MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Pius Msekwa amemshambulia Mbunge wa Ngorongoro (CCM), Kaika Saning'o Ole Telele akisema kwamba kauli alizotoa bungeni dhidi yake ni fitina yenye uongo ndani yake. Kauli hiyo ya Msekwa imekuja wiki moja bada ya kulipuliwa bungeni na wabunge wa chama chake huku wale wa kambi ya upinzani wakimtuhumu kuingilia mamlaka ya kiutendaji ya Bonde la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), wakati si mtendaji. Baada ya kukaa kimya tangu kutolewa kwa madai hayo Agosti 18, mwaka huu, jana Msekwa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Hifadhi hiyo aliibuka mjini hapa kwa kuitisha mkutano na waandishi kwenye Ofisi za Makao Makuu ya CCM kufafanua tuhuma moja baada ya nyingine huku akiita maneno ya Telele kwamba: “Ni aina ya uongo unaoitwa usongombwingo". Msekwa alifafanua maana ya usongombwingo kuwa ni maneno ya uwongo yenye fitina ndani yake. Yaani siyo uongo wa kawaida, bali wenye lengo la kumfitini aliyetajwa." "Maneno yaliyonukuliwa na magazeti kwamba yalisemwa bungeni na Mheshimiwa Telele yalikuwa na lengo la kuchafua jina langu mbele ya umma. Yalikuwa ni maneno ya kashfa dhidi yangu, yaliyojikita katika kuchafua historia ya muda mrefu ya uadilifu wangu katika kutekeleza kazi za umma nilizopangiwa katika nyakati mbalimbali na marais wangu, kuanzia Rais Nyerere (Julius) hadi Rais Kikwete (Jakaya)." Alipoulizwa kwa nini amemzungumzia Telele peke yake wakati suala hilo lilisemwa na wabunge wengine, Msekwa alijibu: “Kwa sababu yeye ndiye aliyelianzisha, wengine walidakia na kuendeleza.” Kutohudhuria mjadala wizara Kuhusu kutokuwapo kwake kwenye mjadala wa hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Msekwa alisema bila shaka hoja hiyo inatokana na dhana mpya iliyojengeka ya kukusanya watu wengi Dodoma kwa gharama kubwa wakati wa mikutano ya Bunge la bajeti bila sababu za msingi. Alisema kwa kuwa tayari alikuwa amekutana na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, hakuona umuhimu wa kuwapo Dodoma na badala yake alipanga ratiba ya shughuli nyingine zinazohusiana na uenyekiti wake wa bodi. Alisema kazi hizo ni pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa hoteli za kitalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na siyo kugawa viwanja kwa wawekezaji pamoja na miradi mingine inayotekelezwa kwa fedha za NCAA ikiwamo Shule ya Sekondari ya Nainokanoka ambayo imekuwa ikijengwa kwa muda mrefu bila kukamilika. "Hii ni kazi muhimu zaidi kuliko kukaa tu kwenye Gallery ya Bunge na kulipwa posho za kusikiliza hoja mbalimbali za wabunge zinazoelekezwa kwa Waziri!," alisema Msekwa na kuongeza kuwa taarifa ya kazi zake hizo itawasilishwa kwenye kikao cha Bodi ya NCAA. Msekwa alisema kimsingi bajeti ya wizara ni sehemu ya Bajeti Kuu ya Serikali ambayo tayari ilishapitishwa na kwamba kazi wanayofanywa wabunge hivi sasa kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (b) cha Katiba ya nchi ni kujadili utekelezaji wa kila wizara. "Kwa hiyo hakuna kazi inayohitajika ya mwenyekiti kusaidia kuhakikisha kuwa bajeti ya wizara inapitishwa vizuri na Bunge, kwa sababu bajeti ya wizara inakuwa tayari imepitishwa wakati Bunge linapopitisha bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha," alisema. Alisema alipokutana na Kamati ya Bunge, alijibu hoja zote alizoulizwa na kamati hiyo na kwamba tuhuma zilizotolewa na Telele hazikujitokeza wakati huo na kwamba madai ya Telele kwamba alikwenda Ngorongoro kugawa maeneo ni lugha ya kuudhi ambayo inakatazwa na Bunge. Wakati Telele akichangia alisema wakati wenyeviti wenzake (Msekwa) wote wako Dodoma yeye alikwenda kutafuta maeneo ya kujenga hoteli... “Mwenyekiti wa Tanapa yuko hapa. Yeye hayumo humu, labda alijua kwamba tutazungumza huku. Lakini kule aliko anatusikia.” Jina la Rais Tuhuma nyingine ambayo Msekwa aliikanusha ni madai kwamba alitumia jina la Rais Kikwete kuhalalisha utoaji wa maeneo ambayo ni mapitio ya wanyama kujengwa hoteli. Alisema Desemba 28, 2006 alikutana na Rais Kikwete pamoja na Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Bernard