Mikataba ambayo Chikawe na Malima wanataka kuingiza taifa inahusu uchimbaji wa madini aina ya kopa (Copper), wilayani Mpanda mkoani Rukwa na mradi wa madawa ya virutubisho kwa wagonjwa wa ukimwi – Secomet V.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, Chikawe na Malima wamepanga kutekeleza miradi hiyo miwili kupitia kampuni ya Lion of Afrika Ltd., ambayo mtendaji wake mkuu ni Abdurazak Ebrahim.
Mradi mwingine, uliopangwa na vigogo hao wa serikali, unahusu usindikaji wa nyama pamoja na maziwa. Taarifa zinasema Abdurazak Ebrahim mfanyabiashara mwenye uraia wa Afrika Kusini, anasifika duniani kwa “ushawishi,” na kwamba anafahamika sana ndani ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutokana na kubebwa na viongozi hao wawili.
MwanaHALISI limeelezwa tayari Malima “amenasa” katika mikono ya Abdurazak Ebrahim. Imeelezwa kuwa tarehe 27 Mei 2011 aligharamiwa usafiri kutoka Dar es Salaam hadi nchini Afrika Kusini, pamoja na malazi katika hoteli ya kimataifa ya Michelangelo iliyoko Cape Town. Aliondokea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la ndege la Afrika Kusini (South African Airways) Na. SA 323.
Ziara ya Malima nchini humo ililenga kufanikisha mradi wa kuchimba kopa wilayani Mpanda unaofanywa na kampuni ya Abdurazak Ebrahim. Uthibitisho wa malazi (Confirmation of Accommodation) wa uongozi wa hoteli ya Michelangelo kwenda kwa Malima, tarehe 9 Juni 2011, unaonyesha kiongozi huyo wa serikali alilala katika hoteli hiyo kwa siku nne – kati ya tarehe 9 na 13 Juni 2011.
Kila siku alilipiwa na mwenyeji wake, fedha za Afrika Kusini, Rand 2, 830 (karibu Sh. 500,000).
Malima amejitambulishwa katika hoteli ya Michelangelo kwa jina la Johan Ernest Malima. Gazeti hili halikuweza kufahamu mara moja, kwa nini Malima anayetambulika nchini kuwa ni muumini mzuri wa madhehebu ya kiislamu, alikubali kutumia jina hilo linalotumiwa na waamini wa kikristo.
Katika uthibitisho huo wa hoteli, mwenyeji wake anasema, “…Dereva atakuja uwanja wa ndege wa Cape Town na kukuchukua... atakuwa na kibao chenye jina la hoteli ya Michelangelo... na wewe utajitambulisha kwake kwa jina la Ernest Malima.”
Haikufahamika iwapo Malima aliwasiliana na ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini na kueleza kuwa angalau kwa safari hiyo hatajulikana kwa majina yake rasmi kama anavyofahamika kwa aliyemteuwa na kwa Watanzania kwa jumla.
Abdurazak Ebrahim anafahamika nchini Afrika Kusini kuwa ni mwenye mahusiano na watu wengi ndani na nje ya nchi hiyo, “hususani katika mambo ya uwekezaji katika uchimbaji wa madini na biashara ya dawa za binadamu ...,” anaeleza kiongozi mmoja wa serikali ya Tanzania ambaye hakutaka kutajwa gazetini.
Alikuwa akijibu swali la gazeti hili iwapo serikali inafahamu mahusiano kati ya kigogo huyo na mawaziri wa Tanzania.
Gazeti limeshindwa kuwapata Chikawe na Malima. Wote wawili simu zao ziliita bila kupokelewa. Mwandishi alipowatumia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kuwauliza kuhusika kwao katika miradi hiyo, hakuna aliyejibu.
Ujumbe kwa Malima ulisema, “MwanaHALISI linataka kufahamu ni biashara gani unayofanya na Abdurazak Ebrahim hadi akulipie hoteli na tiketi ya kwenda Afrika Kusini, Juni mwaka huu, wakati wewe ni waziri?”
Aidha, gazeti lilikuwa limetaka kujua iwapo Adam Malima Kigoma, ndiye yuleyule Johan Ernerst Malima.
