KATIBU Mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula, amemtaka Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) amwoneshe liliko shamba alilodai ni la hekta 2,000 analolimiliki.
“Iwapo Mheshimiwa Halima Mdee atashindwa kutuonesha shamba hilo lilipo, tutaamini kwamba amekula njama na waliomdokeza, kuwa kuna hekta hizo 2,000 mali ya ndugu Mangula ili wanihujumu na walidhulumu,” alisema Mangula katika barua yake kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Barua hiyo iliyoandikwa juzi na kunakiliwa pia kwa Waziri Mkuu, Mdee mwenyewe na vyombo vya habari, ilisema katika mazingira kama hayo, Mangula ataomba mwongozo wa kisheria kutoka kwa wanasheria wake.
Hivi karibuni, Mdee alizungumza bungeni akiwataja Mangula, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Mbunge Hassan Ngwilizi, kwamba wanamiliki ardhi kinyume cha
utaratibu na kuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi.
Alidai ardhi hiyo iko katika eneo la lililokuwa Shirika la Usimamizi wa Ranchi za Taifa (NARCO) Mvomero mkoani Morogoro.
“Hali ilivyo sasa, jina langu limechafuliwa, familia yangu hainiamini kwa kuwaficha mali hiyo, ilihali mali zote wanazijua kwamba ninamiliki kwa niaba yao, nimechonganishwa na wanavijiji wa Dakawa ambao mheshimiwa huyo amesema nimewanyang’anya hekta 2,000
kutoka NARCO na kuitoa ardhi iliyomilikiwa kihalali na Serikali,” alisema Mangula.
Alisema, Mdee ambaye ni Waziri Kivuli wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi bungeni, anamkumbusha kauli ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa, ambaye “aliwahi kunizushia tuhuma nzito katika mkutano wa hadhara alioufanya Tabora kwamba amegundua orodha mpya ya mafisadi wa nyongeza, akanitaja mimi kuwa miongoni mwao na alinituhumu kuwa namiliki shamba la ukubwa wa eka 2,000 Njombe.”
Alishangaa kuwa wakati Katibu Mkuu Chadema alidai kuwa yeye anamiliki eka 2,000 Njombe, Mbunge Mdee anataja kuwa anamiliki hekta 2,000 Dakawa.
Kuhusu maisha yake ya sasa, Mangula alisema anaishi kijijini Kinenulo, Njombe alikoamua kuishi baada ya utumishi wa umma, akiwa Mkuu wa Wilaya kwa miaka sita, Mkuu wa Mkoa na Katibu wa Mkoa miaka 11 na Katibu Mkuu CCM miaka 10.
Alisema alipokea taarifa hizo za Mdee akiwa msibani kijijini Lugenge, akiwa amefiwa shangazi yake na kuambiwa na wanawe baada ya kusikia tuhuma hizo .
“Walishituka sana na kushangaa kwa nini nilikuwa sijawaeleza kughusu shamba hilo. Niliwajibu kuwa hakuna mali ninayomiliki wao wasiijue.
Niliwambia wavute subira na kwamba tutamtafuta mpaka tumwelewe mtu aliyetuficha taarifa kuhusu ‘shamba letu hilo.’”
Alisema anachoshindwa kuelewa ni kwa nini yeye au wanawe ambao ni wakazi wa Kawe, hawajaambiwa na Mamlaka husika (Idara ya Ardhi Mvomero) kuhusu shamba hilo mpaka atumwe Mbunge wao Mdee, akaliambie Bunge nao wasikie kutoka bungeni.
Kuhusu shamba alilonalo Kinenulo, alisema amemilikishwa hekta 32 alizolima miti ya pines hekta nne, maparachichi hekta mbili, matunda aina ya apples hekta mbili, mikaranga hekta moja, mibuni hekta moja; na nusu hekta analima mboga.
“Baada ya kupata taarifa hiyo ya neema, nitamwomba sasa Mdee anayetupigania wapiga kura wake wa Kawe, akatuoneshe (mimi na wanangu) shamba hilo lilipo, ili tuanze mchakato wa kupewa hati kama yeye hakukabidhiwa hati hiyo kwa niaba yetu.
Hivi sasa naishi kwa pensheni ya Sh 130,000 tangu Juni 2006,” alisema Mangula.
No comments:
Post a Comment