Monday, August 15, 2011

Bei ya petrol juu tena

BEI ya bidhaa ya petroli imepanda tena kwa zaidi ya Sh 100 kwa lita kuanzia Jumatatu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura) imetangaza Jumapili.

Kwa tangazo hilo la Ewura, katika Jiji la Dar es Salaam lita ya petroli imepanda hadi kufikia Sh 2,114 ambayo ni bei kikomo kutoka Sh 2,004 zilizotangazwa na Ewura Agosti 3, mwaka huu ambazo hata hivyo ziligomewa na wafanyabiashara.

Dizeli kwa bei ya rejareja sasa itauzwa Sh 2,031 kutoka Sh 1,911 huku mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 2,005. Kwa upande wa bei za jumla petroli itauzwa kwa Sh 2,046.62, dizeli itauzwa kwa Sh 1,963.81 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 1,937.90.

Wiki mbili zilizopita, Ewura ilitangaza bei hizo mpya ambazo ziligomewa na wafanyabiashara wa mafuta hadi Serikali ikatishia kuchukua hatua za kisheria dhidi yao ndipo baadhi yao wakalegeza msimamo.

Hata hivyo, Kampuni ya BP Tanzania iliendelea na msimamo wa kutouza mafuta kwa bei hiyo ya Serikali na kwa ukaidi huo tayari kampuni hiyo imefungiwa na Ewura kutojihusisha na biashara ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa miezi mitatu.

Hatua hii ya Ewura kupandisha bei tena ya mafuta ni wazi kuwa itazua manung’uniko kwa wananchi ambao walitarajia kuwa ile ahadi ya Serikali iliyoitoa wakati wa bajeti ya kushusha bei za bidhaa hiyo ingedumu kwa muda mrefu.

Meneja Biashara ya Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alitetea uamuzi wa kupandisha bei ya mafuta kuwa umetokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani pamoja na kupanda kwa kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Samwel alisema viwango vya bei zilizotumika katika soko la dunia zimepanda kwa wastani wa asilimia 5.42 na thamani ya Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa shilingi 47.12 kwa Dola moja ya Marekani.

Ewura pia imezidi kujitetea kuwa kanuni mpya ya kukokotoa bei za bidhaa hiyo bado inafanya mafuta kuuzwa kwa bei ya chini ukilinganisha na kanuni ya zamani. Samwel alitoa mfano kuwa iwapo Ewura ingetumia kanuni ya zamani ya kukokotoa bei mpya, petroli ingeuzwa kwa Sh 2,298.33, dizeli ingeuzwa Sh 2,213.36 wakati mafuta ya taa yangeuzwa kwa Sh 2,188.89.

“Bei za rejareja na za jumla zingepanda zaidi endapo furmula ya zamani ingeendelea kutumika,” alisema Meneja Biashara ya Petroli wa Ewura. Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Ewura ya mwaka 2008, bei za bidhaa ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na akaongeza kuwa mamlaka yake itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei za bidhaa za mafuta.

Hata hivyo, Samwel alitoa matumaini kwa Watanzania kuwa kuna uwezekano mkubwa baada ya wiki mbili bidhaa ya petroli ikapungua bei kutokana na bei katika soko la dunia kuanza kushuka.

“Bei itashuka iwapo Shilingi haitaporomoka zaidi, ila ikiendelea kuporomoka bei haitashuka sana,” alisema ofisa huyo wa Ewura. Akielezea hali ya biashara ya mafuta kwenye soko la ndani, alisema upatikanaji wa mafuta unaendelea vizuri kwani Ijumaa jumla ya lita milioni 9.5 zimeingizwa kwenye soko la ndani na juzi Jumamosi lita milioni 4.9 za bidhaa hizo ziliingizwa kwenye soko.

Alisema meli za mafuta zinaendelea kuingia nchini na zingine ziko bahari zikisubiri kupakua shehena hiyo. “Hivyo nawahakikishia kuwa upatikanaji wa mafuta utaendelea kuwa mzuri,” alisema. Kuhusu baadhi ya vituo vya Kampuni ya Total na Orxy kuendelea kutotoa huduma kwa wananchi, Ewura imeahidi kutoa tamko leo.

No comments:

Post a Comment