziri Maige pia alikasirishwa na wingi wa wajumbe waliokuwa wanakwenda safari hiyo na ilionekana kuwa wanakwenda kutalii badala ya kwenda kujifunza kwa kuwa kuna baadhi ya ambao walikuwa wasafiri wasifu wao hauendani na shughuli za kutangaza utalii.
“Mzee Msekwa alipopata simu ya Waziri alitoa amri haraka na kuwaagiza watumishi hao kusitisha haraka safari hiyo na kuwaonya kuwa iwapo hawatatekeleza, basi, wangechukuliwa hatua za kinidhamu”, alieleza mtoa taarifa wetu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Taarifa zaidi zilizokusanywa na Raia Mwema zinaeleza kuwa ujumbe huo ungeteketeza kiasi cha dola za Kimarekani 72,200 ambazo ni karibu sawa na shilingi za Kitanzania milioni 120.
Dola moja ya Kimarekani kwa sasa hununuliwa kwa Shilingi kati ya 1,650 hadi 1,660 katika maduka mengi ya kuuzia fedha na bei hiyo hutegemeana na nguvu ya soko.
Katika safari hiyo, kila mjumbe wa bodi angelipwa posho ya dola za Kimarekani 6,000 wakati wajumbe wengine wangelipwa dola 5,600 ambazo ni karibu sawa na sawa na shilingi 9,240,000, na fedha hizo ni mbali na gharama za tiketi ya ndege ya daraja la juu (business class) ya kwenda na kurudi Hong Kong ambayo ingegharimu dola zaidi ya 1,500 kwa kila mjumbe.
“Kila mjumbe alikuwa alipwe posho dola za Kimarekani 5,600, na fedha hizo ni tofauti na gharama za tiketi za ndege ya shirika la Emirates, “ aliongeza mtoa habari wetu.
Takwimu zinaonyesha ya kuwa NCAA imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.4 kwa safari za nje ya nchi na watumishi hufanya safari 32 kwa mwaka ambazo ni sawa na wastani wa safari tatu kwa kila mwezi katika maeneo mbalimbali duniani kwa kigezo cha kutangaza utalii.
Mamlaka hiyo pia hutoa kiasi cha shilingi milioni 789 kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na shirika la TTB kama fedha za kutangaza utalii nje ya nchi na pia hutoa milioni 327 kwa ajili ya matangazo kwenye michezo ya Ligi Kuu ya mpira wa miguu ya Uingereza.
NCAA pia hutoa shilingi milioni 35 kwa ajili ya matangazo katika gazeti la US Today la nchini Marekani na Support Tourism Office iliyoko nchini Abudhabi (Falme za Kiarabu) shilingi milioni 24.
Matumizi ya fedha hizo hata hivyo yanakwenda kinyume na utafiti wa mtaalamu wa shughuli za Utalii nchini Dk.Victor Appolo Lunyoro aliyoipa kichwa cha habari Global Tourism Marketing Campaign, The case of Ngorongoro Conservation ya mwaka 2009 ambayo inaeleza kuwa ziara ya mafunzo au maonyesho huchangia asilimia mbili tu ya watalii wanaotembelea Bonde hilo.
Katika mchanganuo wake mtaalamu huyo anabainisha kuwa asilimia 34 ya watalii wanaotembelea Bonde hilo ni wale waliosikia kwa ndugu na jamaa zao waliokwishaku tembelea, asilimia 27.5 ni watalii wanaopata taarifa kupitia kwa kampuni za uwakala wa utalii, asilimia 17.9 hupata taarifa kupitia mitandao na tovuti mbalimbali, asilimia 1 kupitia vipeperushi, asilimia 0.2 maonyesho na nyinginezo asilimia 6.7.
