Friday, August 26, 2011

Vigogo Chadema kizimbani

KATIBU wa Jumuiya ya Vijana ya Chadema (BAVITA), Anold Kamunde na aliyekuwa Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema, Gervas Mgonja wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha na kupora vitu na fedha vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 3.5.

Mbali na hilo pia askari Polisi, Salumu Idefonce (23) wa Kituo kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha amefikishwa mahakamani kwa madai ya mauaji ya mlinzi wa kampuni ya kuuza na kununua madini ya Classic Gems, Joseph Kisuda.

Wakisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Agustino Kombe, ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa Mgonja na Kamunde, walifanya hayo wakitumia bunduki aina ya SMG na bastola katika tukio lililotokea Ngarenaro jijini hapa Juni 8.

Kombe alidai hivyo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Rose Ngoka, kuwa
watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kwa kumpora Elizabeth Mkuka, fedha taslimu Sh milioni 1.8 na simu mbili.

Aliendelea kudai kuwa Mgonja na Kamunde walitenda kosa hilo saa 3 usiku kwa kiasi hicho cha fedha na simu mbili za Sumsung na BlackBerry zote zikiwa na thamani ya Sh milioni 1.6.

Viongozi hao walikana mashitaka yao na kesi yao itatajwa Septemba 8 na walirudishwa rumande kwani upelelezi haujakamilika na walinyimwa dhamana kutokana na uzito wa kesi yenyewe kisheria.

Katika kesi ya Idefonce, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Sabina Slayo, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Devotha Msofe, alidai kuwa mtuhumiwa anashitakiwa kwa mauaji pamoja na wenzake wawili katika tukio la Mei 21 katika kampuni hiyo ya madini.

Wenzake ambao wako rumande ni Abdul Philipo ‘Baba Salimu’ na Prosper Saimoni ‘Otieno’.

Mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwani Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji ila Mahakama ya juu yake.

Kesi hiyo itatajwa mahakamani hapo Septemba 6 na alirudishwa rumande hadi siku hiyo.

Habari za nje ya Mahakama zilidai kuwa viongozi wa Chadema wataunganishwa na washitakiwa wengine waliokuwa walisomewa mashitaka juzi katika Mahakama hiyo kwa mashitaka hayo hayo.

No comments:

Post a Comment