Monday, October 24, 2011
Askofu Mokiwa amtega Lowassa Urais 2015
Waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa akizungmza na mamia ya waumini wa kanisa la Anglikan kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari iitwayo Askofu John Sepeku ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam jana, Kushoto kwake ni Askofu wa kanisa hilo D Valentino Mokiwa
AMWAMBIA KAMA AKIINGIA IKULU AREJESHE SHULE ZA KANISA HILO, MWENYEWE AKWEPA KITANZI
Boniface Meena
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa amemwomba aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwamba endapo atafanikiwa kuingia Ikulu awarudishie shule zilizokuwa zikimilikiwa na kanisa hilo baada ya Serikali kuwa na idadi ya kubwa ya shule zake.
Kauli ya Dk Mokiwa inakuja siku chache baada ya Lowassa kuitisha mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwake Monduli, Arusha na kusema si sahihi kwa watu kuzungumzia mbio za urais wa 2015 wakati nchi imetoka kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Katika mkutano huo, Lowassa alisema watu wanapaswa kujikita katika mambo ya msingi, ikiwamo namna kuinua uchumi wa nchi badala ya kuendeleza mijadala ya urais wakati tayari yupo Rais Jakaya Kikwete aliyechaguliwa mwaka jana huku akiwa na miaka minne mbele.
Jana, Askofu Mokiwa akiwa katika Ibada ya Mavuno iliyoambatana na harambee ya kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya John Sepeku, Yombo Buza, Dar es Salaam alimwambia Lowassa: “Mungu akikujalia ukaingia Ikulu urudishe zile mali ambazo ni shule kwani kuna mali zetu nyingi.”
Dk Mokiwa aliongeza, “Tuziombee nia zote zilizo njema kwa kuwa shule zilichukuliwa tuliachwa na makovu na ilifikia sehemu watoto wa Anglikana walikuwa hawaruhusiwi kusoma katika shule hizo.”
Ombi kama hilo la Anglikana liliwahi kutolewa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambalo lilimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake kuwarejeshea shule zao zilizotaifishwa wakati wa Azimio la Arusha, lakini mkuu huyo wa nchi akiwa katika Baraza la Idd mjini Dodoma, alikataa ombi hilo akisema haliwezekani kwani kufanya hivyo ni kurejesha historia ya nchi nyuma.
Kauli hiyo ya Rais iliungwa mkono na Kanisa Katoliki ambalo lilisema kama ni madai ya kurejeshewa shule, lenyewe lingekuwa la kwanza kupaswa kulalamika kwani mali na shule zake nyingi ndizo zilizokuwa zimetaifishwa na kutaka madhehebu mengine kujikita zaidi katika ujenzi wa shule mpya.
Hata hivyo, jana Dk Mokiwa akikazia madai hayo katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Segerea alisema kuchukuliwa kwa shule hizo kuliwaacha na makovu hadi kufikia hatua wakati huo watoto wa madhehebu ya Anglikana hawakuruhusiwa kusoma katika shule nyingine.
Alisema shule hizo hazikuchukuliwa na Serikali kwa ridhaa yao na hivi sasa wanazihitaji kwa kuwa nchi imefikia miaka 50 ya uhuru.
“Mahali pa kanisa panaendelea kutishiwa, kanisa lirudishiwe shule na mali zake ili liweze kuwa mshindani wa Serikali katika kuboresha elimu kwani ingekuwa ni nchi nyingine, madhehebu yangekuwa yamekwenda mahakamani," alisema na kuongeza: “Serikali ijue ina mali ambazo si zake.”
Alisema kanisa lilikuwa linamiliki asilimia 50 hadi 60 za shule wakati huo lakini Serikali ilipozichukua ikiwaacha hivyohivyo: “Leo tumekutana na malengo ni kumalizia shule na mabweni ambayo hayana vyoo ya Shule ya John Sepeku na ndiyo maana mavuno ya siku hii ni ya kuchangia shule hiyo".
Dk Mokiwa alisema katika harambee hiyo walikuwa wakihitaji Sh100 milioni ili kumalizia ujenzi wa shule hiyo na kutaka aliye nacho asiogope kutoa.
Katika mahubiri yake, aliwataka waumini wachangie fedha za ujenzi huo bila kuogopa kuitwa mafisadi akisema mafisadi wa kweli walitakiwa kupelekwa mahakamani.
“Siku hizi watu wanaogopa kuchangia kwa kuogopa kuitwa mafisadi. Fisadi wa kweli si angekuwa amefungwa, leo hatuko yatima kwani tupo na wenzetu wenye uchungu na haya tunayoyasema,” alisema Dk Mokiwa.
Lowassa akwepa
Hata hivyo, Lowassa hakugusia ombi hilo la kurejesha shule hizo wala mpango wa kugombea urais wa 2015 baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wake.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lowassa alisema ni kweli shule za sekondari nyingi zilianzishwa na madhehebu ya dini. Hata hivyo, alisema Serikali nayo ilikuja kupata uwezo na ndiyo maana hivi sasa kuna shule ya sekondari kila Kata.
Lowassa alisema pamoja na kuwapo kwa shule nyingi, bado wanaomaliza masomo ya sekondari wengi hawaendelei mbele kitu ambacho alisema hakisaidii.
“Nadhani tatizo ni mfumo, hivyo tumesahau shule za ufundi ambazo zingeweza kuwasaidia hawa vijana wanaotoka sekondari,” alisema Lowassa.
Lowassa alitoa changamoto kwa madhehebu hayo kujenga shule za ufundi ili kuondoa tatizo la ajira ambalo linahitaji utaalamu: “Madhehebu ya dini yaanzishe vyuo vya ufundi kwa kuwa tatizo la ajira nchini kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka.”
Akianzisha harambee hiyo, Lowassa alisema amekuwa akialikwa kwenye harambee nyingi lakini hivi sasa ameweka sharti ambalo kama harambee lengo ni kufikia kiasi fulani, basi kanisa liwe limeshafanya jitihada za kupata kiasi kadhaa ili uchangiaji uanzie hapo.
Lowassa alichangisha kiasi cha Sh129.9 milioni, kati ya hizo, ahadi ni Sh60milioni na fedha taslimu zilikuwa ni Sh65 milioni. Mwenyewe alichangia Sh20 milioni.
Katika hafla hiyo, Lowassa alifuatana na mke wake, Regina pamoja na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Segerea ambaye alichangia Sh3milioni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment