Thursday, August 18, 2011

Ewura yajirudi

BAADA ya kubanwa na Baraza la Mawaziri kwa kuyumbisha bei ya mafuta, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imekubali kufanya marekebisho ya fomula ya ukokotoaji, kwa kuzingatia akiba za mafuta zinazokuwa nchini wakati husika.

Uamuzi huo wa Ewura ambao unasubiri baraka za Bodi yake ndipo mchakato huo uanze, umekuja baada ya wananchi kulalamikia hatua ya Mamlaka hiyo kupandisha bei ya petroli kwa zaidi ya Sh 100 kwa lita, katika kipindi cha saa 48 baada ya bei hizo kushushwa.

Baada ya Ewura kutangaza bei mpya, wananchi wengi walilaani hatua hiyo, kuwa inalenga kunufaisha wafanyabiashara na si wananchi kama ambavyo iliahidiwa na Serikali kuwa ingeshusha bei za mafuta, ili kuleta nafuu ya maisha kwa wananchi.

Mabadiliko hayo ya bei pia yalileta mgongano kati ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu.

Wakati Ngeleja akiliambia Bunge kuwa bei hizo hazihusu akiba ya mafuta iliyopo nchini, Masebu alisema bei hizo zitaanza kutumika mara moja bila kujadili akiba iliyopo sawa na inavyofanyika kwenye kodi.

Ni kutokana na kusigana kwa wakubwa hao, huenda ndiko kuliikera Serikali na kulazimika Mkurugenzi huyo kuitwa mbele ya Baraza la Mawaziri juzi na kuhojiwa juu ya hatua yake ya kupandisha bei ya petroli bila kujali akiba ya mafuta iliyopo nchini.

Gazeti hili jana liliripoti namna Masebu alivyohenyeshwa na mawaziri, kwa namna Mamlaka yake inavyoyumbisha bei za mafuta, hivyo kuwafanya wananchi kutoonja nafuu ya maisha waliyoahidiwa na Serikali wakati wa Bajeti ya mwaka huu.

Katika Bajeti yake, Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ilitangaza kuondoa baadhi ya tozo kwa asilimia 50 zilizokuwa zinatozwa na taasisi mbalimbali. Hali hiyo ingesaidia kupunguza bei ya mafuta kwa zaidi ya Sh 200 kwa lita.

Taarifa ya Ewura iliyotolewa jana na kusomwa na Mkuu wake wa Mawasiliano, Titus Kaguo, ilisema imefanya hivyo kwa vile wadau na umma wangependa kuona Mamlaka hiyo ikipitia upya utaratibu wake wa kutangaza bei za mafuta kila baada ya wiki mbili.

“Kwa kuwa Ewura ni taasisi sikivu na yenye kujali maoni ya wadau, itakaa na wadau na kukubaliana haja ya kurekebisha fomula, ili ieleze namna ya kutathmini akiba iliyopo kabla ya kubadilisha bei za mafuta,” alisema Kaguo.

Ewura ilitetea uamuzi wake wa kupandisha bei za mafuta kuwa ulitokana na kupanda kwa bidhaa hizo kwenye soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.

Juu ya bei kuanza kutumika bila kujali akiba iliyopo ndani ya nchi, Ewura kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, ilisema suala la bei ya mafuta yaliyomo kwenye maghala lina sura mbili, ambazo ni bei mpya kumrudishia gharama alizowekeza kwenye akiba aliyonayo.

Pili, Masebu alisema bei pia inatakiwa imwezeshe mwekezaji kuwa na mtaji wa kutosha kuagiza shehena nyingine kwa bei itakayokuwa kwenye soko, wakati anaagiza shehena nyingine ya mafuta, ili kuweka mfumo endelevu wa kuhakikisha kunakuwa na mafuta ya kutosha muda wote.

Katika mkutano wake wa jana, Kaguo alisema Ewura itafuatilia kwa karibu uanzishwaji wa mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja, ambao utawezesha kupata kiasi halisi cha mafuta yatakayokuwa yanaagizwa na kujua bei zake kwa usahihi zaidi.

Alisema bei hizo ndizo zitatumika kukokotoa katika kila kipindi husika. Mfumo huo tangu uanze kuelezwa na Ewura, haijajulikana utaanza lini na Kaguo alipoulizwa alisema ili uanze ni lazima kuwe na Bodi na Menejimenti ya kusimamia kampuni itakayofanya kazi hiyo.

“Bodi inaundwa na waziri, hivyo pindi atakapoiunda, utaratibu wa kupata menejimenti utaanza na ndipo uagizaji mafuta kwa pamoja utaanza,” alisema Kaguo.

Kwa mfumo wa biashara ya mafuta ulivyo sasa, kila kampuni inaagiza kwa vyanzo vyake inavyovijua, huku kampuni zingine kama BP na Engen, zikiagiza kutoka kampuni mama zilizoko Ughaibuni.

Naye Lucy Lyatuu anaripoti kuwa baadhi ya wadau wa usafiri nchini, wameiomba Serikali iifute Ewura kwa kushindwa kusimamia sheria.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (DABOA), Ibrahim Awadh, alisema wanaishangaa Ewura kutokana na kwamba walitarajia bidhaa hiyo iendelee kushuka badala ya kupanda.

Alisema kwa utaratibu huo wa Ewura, imesababisha usumbufu kwao kwa kuwa nao wamekopa fedha benki na kusumbuliwa kunachangia washindwe kulipa mkopo huo kwa muda unaotakiwa.

“Mimi nafikiri katika hili, Serikali ingeifuta kabisa Mamlaka hiyo na kuacha kujiingiza katika biashara huria ya kupanga bei,” alisema Awadh.

Alisema miaka ya nyuma hakukuwa na Ewura, lakini mambo yalikwenda vizuri na hata Serikali ya Awamu ya Tatu ilifanikiwa kuimarisha Shilingi sokoni na kudhibiti bei ya mafuta.

“Kwa mfano wakati wa uongozi wa Mkapa (Benjamin Rais wa Awamu ya Tatu) aliacha mafuta ya dizeli yakiuzwa Sh 800 kwa lita lakini hadi sasa yameongezeka zaidi ya mara tatu, ina maana kwa miaka mingine 10 ijayo wananchi wataishije?” Alihoji Awadh.

Alisema chama hicho kinatarajia kuandika barua kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (SUMATRA) baada ya Mfungo Mtukufu wa Ramadhan, kuelezea kusudio la kupandisha nauli kuliko kuendesha biashara kwa hasara.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama, alisema utaratibu wa Ewura wanauona kama mchezo wa kuigiza: “Yawezekana kuwa Ewura, ni wamiliki wa vituo vya mafuta.”

Alisema kigezo cha mafuta kupanda katika soko la dunia na thamani ya Shilingi kuanguka, ni kiini macho na kuhoji kwa nini katika Awamu ya Tatu hayo yote hayakutokea.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, alisema kutokana na mkanganyiko uliosababishwa na EWURA, aliiomba Mamlaka hiyo kuweka wazi fomula ya ukokotoaji, ili kila mwananchi afahamu kinachofanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji wa Mafuta (TAOMAC), Salum Bisarara, alisema suala la mafuta ni tatizo kubwa la kitaifa na kwa sasa Msemaji Mkuu ni EWURA.

Alifafanua kuwa kitakachosemwa na Mamlaka hiyo watakubaliana nacho.

No comments:

Post a Comment