Waendesha mashtaka wamemuomba jaji kutupilia mbali kesi inayo mkabili aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Dominique Strauss Kahn.
Bw Strauss Kahn anakabiliwa na kesi ya jaribio la kumbaka mhudumu wa hoteli moja mjini New York.
Waendesha mashtaka wamemuelezea jaji kwamba '' hawajaridhika kuwa mshitakiwa ana hatia bila shaka yoyote''.
Kesi hiyo, iliyoanzishwa kufuatia madai ya mhudumu wa hoteli moja, Nafissatou Diallo, ilivunjika wiki chache zilizopita kufuatia maswali kuhusu uaminifu na nia bi Diallo.
Bw Strauss-Kahn, mwenye umri wa miaka 62, alikamatwa mwezi Mei na kufunguliwa mashataka ya kujaribu kumbaka mwanamke huyo mhamiaji kutoka Afrika, mwenye umri wa miaka 32.
Waendesha mashtaka wamemueleza jaji kuwa Bi Diallo ''hakuwa mwaminifu kuhusu maswali mazito na hata yale madogo''.
Jaji anatarajiwa kutoa uamuzi wake siku ya jumanne.
Iwapo kesi hiyo itatupiliwa mbali Bw Strauss-Kahn atakuwa huru kurudi nchini Ufaransa, japo bado anakabiliwa na kesi nyingine bado dhidi ya Bi Diallo.
Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano mfupi na waendesha mashtaka katika mahakama hiyo ya Manhattan, wakili wa Bi Diallo, alisisitiza kuwa haki haikuwa imetendeka.
Umaarufu wa Strauss-Kahn wapungua Ufaransa.
Nchini Ufaransa, maafisa bado wanafikiria ikiwa watamfugulia mashtaka Bw Strauss-Kahn kwa tuhuma za kujaribu kumbaka mwandishi wa habari nchini humo Tristane Banon wakati alipokuwa akihojiwa naye mwaka wa 2003.Bw Strauss-Kahn alidhaniwa kuwa angempa ushindani mkali rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy katika uchaguzi wa urais wa Aprili 2012.
Hata hivyo kura ya maoni ya hivi karibuni inaonyesha kuwa theluthi mbili ya raia nchini Ufaransa hawamtaki Bw Strauss-Kahn kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.
No comments:
Post a Comment