Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zinazozozana nchini Libya kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa visa vya uhalifu na vya kulipiza kisasi havitokei.
Wito huo umetolewa huku ripoti za ukiukaji wa haki za binadamu zikiibuka ambazo zinadaiwa kutekelezwa na pande hizo mbili, upande wa waasi na wanajeshi watiifu kwa Kanali Gaddafi.Msemaji wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu Rupert Colville amesema kuwa ni vigumu kuthibitisha ripoti hizo za mauaji na unyanyasaji wa watu.
''Tunawasihi wale wote walioko kwenye nafasi za utawala nchini Libya, ikiwa ni pamoja na makamanda wa jeshi, wachukue hatua za dharura kuhakikisha kuwa uhalifu au visa vya kulipiza kisasi havitekelezwi'', Muakilishi huo alisema.
Uhalifu unatekelezwa na pande zote
Shirika la kimataifa kuhusu haki za binadamu, Amnesty International limesema ''linaushahidi wenye nguvu'' wa uhalifu uliotekelezwa na pande hizo mbili pwani mwa mji wa Zawiya, ikiwa ni pamoja na madai ya ghasia zilizotekelezwa na waasi dhidi ya wahamiaji wa Afrika, waliodaiwa kuwa mamluki.Na Umoja wa Mataifa umekubali kutoa dola billioni moja na nusu amana ya Libya, baada ya kuondoa jina la baraza hilo la kitaifa (NTC), na badala yake kuweka kuwa pesa hizo zitaelekezwa kwa utawala mbadala nchini Libya.
Afrika Kusini ilikuwa imekwamisha hatua hiyo ikidai kuwa ilikuwa na wasiwasi kuwa iwapo Baraza la Mpito la Kitaifa (NTC) litapewa pesa hizo itamaanisha ni kuwatambua waasi hao kama utawala wa Libya, jambo ambalo Muungano wa Afrika haukuwa umekubaliana.
NTC kuhamisha makao yao
Baraza hilo la Mpito la Kitaifa(NTC) limetangaza kuwa linapanga kuhamisha makao yao makuu ya kisiasa kutoka ngome yao ya Benghazi hadi mji mkuu Tripoli.Mapigano bado yanaendelea mjini Tripoli, mji ambao kwa kiasi kikubwa unadhibitiwa na waasi.
Waasi hao sasa wanajaribu kufika mji wa Sirte, alikozaliwa Kanali Muammar Gaddafi, lakini wamekabiliwa na upinzani mkali.
Kulikuwa na taarifa kuwa ndege za kivita za NATO zilitekeleza mashambulio ya angani usiku kucha mjini humo.
No comments:
Post a Comment