SERIKALI inachunguza kiini cha barabara ya Kilwa kutoka Mivinjeni hadi Mbagala jijini Dar es Salaam kujengwa chini ya kiwango ili aliyehusika airekebishe kwa gharama zake.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe amelieleza Bunge mjini Dodoma kuwa, Mhandisi, Mhandisi Mshauri na wataalamu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanachunguza ili kufahamu kiini cha tatizo.
Mwakyembe amewaeleza wabunge kuwa, viongozi wa Wizara hiyo wamekuwa wakali katika kusimamia ubora wa barabara zinazojengwa na ametoa mifano ya barabara kadhaa ambazo zinachunguzwa na nyingine waliosababisha zijengwe chini ya kiwango wametakiwa kuzirekebisha kwa gharama zao.
Kwa mujibu wa Mwakyembe, Mkandarasi aliyejenga barabara ya Nangurukuru- Mbwemkulu ametakiwa kuirekebisha kwa gharama zake.
Amesema, barabara ya Sekenke- Selui inachunguzwa ili aliyesababisha ijengwe chini ya kiwango awajibike.
Amebainisha kwamba, kwa kawaida barabara za lami, baada ya kukamilika kujengwa huwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja lakini sasa Serikali imeongeza hadi miaka mitatu, na barabara za changarawe zinakuwa kwenye uangalizi kwa miezi sita.
Dk. Mwakyembe ameyasema hayo wakati anajibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chonga, Haroub Mohammed Shamis aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali baada ya Waziri wa Ujenzi, John Magufuli kuikataa barabara ya kutoka Mivinjeni hadi Mbagala kwa maelezo kuwa imejengwa chini ya kiwango.
Mbunge huyo pia alisema, kwa kuwa bidhaa zinazokuwa chini ya kiwango huchomwa moto na nyingine hupondwa na tingatinga, je barabara zinazokuwa chini ya kiwango hufanywaje?
Awali Mbunge huyo aliuliza, ni vigezo gani vinavyotumika kumpata mshauri huyo wa ufundi na ni kwa nini baadhi ya miradi inaharibika mara tu baada kukabidhiwa.
Dk. Mwakyembe amewaeleza wabunge kuwa, kazi ya ujenzi wa miradi ya barabara inahitaji maandalizi yanayohusisha upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na tathimini ya athari kwa mazingira na kijamii.
“Aidha, wakati wa ujenzi unahitajika usimamizi thabiti ili kukidhi ubora kulingana na usanifu wa viwango vilivyoko kwenye mkataba” amesema Mwakyembe.
Ametaja vigezo vya kumpata Mhandisi Mshauri kuwa ni pamoja na uzoefu wa kampuni ya ushauri wa kulinganisha na mradi husika, uzoefu wa kiwango cha elimu kwa wataalamu wanaohitajika kufanya kazi husika, na gharama iliyopendekezwa na mshauri kwa ajili ya kufanya kazi husika.
“Barabara inaweza kuharibika mapema baada ya ujenzi kutokana na mkandarasi kujenga barabara chini ya ubora katika viwango vilivyowekwa na Mhandishi Mshauri kukosa umakini katika kusimamia na kudhibiti ubora wa kazi wakati wa ujenzi. Aidha, usanifu hafifu wa barabara husika nao unaweza kuwa sababu” amesema.
No comments:
Post a Comment