“Kwa mchanganuo huo utaona kuwa bajeti ya matangazo ya mamlaka ni karibu shilingi bilioni 4 kwa mwaka na asilimia 70 ya fedha hizo hutumika kwa safari za nje ya nchi na ndiyo maana Waziri ameamua kuingilia kati kwani inaonekana kuwa kuna ufujaji wa fedha makusudi unaofanywa na watumishi na ndiyo sababu ya kumtumia Mwenyekiti wa Bodi Mzee Msekwa,” alieleza mtoa taarifa wetu.
Akizungumzia hatua hiyo ya kupiga “stop” safari hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Pius Msekwa alilithibitishia Raia Mwema kwa njia ya mawasiliano ya simu kuwa ni kweli wamefuta ziara hiyo ya kwenda Hong Kong kwa kufuatia maagizo ya Waziri Maige.
“Ni kweli safari imefutwa na hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri, na watumishi lazima watekeleze jambo hilo; vinginevyo watakuwa wanakwenda kinyume cha maagizo halali ya Serikali”, alisema Mzee Msekwa.
Msekwa, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alieleza kuwa hafahamu gharama halisi za safari hiyo lakini akaongeza kuwa fedha nyingi zingetumika kugharimia safari ya ujumbe huo.
“Sina takwimu sahihi za gharama hapa mbele yangu, lakini najua safari kama hizo zinatumia fedha nyingi ila kwa sasa hakuna safari na Waziri ameagiza, na maagizo yake yametekelezwa”, alisisitiza Msekwa.
Kwa upande wake, kiongozi wa msafara huo, Halima Mamuya, alikataa kuzungumzia nia na madhumuni ya safari hiyo; hasa wakati ambapo Waziri alikwishakutoa maelekezo kuwa safari za nje zifutwe ili kubana fedha za Mamlaka hiyo.
“Kwanza nani kakuambia taarifa hizo? Mimi sijui chochote. Waulize watu wa NCAA. Mimi ni mjumbe tu wa Bodi. Siwezi kuzungumzia masuala ya Menejimenti ya Ngorongoro”, alijibu Mamuya; huku akilaumu waandishi wa habari kwa kumfuatafuata.
Naye Msemaji wa NCAA, Adam Akyoo, alisema kua ni kweli safari hiyo imefutwa, lakini walikuwa wamefuata taratibu zote za kiserikali za mtumishi kusafiri nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kujaza fomu ya safari kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo na Idara ya Utumishi.
Akyoo alisema safari hiyo ilikuwa ya kawaida na nia na madhumuni yake ilikuwa kwenda kujifunza pamoja na kutangaza utalii katika maonyesho ya utalii na utamaduni huko Hong Kong barani Asia.
“Safari unayoizungumzia haikuandaliwa kwa kificho. Kila kitu kilikuwa wazi na taratibu zote za kiserikali zilifuatwa ikiwa ni pamoja na ujazaji wa fomu za safari ili kupata ruhusa”, alisema Akyoo.
Aliongeza kuwa, hata hivyo, Menejimenti inaheshimu hatua zilizochukuliwa na Waziri, na hawana kinyongo na hatua yake ambayo ina maslahi kwa ustawi wa Mamlaka yao na akasisitiza kuwa safari hiyo ilikuwa na uwazi wa kutosha na hakukuwa na upindaji wa sheria za utumishi.
Waziri Maige hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi kuelezea sababu za kusitisha safari ya wajumbe hao; kwani ilielezwa kuwa yuko mjini Dodoma akijiaandaa kuwasilisha bajeti ya Wizara yake ndani ya wiki hii.
Wachunguzi wa mambo wanaeleza kuwa fedha hizo – Shilingi milioni zaidi ya 120 ambazo zingetumika ndani ya siku 10 tu, zinaweza kutosha kununua tani 343 za mahindi ambazo zingewasaidia wananchi wanaokabiliwa na njaa kali ndani ya hifadhi ya Ngorongoro zingeweza kusaidia familia zenye njaa kwa zaidi miezi minne.
No comments:
Post a Comment