Tuesday, August 23, 2011

Wauza "unga" wanyongwe - Wabunge

UKUMBI wa zamani wa Bunge (Pius Msekwa), jana ulitawaliwa na majonzi na simanzi baada ya wabunge kuonyeshwa video ya watu wanaoingiza, kusafirisha, kuuza na kutumia dawa za kulevya.

Idadi kubwa ya wabunge walioiona video hiyo walitaka wafanyabiashara wanaoingiza na kuuza dawa hizo hapa nchini wanyongwe huku Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mohamed Mwidau (CUF), akimwaga machozi ukumbini.

Video hiyo pia ilionyesha baadhi ya watu waliokufa kwa kupasukiwa na vidonge vya dawa za kulevya walivyomeza, waliouawa kwa kufichua siri, viongozi wa dini na wanamichezo wanaohusika na biashara hiyo.
Tume ya kudhibiti dawa za kulevya ndio walioandaa semina kwa wabunge na kuwaeleza ukubwa wa tatizo, njia zinazotumiwa kuingiza, kusafirisha, madhara wanayoyapata watumiaji na wasafirishaji.

Watendaji wa kitengo cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya walibainisha kuwa mtandao wa wauza ‘unga’ ni mkubwa na upo kwenye idara mbalimbali za serikali, ikiwamo Uhamiaji wanakoshughulikia kutoa pasi za kusafiria.

Walibainisha kuwa hivi sasa wanaouza dawa za kulevya wamepanua wigo wa soko lao na wanawalenga zaidi watoto wa shule za msingi na sekondari, hasa zile wanazosoma watoto wa wenye uwezo kifedha.
“Waheshimiwa wabunge, hivi sasa wauzaji wameamua kuuza dawa hizo kwa kuzipaka kwenye ‘chocolate’ zinazouzwa katika shule wanazosoma watoto wetu. “Wanafanya hivi hasa kwenye shule wanazosoma watoto wa vigogo, kwa kuwa wanajua kila siku mnawapa watoto wenu kati ya sh 500-1,000, nawaombeni muwape tahadhari watoto wenu,” alisema mtendaji huyo.

Baada ya mtendaji wa kitengo hicho kumaliza kuwasilisha mada zake, wabunge walipata nafasi ya kuchangia, ambapo idadi kubwa walitaka wanaojihusisha na dawa hizo wanyongwe.

Akichangia mjadala huo, Mwidau, alisema ndugu zake wawili wamefariki dunia hivi karibuni kwa kupishana wiki moja baada ya kukosea ‘kujidunga.’ Mbunge huyo alisema watu wanaoingiza dawa hizo wanapaswa kunyongwa kwa sababu wanahujumu uchumi wa taifa pamoja na kubomoa kizazi kijacho.

Mwidau hakuweza kuendelea na mchango wake kwani aliangua kilio, jambo lililowafanya wabunge wengi kukumbwa na simanzi pamoja na kumpa pole kwa msiba huo.

Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema hakuna sababu ya kuwafikisha mahakamani watu wanaokamatwa na dawa za kulevya bali wapigwe risasi hadharani.
“Tubadilishe sheria ili ziruhusu mtu anayeingiza, kuuza au kusafirisha dawa za kulevya apigwe risasi hadharani,” alisema.

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema sheria ya kunyonga watu ipo lakini haitekelezwi hivyo ni vema watu watakaopatikana na kosa la kuuza, kuingiza na kusafirisha dawa hizo wanyongwe.

“Serikali iko ‘loose’ sana,  kule gerezani kuna mtu analipwa mshahara na posho kwa ajili ya kunyonga watu lakini hanyongi, sasa hatuoni ni kumlipa mshahara bila kufanya kazi? Tuwapeleke wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanyongwe,” alisema.

Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah (CCM), alisema adhabu ya kifo ipo hata kwenye vitabu vya dini, hivyo serikali isisite kuitekeleza kwa watu wenye lengo la kuwaua Watanzania kwa kuuza dawa za kulevya.

Peter Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM) alisema kuna haja ya kuunda mahakama maalumu kwa ajili ya kusikiliza kesi za wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Mkuu wa Tume ya Kuzuia Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, alisema hivi sasa wanakabiliwa na tatizo kubwa la kisheria, kwani baadhi ya watuhumiwa huachiwa kwa dhamana au kesi zao huisha kwa wahusika kutozwa faini.

Alibainisha kuwa sheria ya kupambana na dawa za kulevya inaweka bayana kuwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya zenye thamani ya sh milioni 10 halina dhamana na kifungo chake ni maisha au kisichopungua miaka 20.

Alisema lakini mahakimu na majaji wamekuwa wakiwakatisha tamaa watendaji wa kitengo hicho kupambana na dawa za kulevya kwa kutoa dhamana kwa wahusika kinyume cha taratibu.

Alibainisha kuwa hivi karibuni waliwakamata raia wawili wa Pakistan na Watanzania wawili wakiwa na kilo 180 za dawa za kulevya lakini katika mazingira ya kutatanisha Wapakistan hao walipewa dhamana.

Naye Kamishna wa kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya, Godfrey Nzowa, alisema wanapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi na kitengo chake kimejitahidi kutovujisha siri za watoa taarifa.

Akihitimisha semina hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hivi sasa serikali inafanya mchakato wa kuanzisha mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Alisema kuwa pia inaangalia uwezekano wa kuanzisha mahakama ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Kubwa zaidi ni kwamba tutazifanyia marekebisho sheria zetu ili tuwape adhabu kali zaidi wanaofanya biashara hii, pia tutajenga vituo vya kuwahudumia watu walioathirika kwa utumiaji wa dawa hizo.

No comments:

Post a Comment