Monday, August 22, 2011

Sitta na dhambi ya unafiki ndani ya CCM


Samwel Sitta 
 
Na Jabir Idrissa
 
NIMEKUWA nikimsifu Samwel Sitta anaposimama kueleza, kujadili na kutetea anachokiamini. Huwa namsifu mwanasiasa huyu mwerevu kwa sababu huwa anaeleza kwa msisitizo, nguvu na mvuto mkubwa hicho anachokiamini.

Lakini nilivyopima mwenendo wake wakati akiwa spika wa Bunge tangu Desemba 2005 hadi Agosti 2010, na haya anayozungumza sasa akiwa mbunge na Waziri wa Afrika Mashariki katika serikali ya awamu ya nne, yanashangaza.

Anashangaza. Namsikitikia. Alivyo mwerevu, nilijua atakuwa anapima athari kabla hajatoa kauli yoyote. Kauli zake zinasikitisha.

Hivi anapozungumza huwa anatazama uhalisia wa mambo au huwa anatafuta umaarufu? Au Sitta huyasema hayo katika mbinu za kujionyesha yu mwanasiasa pekee msafi na mahiri?
Je, hiyo ni mikakati yake ya kupalilia mazingira ya kupata urais, wadhifa anaounyemelea kama alivyoomba idhini ya chama chake CCM akitaka kimteue awanie 2005?

Sitta ana kitu kizuri kama kiongozi na hiki kimekuwa sababu kwangu kumsifu. Anapotoa kauli zinazojenga umadhubuti wake kama kiongozi, huwa anaonekana machoni.
Ana msimamo mkali dhidi ya watuhumiwa ufisadi, hasa wale watatu wanaokishughulisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati huu wa kampeni ya kujivua gamba – Andrew Chenge, Edward Lowassa na Rostam Aziz.

Anapowasema watuhumiwa hawa, huwa anakunja uso; anatoa macho, anatunisha mishipa ya shingo. Anaonyesha uchungu na hasira kali.

Kila anapotaja tatizo la ufisadi ambalo nakubaliana naye lilivyo hatari kwa uendelevu wa raslimali za nchi na uchumi wa taifa, Sitta huwashambulia wanasiasa hao.
Ufisadi wenyewe ulianzia kwenye mkataba uliofungwa kati ya serikali ya Tanzania na Richmond Development LLC, kampuni iliyothibitika kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura pasina kuwa na uwezo wa zana na fedha.

Sitta amepata kusema serikali – na hapa alimsema wazi Rais Jakaya Kikwete alipomaliza kuhutubia Bunge la Tisa mwaka 2010 – kwamba wakati mwingine iwe kali na bora ifanye kama China inaposhughulikia wahujumu uchumi.

Inajulikana China huua wanaokutwa wamehujumu uchumi wa taifa, kitendo kinachoiweka pabaya nchi na kutajwa kama taifa kubwa lisiloheshimu haki za binadamu na hivyo kushutumiwa kwa ukiukaji wa haki hizo.
Anatamani hayo wakati ndiye aliyesimamisha mjadala wa ufisadi uliofanywa kupitia mkataba wa Richmond, hatua aliyoamua bila ya kupata baraka za wananchi. Sitta, aliamua tu hilo kwa sababu yeye ni spika (wakati ule).

Aidha Sitta ni kati ya viongozi waandamizi walioshiriki kupanga na kuanzisha chama kilichokuja kwa jina la Chama Cha Jamii (CCJ) miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu uliopita wa rais, wabunge na madiwani.
Wiki tatu zilizopita, alipovikwa, kwa muda, uwaziri mkuu na hivyo kuwa kiongozi mkuu wa shughuli za serikali bungeni, badala ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyekuwa safarini, Sitta alionyesha udhaifu wake.

Aliwasakama wabunge wanaotoa maoni kutaka kero zilizomo katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitatuliwe. Aliwakemea akidai eti wanania ya kuuvunja muungano hivyo “waangaliwe.”
Sitta alimwaga hasira pamoja na kujua fika kwamba miongoni mwa wabunge waliolalamikia kero, ni wenzake kutoka CCM; wakiwemo Jadi Simai Jadi (Mkwajuni), Yahya Kassim Issa (Chwaka) na Mohamed Chombo (Magomeni).

