Tuesday, August 16, 2011

KUTOKANA na uhaba wa maeneo ya wazi ya kupumzikia, burudani na michezo katika miji mingi nchini hasa Dar es Salaam unaochangiwa na ujenzi holela, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, itaanza kulitumia Bonde la Mto Msimbazi kwa shughuli hizo.

Kutokana na hatua hiyo, wananchi wote waliovamia maeneo hayo katika kata za Buguruni, Hannasif, Jangwani, Kigogo, Kinondoni, Magomeni, Mchikichini, Tabata, Upanga Magharibi na Mashariki na Vingunguti, ambako kutafanywa bustani ya Jiji, hawatalipwa fidia.

Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Anna Tibaijuka, alisema hayo jana, wakati akiwasilisha bungeni Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka huu wa ambapo aliomba Bunge liridhie na kupitisha Sh 47,895,198,000.

Profesa Tibaijuka kwenye kipengele cha Usimamizi na Uendelezaji wa Miji, alisema, “Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI, hutoa kanuni na miongozo kuhusu usimamizi na udhibiti wa uendelezaji wa miji nchini … mwaka 2010/11 Wizara iliandaa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 2007.

Lengo ni kupeleka madaraka kwa maofisa wa ardhi wa kanda.”

Aliongeza: “Miongoni mwa maeneo hayo ni Jiji la Dar es Salaam, kwa mwaka 2011/12 wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Manispaa zake litaandaa mpango wa kuboresha eneo la Bonde la Msimbazi ili litumike kama bustani ya Jiji.

“Natoa wmito kwa mamlaka na taasisi husika kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha wananchi wanahamishwa, kuhusu mpango huo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vya baadaye, aidha waliovamia eneo hilo au kufanya maendeleo waelewe kuwa hakuna mustakabali katika shughuli zao ndani ya bonde hilo,” alisisitiza Profesa Tibaijuka.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo ya Mipangomiji ya mwaka 2007, Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam wa mwaka 1979 na agizo la Rais, vinaelekeza kuwa Bonde hilo lilindwe kwa maslahi ya umma.

Hata hivyo, pamoja na mpango huo, Waziri alibainisha changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa shughuli za wizara hiyo kuwa ni pamoja na kuwapo madeni makubwa ya halmashauri zilizokopeshwa fedha katika Mfuko wa Kupima Viwanja.

Waziri alisema kuanzia Julai 2000 hadi Juni, Wizara ilitoa mkopo wa Sh bilioni 1.101 kwa halmashauri 42 lakini Sh 651,758,143 zimerejeshwa huku Sh 642,130,579 bado, wakati katika mradi wa viwanja 20,000 Dar es Salaam ulikopesha kwa halmashauri, Sh bilioni
2.62 hadi Juni mwaka huu hazijarejeshwa.

Katika kukabiliana na hilo, alisema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha wanashauriana ili halmashauri hizo zirejeshe mikopo yao moja kwa moja kupitia ruzuku zao zinazotolewa na Hazina.

No comments:

Post a Comment