Saturday, August 13, 2011

Ngeleja sasa aja na bajeti ya 1.2 trilioni

Symbion, NSSF wapewa miradi ya kuzalisha Nchi nzima

KAMPUNI ya Symbion Power ya Marekani na Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) wamepewa zabuni ya kuingiza nchini mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura, katika mpango ambao Serikali itauwasilisha bungeni leo.

Symbion Power ni kampuni ambayo ilinunua mitambo iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya Dowans Tanzania, imepewa zabuni ya kuzalisha megawati 205 za umeme, wakati NSSF wataingiza mitambo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 150.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, iliyowasilishwa na kujadiliwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo Mwananchi limeiona, mpango wa dharura kati ya Agosti 2011 na Desemba 2012 itaigharimu Serikali Sh1.24 trilioni.

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni ya dharura itakayozalisha megawati 1,032 zikiwemo 572 kati ya sasa na mwezi Desemba mwaka huu na megawati 460 zaidi ifikapo Desemba 2012.

“Ili kukabiliana na mgawo wa umeme kwa kipindi cha dharura, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, pamoja na taasisi za umma itatumia uwezo wa mitambo iliyopo nchini kukodisha na kununua mitambo ya kufua umeme itakayotosheleza mahitaji ya sasa na baadaye,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Ngeleja.

Hata hivyo mpango huo wa Serikali ambao unatarajiwa kujadiliwa bungeni leo, nusura ukataliwe na Kamati husika kutokana na kile wajumbe wa kamati hiyo walichosema kuwa ni kuchelewa kuwasilishwa mbele yake ili ijadiliwe kama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alivyoahidi.

Kamati hiyo ilikutana na upande wa Serikali kwa mara ya kwanza juzi, zikiwa zimebaki siku mbili  kabla Ngeleja hajarejea bungeni leo ili kutafuta ridhaa ya Bunge kupitisha bajeti ya wizara yake, baada ya kufanya marekebisho yenye lengo la kuliwezesha Taifa kuondoka gizani.

Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Pinda iliondoa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni Julai 18, mwaka huu baada ya wabunge wengi, wakiwemo wa upinzani na wale wa CCM kuweka msimamo wa kutoiunga mkono kwa maelezo kwamba haikuwa na majibu ya matatizo ya uhaba wa umeme nchini.

Pinda alitumia kipengele cha 55 (3) (b) pia cha 59(1) vya  kanuni za kudumu za bunge toleo la 2007, ambavyo vinampa nafasi ya kuliambia Bunge sababu za kuahirisha bajeti na muda ambao utatumika katika kuirekebisha.

Pinda aliomba muda wa wiki tatu kwa ajili ya Serikali kujipanga upya, kauli ambayo aliitoa wakati Shirika la Umeme nchini (Tanesco) likiwa limetangaza mgawo wa umeme usio na kikomo kutokana na uhaba wa maji kwenye mabwawa ya kuzalishia nishati hiyo.

Ilikuwa ni ahadi ya Pinda kwamba katikia mchakato huo, Serikali ingeshirikiana na wabunge kupitia kamati za kisekta ambazo baadaye zilitajwa kuwa Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Fedha na Uchumi na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, lakini hadi juzi hakuna kamati hata moja ambayo ilikuwa imeshirikishwa katika mkakati huo.

Hali hiyo ndiyo ilisababisha Kamati ya Nishati na Madini juzi kugomea mpango huo wa Serikali kwa maelezo kwamba, haikuwa na muda wa kutosha kuujadili huku baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakihoji sababu za kuchelewa kushirikishwa kwao.

"Jana (juzi), huko hali ilikuwa mbaya sana, wajumbe walichachamaa wakawaambia watendaji wa Serikali kuwa wamekaa muda wote huo halafu wanaleta mpango wao wakati zikiwa zimebaki siku mbili tu, wakasema hawataki," kilieleza chanzo chetu cha habari na kuongeza:

"Lakini busara zilitumika ikaonekana kwamba, tujadili tu ili tuone kama kuna jambo la kusaidia, ndo leo (jana) tunaendelea."

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata bungeni zilidai kuwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba ilishaomba kukutana na uongozi wa Wizara zaidi ya mara tatu, lakini kila walipotaka kufanya hivyo, upande wa Serikali ulisema hauko tayari.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, wiki hii aliomba mwongozo wa Spika, akihoji sababu za Serikali kutokutana na kamati husika tangu kuahirishwa kwa mjadala wa hotuba ya Nishati na Madini, lakini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema: "muda bado unaruhusu Serikali kukutana na kamati husika”.

Mwananchi limedokezwa kuwa huenda bajeti hiyo ikapata wakati mgumu wakati bunge litakapokaa kama kamati, kutokana na ukweli kwamba ni kamati ya Bunge ya kisekta moja tu iliyopata fursa ya kushiriki mchakato wa maandalizi yake, tena nyakati za mwisho tofauti na matarajio ya awali ya kushirikishwa kwa kamati tatu.

No comments:

Post a Comment