Lakini pengine hilo lilionekana si jambo zito kwa kuwa imani iliyojengeka nchini ni kwamba wanaolalamikia zaidi matatizo ya muungano ni Wazanzibari kuliko Watanzania wa Bara.
Sitta alipopata nafasi nyingine ya kusema bungeni hivi karibuni ni alipoona mjadala wa kuisakama serikali kwa kushindwa kupata ufumbuzi wa tatizo kubwa la umeme.

Aliomba ruhusa ya Spika Anne Makinda kuweka uzito pale mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangwala alipoibua hoja ya kutaka mwongozo wa spika dhidi ya kauli za David Kafulila, mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), aliyeituhumu serikali kuwa legelege.

Kafulila, kijana aliyehama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla, alisema, “Serikali legelege haiwezi...” wakati akijadili makadirio ya matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Sitta akionekana kuchangamsha wabunge wa CCM ambao wengi hulala alisema, “Wabunge wa upinzani kazi yao ni kubeza kila kitu kinachofanywa na serikali, lakini sisi tutahukumiwa na wananchi. Siku zote wapinzani mambo yao ni ya unafikinafiki.”

Kama kuisema serikali ya CCM “ni legelege” inakuwa ni sawa na kuudhi baadhi ya wabunge kama alivyolenga dokta wa Nzega, haya maneno ya Sitta “Wapinzani mambo yao ni ya kinafikinafiki” hayamuudhi yeyote?

Unafiki ni moja ya dhambi nzito katika vitabu vya dini. Katika Uislam, mnafiki ametajwa na Muumba kama mtu mbaya anayestahili adhabu kali.
Kwa Khalifa (sahaba mtukufu) Umar ibn al-Khattab (592-644), mtu aliyefanya unafiki katika kampeni ya kueneza Uislam wakati wa Mtume Muhammad (S.A.W) alitaka kumuua kwa upanga. Ni bahati tu alizuiwa na Mtume.

Sitta anapoita “wanafiki” wale wabunge wanaoutia kasoro na kutaka zirekebishwe haraka, alijitazama kwanza? Kama hakujitizama ndio maana kauli yake hiyo ilifuatiwa na sauti nzito za wabunge wakisema au kumwimbia, “CCJ, CCJ, CCJ.”

Akiulizwa kuhusu CCJ anasema yeye ni mtaji wa kisiasa ndiyo maana hufuatwa na wanasiasa wanapomhitaji kwa ajili ya kupata ushauri wake.
Wakati Sitta anawaita wapinzani wanaoikosoa serikali kuwa ni wanafiki, yeye mwenyewe katika ziara ya mkoani Mbeya ameungana na wapinzani kutaka waliosababisha mgao wa umeme waadhibiwe.
Alisema waliosababisha mgao nchini lazima waadhibiwe maana wameitia serikali aibu. Hivi si yeye aliyezima mjadala wa kampuni ya Richmond ambao wamiliki wake ndio wanadaiwa kuwa mafisadi?

Spika huyu wa zamani anataka wabunge wa CCM tu waikosoe serikali, wapinzani wakifanya hivyo ni wanafiki! Hilo lake la kuanzisha mjadala na kuuzima kabla ya kufika mwisho ni nini?

Wingu limetanda juu yake kutokana na kitendo chake cha kuanzisha CCJ akiwa bado CCM. Nani msaliti au mnafiki; wabunge na Watanzania wanaokosoa muungano wakitaka matatizo yaliyopo yarekebishwe ili uwe endelevu kwa maslahi ya Watanzania wote au yeye aliyeanzisha chama kipya kabla ya kuhama CCM?
Na kwa hapa itabaki hivyo, kwamba kadri Sitta anavyojitutumua kupinga ufisadi na mafisadi, wakiwemo watendaji katika serikali ya CCM, ndivyo anavyojiingiza kwenye kapu la wanasiasa wasio safi na wanaopaswa kujivua gamba.

Nataka kumsihi Sitta kwamba kabla ya kuwatangaza wengine kuwa lazima wajivue magamba kwa kuwa ni wachafu, ni muhimu akaanza kuchukua hatua ya kufuta aliyoyatenda na ambayo yana sura ya uchafu. Vinginevyo, anajikweza bure.

No comments:

Post a Comment