Murunya wakati huo akikaimu nafasi hiyo na kiongozi huyo wa nchi aliwapa maagizo ambayo yaliwasilishwa kwenye mkutano wa bodi kwa waraka maalumu. “Katika waraka huo, maelekezo ya Rais kuhusu haja ya kuongeza idadi ya vitanda katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro yameainishwa waziwazi,” alisema Msekwa na kuongeza kuwa madai kwamba anatumia jina la Rais vibaya pia si ya kweli. Alisema maombi ya kujenga hoteli kwenye mapitio ya wanyama yaliwahi kutolewa na Bodi iliyokuwapo wakati huo kukubali, lakini utekelezaji wa mradi huo haukufanyika kutokana na katazo la Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC). “Tunaendelea kutekeleza uamuzi wa NEMC kwa kutoruhusu hoteli yoyote nyingine kujengwa katika mapitio ya wanyama. Ndiyo sababu katika orodha ya viwanja vilivyogawiwa na Bodi katika mkutano wake wa 87 wa Oktoba,2007, hakuna kiwanja chochote kilichopo kwenye mapitio ya wanyama kama Mheshimiwa Telele anavyodai,” alibainisha Msekwa. Kujifanya Mtendaji Msekwa alisema hajawahi kufanya kazi za watendaji na kwamba tuhuma hizo si za leo kwani zilianza muda mfupi tu baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi. Alisema baada ya siku 100 tangu kuteuliwa kwake, alimwandikia waraka Waziri husika ambaye wakati huo alikuwa Anthony Diallo akimweleza jinsi atakavyofanya kazi na kwamba amekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa ya bodi yake kila baada ya muda fulani kwa waziri. Mwenyekiti huyo wa NCAA alisema tuhuma hizo ziliendelea hata baada ya Waziri Jumanne Maghembe kuhamishiwa katika wizara hiyo na kwamba waziri huyo alifanya uchunguzi na kubaini kuwa hazina ukweli wowote. Msekwa aliongeza kuwa hata kikao cha bodi kilichojadili tuhuma hizo kilizitupilia mbali na kwamba anamshangaa Telele ambaye wakati huo alikuwa mjumbe kuziibua upya hali akifahamu kwamba zilikuwa zimeshawekwa kando. Alisema Ngorongoro haiwezi kufia mikononi mwake kwani tangu alipochukua uenyekiti wa chombo hicho ameongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato kutoka Sh17.79 bilioni mwaka 2005/06 hadi Sh48.7 katika mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2011. Msekwa alisema hasira dhidi yake zinazoonyeshwa na Telele huenda zinatokana na kutoteuliwa kuwa mjumbe wa bodi katika kipindi cha pili hivyo kuamua kuwashambulia watu ambao kimsingi hawahusiki na uteuzi huo. Kuhusu ombi la kuvunjwa kwa bodi hiyo Msekwa alisema: “Ni vyema (Telele) hilo ni jambo ambalo halitekelezeki kisheria,” na kwamba labda utumike ubabe kutokana na Sheria ya Mamlaka ya Ngorongoro kutompa Waziri uwezo wa kuivunja. Kilichosemwa Agosti 18 Akichangia hotuba ya Bajeti ya Maliasili na Utalii, Telele alisema Msekwa amekuwa akiingilia kazi za watendaji wa Ngorongoro kiasi cha kutoa ofa za ujenzi wa hoteli kwa wafanyabiashara katika Bonde la Ngorongoro na kwamba maeneo ambayo yanatolewa ni mapito ya wanyama aina ya faru. "Kwanza nadhani jambo hili aangalie tunaheshimu sana Chama cha Mapinduzi ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na maombi yanavyokuja ya kujenga hoteli wanasema Rais amesema, Rais gani anasema kwamba tujenge hoteli aende kinyume na taratibu zilizowekwa na wahifadhi na watalaamu wa hifadhi?" Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alisema: "Haiwezekani Mwenyekiti wa Bodi ya Ngorongoro ambaye moja ya majukumu yake ni kukagua hali halisi ya hifadhi hiyo, ajiingize pia katika shughuli za utendaji tena zilizo nyeti kama hizo." Aliitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya Msekwa kwa kukiuka mipaka ya majukumu yake na kwamba kambi ya upinzani ipo tayari kuipa Serikali ushirikiano kuhusiana na tuhuma hizo. Pia mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka akichangia hotuba hiyo alisema bodi hiyo ifumuliwe ili iundwe upya kwa maelezo kwamba ilikuwa imekiuka ushauri wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kuruhusu ujenzi kwenye njia za faru. |
Tuesday, August 23, 2011
Msekwa: Nimetupiwa fitina inayoitwa usongombwingo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment