Wednesday, August 24, 2011

Jairo asafishwa

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, amerejeshwa kazini baada ya tuhuma dhidi yake zilizotolewa bungeni kutothibitishwa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kwamba Jairo anarejea kazini leo, kuendelea na nafasi iliyokuwa ikikaimiwa na Eliakim Maswi.

Alipewa likizo Julai 21 kupisha uchunguzi dhidi yake. Luhanjo alisema matokeo ya uchunguzi wa awali uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), haukuthibitisha kuwapo kwa usahihi tuhuma zilizokuwa zimetolewa dhidi yake.

Luhanjo aliyefuatana na CAG, Ludovick Utouh na Naibu wake, Jumaa Mshihiri katika mkutano huo, alisema utaratibu wa taasisi kuombwa kuchangia fedha kwa ajili ya kuwezesha
bajeti za wizara zao ni wa kawaida.

Alisema waziri anayepeleka bajeti ya Serikali, hutakiwa kufuatana na maofisa wake. “Kuomba mchango ni suala la kawaida,” alisema Luhanjo ambaye alimpa nafasi CAG aeleze kwa ufasaha matokeo ya uchunguzi huo.

Matokeo ya uchunguzi yaliyosomwa na Utouh yalionesha kuwa ukaguzi maalumu ulibaini kuwa fedha zilizochangwa kwa mtindo unaotuhumiwa hazikufikia Sh bilioni moja na taasisi zilizohusika katika uchangiaji huo si 20 kama tuhuma zinavyodai.

Kuhusu madai kwamba fedha hizo zilitumika kushawishi wabunge kupitisha bajeti ‘kiulaini’, Utouh alisema ukaguzi wake haukupata ushahidi wowote juu ya matumizi hayo.

Alisema timu ya ukaguzi ilitumia mbinu zikiwamo za mifumo ya kielektroniki ya kuchambua data na kupata jumla ya malipo kwa kila ofisa.

Katika uchambuzi huo, ilibainika kuwa malipo yaliyofanyika ni kwa ajili ya posho za kujikimu, takrima na posho za vikao, kwa maofisa walioshiriki shughuli nzima ya kuwasilisha bajeti.

“Hakuna ushahidi wowote wa malipo kwa waheshimiwa wabunge,” alisisitiza. Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), ndiye aliyeibua tuhuma hizo bungeni Julai 18, kwa
kuwasilisha barua iliyoandikwa na Jairo ikizitaka idara na taasisi zote za wizara hiyo, kila moja ichangie Sh milioni 50, kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya uwasilishaji wa hotuba ya bajeti.

Wabunge walihoji uhalali wa michango hiyo na matumizi ya fedha hizo zilizopitishwa kwenye akaunti ya Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) katika Benki ya NMB tawi la Dodoma, na kuzua hisia kuwa zililenga kuhonga wabunge kwa kuwashawishi ili bajeti ipite kirahisi.

Akifafanua zaidi juu ya uchunguzi, Utouh alisema walibaini kuwa jumla ya fedha zilizochangwa ni Sh 578,599,100 na si Sh bilioni moja iliyotajwa kwenye tuhuma.

Alisema taasisi nne za wizara zilichangia jumla ya Sh 149,797,600. Alizitaja taasisi hizo na fedha zilizochangiwa kwenye mabano kuwa ni Wakala wa Nishati Vijijini –REA (milioni 50/- ), Shirika la Umeme Tanzania –Tanesco (milioni 40/-), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania –TPDC (milioni 50/-) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliyochangia Sh 9,797,610.

Idara ya Uhasibu ilichangia Sh 150,720,000 na Idara ya Mipango Sh 278,081,500. Hata hivyo, Utouh alisema Ewura ambayo ilikuwa imeombwa Sh milioni 40 haikutuma mchango wake GST kama ilivyokuwa imeagizwa, bali ilijitolea kugharimia chakula cha mchana na kiasi cha Sh 3,656,000 kilicholipwa kwa Kampuni ya African Conference Centre Ltd na kupokewa kwa stakabadhi namba 917 ya Julai 18, 2011.

Utouh alisema Ewura ililipia gharama za tafrija iliyofanyika Julai 18 jioni katika ukumbi wa St Gaspar kwa gharama ya Sh 6,141,600.

Alifafanua kuwa taarifa ya benki ya Julai 29, kuhusu akaunti namba 505100068 ya GST iliyotumika kukusanya fedha zilizochangwa, inaonesha kuwa jumla ya Sh 99,438,380 zilirejeshwa kwenye akaunti hiyo Julai 20.

Pia taarifa hiyo ya benki inaonesha kuwa Sh 14,860,000 zilirejeshwa kwenye akaunti hiyo Julai 27. Baada ya kupitia vitabu vya hesabu vya GST pamoja na kuhoji wahusika, ilibainika
kuwa Sh 99,438,380 zilisalia kutokana na fedha za kuwasilisha bajeti ya wizara kupokewa.

Ilibainika pia kwamba Sh 14,860,000 zilikuwa ni bakaa ya fedha za kikao cha kazi cha kuandaa uwasilishaji wa bajeti, fedha ambazo zilipokewa Julai 27.

Hivyo hadi Julai 29, bakaa ya fedha zilizochangwa kwa ajili ya kuwasilisha bajeti bungeni ilikuwa Sh 195,235,567.33.

No comments:

Post a Comment