Mbunge wa kike kutoka upinzani aliposimama kutoa mchango wake, wabunge wa CCM walimzomea kwa kumwita “shemeji”, “shemeji” ili aone aibu akae.
Nilijiuliza wabunge wa CCM wamefikia kiwango cha chini hivyo? Masikio ya Naibu Spika, Job Ndugai, kama wenyeviti wenzake, hayakusikia utoto, kejeli na mzaha ule ila aliona uvunjaji kanuni wa wapinzani.
Uvunjifu wa kanuni ndiyo kinga iliyobaki kwa wabunge wa CCM. Nje ya kanuni ni aibu tupu. Spika na wasaidizi wake hukimbilia kanuni kwamba hoja hii izungumzwe hivi na siyo vile ‘mpinzani’ wewe toka.
Wabunge na mawaziri wa CCM wanataka wapinzani watumie lugha ya staha, lakini mbunge wa Mtera, David Livingstone alipotaka wabunge wa upinzani wapimwe akili haikuwa lugha ya kuudhi. Ndiyo, kunya anye kuku, bata anaharisha.
Aliposema thamani ya shilingi inashuka kwa sababu ya picha za wanyama hakustahili kupimwa akili? Mbunge huyu hakumbuki noti ya Sh. 100 baada ya uhuru ilikuwa na picha ya simba na baadaye Mmasai?
Tuache. Leo CCM wanamwita mbunge shemeji kuzima hoja kwamba polisi walioua raia, mafisadi wa rada, waliotafuna fedha za EPA katika Benki Kuu (BoT), waliojigawia Kiwira, waliouza maelfu ya ekari za ardhi Mpanda na walioingia mikataba mibovu ya madini washtakiwe.
Kama hivi ndivyo, ushemeji bungeni ni janga jipya la kitaifa maana hakuna kitu kitakachojadiliwa kwa kina mpaka mashemeji wapende. Inawezekana ushemeji bungeni ndiyo kiini cha baadhi ya bajeti mbovu kupita kiulaini.
Lakini ni nongwa mbunge wa upinzani kuolewa na kumwoa mbunge aliyempenda kutoka CCM? Kama mbunge wa CCM, kwa ashiki zake, ameamua kutembea na mbunge wa upinzani ndiyo atangazwe kwa namna ya utoto vile?
Katika hili wabunge wa CCM wanamdhalilisha nani, yule mpinzani anayetembea na wa CCM au yule wa CCM anayetembea na wa upinzani? Kila mmoja anaweza kuwa na jibu lake, lakini mimi nasema kuwa wanaodhalilika ni wabunge wa CCM wanaokimbia hoja kwa kuingiza ushemeji.
Madhara ya utaratibu huu mpya wa uzomeji, wabunge watafanya kazi ya udaku, umbea, usalata muda mwingi kufikiria na kufuatilia nani ni hawara wa nani ili kesho yake adhalilishwe bungeni.
Watu huanza urafiki, upenzi na kuoana iwe bungeni au kazini. Anne Kilango-Malecela amesaidia kuboresha mada hii maana yeye, akichangia hoja baadhi ya masuala ya nyeti ya usalama yasijadiliwe hadharani ila yaishie katika Kamati ya Kudumu ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, alitoboa siri ya ndoa yake.
Alisema yeye alikuwa mjumbe katika Kamati ya Kudumu ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje ambayo mwenyekiti wake alikuwa mwanasiasa mkongwe, John Samuel Malecela.
“Huko ndiko nilikokutana na Malecela,” alisema mama yule huku ‘mashemeji’ wakicheka.
Kwenye Baraza la Mawaziri ndiko, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohamed Seif Khatibu alikomuopoa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda.
Samwel Sitta alipambana kivyake akafanikiwa kutetea Jimbo la Urambo Mashariki na akawa Spika wa Bunge la Tisa. Mkewe Margaret Sitta alipenya akaingia bungeni kupitia Viti Maalum halafu akateuliwa kuwa waziri.
Wengine waliowahi kuingia bungeni na wake ni William Shellukindo (Bumbuli) na mkewe Beatrice Shellukindo (Kilindi). Mzee Shellukindo hakurudi mjengoni safari hii ameangushwa na Januari Makamba.
Spika Sitta alijitahidi sana, kukaa kando kila Waziri Sitta (mkewe) alipowasilisha bajeti yake, lakini kila mmoja anakumbuka kwamba Pius Msekwa alikosa uvumilivu pale mkewe Anna Abdallah akiwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alipobanwa kwa maswali mazito.
Hizi ni ndoa rasmi, lakini zipo ndoa nyingi zisizo rasmi bungeni ambazo kwa utoto huu wa kuitana shemeji ili kuyeyusha hoja ipo siku spika na wenyeviti wataamua ugomvi.
jumwangul@yahoo.com
No comments:
Post a Comment