Naye Chikawe aliulizwa, “Tunataka utueleze jinsi unavyoufahamu mradi wa dawa za virutubisho kwa wagonjwa wa ukimwi ambao wewe unatajwa pamoja na Abdurazak Ebrahim.”
Nyaraka zilizoandaliwa na mmoja wa mawakala wa Abdurazak Ebrahim, Tosky Hans zinaonyesha “...kuthibitika kuwapo kwa madini ya kopa wilayani Mpanda, lakini uchunguzi wa jiolojia utakaonyesha wingi wa madini hayo bado haujakamilika.”
Katika nyaraka nyingine ambazo zinaitwa nyaraka za siri na za binafsi (private and confidential), inaonyeshwa kuwapo makubaliano ya pande mbili – kati ya Abdurazak Ebrahim kwa upande mmoja na Chikawe na Malima kwa upande mwingine.
Makubaliano kati ya vigogo hao yalifanyika 22 Machi 2011 na yanahusisha upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji madini na nafasi katika uuzaji wa bidhaa mbalimbali kama dawa za banadamu katika ukanda wa Jangwa la Sahara.
Nyaraka zinasema, “makubaliano au mikataba itakayofanywa itakuwa ni kwa manufaa ya watu binafsi” na kwamba katika makubaliano hayo wahusika wameafikiana kuanzisha na kuendeleza mahusiano ya kibiashara kwa kuzingatia vigezo vya mkataba.
Makubaliano hayo pia yanahusisha hatua zote za maafikiano, majadiliano na mawasiliano pamoja na kuwahusisha baadhi ya watu walio katika mahusiano hayo ya kibiashara.
Nyaraka zinasema kuwa makubaliano hayo yatabaki kuwa siri baina ya pande mbili zinazohusika na utakuwa mkataba wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa makubaliano, mikataba yote itasainiwa kwa kutumia sheria za Afrika Kusini.
Kwa upande wa biashara ya virutubisho vya madawa ya binadamu kwa wagonjwa wa HIV – Secomet V – Chikawe na Malima wanatajwa kuanzisha biashara hiyo inayodaiwa kuwa inaweza kuwaingizia mamilioni ya shilingi kwa muda mfupi.
Katika andishi kwa njia ya barua pepe iliyotumwa 11 machi 2011 na Zak Ebrahim kwenda kwa Chikawe, mfanyabiashara huyo anasema “biashara hiyo inalipa vizuri.” Awali Chikawe aliambatanisha ripoti iliyoandikwa na Dk. L.M.M Chuwa wa hospitali ya St. Benard ya jijini Dar es Salaam. Anasema kuwa daktari huyo alikuwa na mazungumzo na Shelys Pharmaceutical mwaka 2007 na walimuagiza Dk. Chuwa kufanya majaribio watu 53 kwa kutumia Secomet V. Majaribio yamepangwa kukamilika katika kipindi cha miezi 6 hadi 9 kutoka sasa.
Hata hivyo, wataalamu wa dawa hiyo wanasema watumiaji wengi wa Secomet V, hali zao zimezidi kuwa mbaya.
“Kuna uniti 28000 zimeuzwa nchini Afrika Kusini kwa mwezi zikiwa na ongezeko la asilimia 20 kwa mwezi. Ni biashara inayojitosheleza na na inayoweza kuwa na uhitaji ndani wiki 8 mpaka 12,” anasema Abdurazak Ebrahim katika andishi lake kwa Chikawe.
Wabia hao wawili wamependekeza kutafuta namna ya kuizalisha nchini vimelea hivyo vya Secomet V.
“Ni muhimu tukapata baadhi ya mawazo toka Tanzania juu ya mipango tunayoitarajia. Kuna aina mbili ya Fulvic Acid ambayo ni ya vidonge na nyingine ni ya maji ambayo itakuwa na gharama kubwa katika usafirishaji dawa zote zinatakiwa kutumiwa na mgonjwa kwa dozi ya mara tatu kwa siku,” anaeleza.
Akiandika kwa njia ya kushawishi, Abdurazak Ebrahim anataka kufahamu kutoka kwa Chikawe kama serikali ya Tanzania ina fedha za kununua bidhaa hizo; “hii ni njia muhimu ya kupata mafanikio kama zikisambazwa Tanzania.”
Uchunguzi wa suala hili unaendelea.
No comments:
Post a Comment