Friday, October 28, 2011

Kisa na mkasa na Salim Kikeke

Simu mpya

iphone
iPhone 4
Simu mpya ya iPhone 4 imeonesha inaweza kufanya kazi za ukachero, baada ya bwana mmoja wa Marekani kumshika mkewe akiwa na mwanaume mwingine.

Programutumizi mpya iitwayo Find My Friends, ina uwezo wa kuonesha rafiki zako wako wapi imemsaidia bwana huyo kupata ushahidi kuwa mke wake ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.
Baada ya kufanikiwa kumkamata mkewe bwana huyo Thomas Metz aliandika kisa chake kwenye mtandao wa MacRomours.com. "Nilimnunulia mke wangu simu mpya ya iPhone na kuweka programutumizi hiyo bila ya yeye kujua" Amesema Thomas.

Bwana huyo amesema alikuwa akisikia tetesi kuwa mke wake ana mwanaume mwingine, lakini hakuwa akiamini jambo hilo.

Siku hiyo Bwana Thomas alituma text kumuuliza mke wake yuko wapi, na mke huyo kujibu kuwa yupo kwa rafiki zake. Hata hivyo kifaa cha kwenye simu kilikuwa kikionesha mke wake yuko katika nyumba ya mwanaume anayetajwa kuwa na mahusiano naye. Mtandao wa cnews.com umesema Bwana huyo sasa amesema anataka kumtaliki mkewe.

Mke kakata nanihii ya mume wake

Mkasi
Mkasi kama huu
Mwanamama mmoja nchini Vietnam amesema alikata uume wa mume wake kwa kutumia mkasi na kuutupa mtoni.

Habari zinasema sakata hilo liliibuka baada ya bwana huyo kutuhumiwa na mkewe kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine, na bwana huyo kujibu kwa kumpiga mangumi na mateke mke wake, Polisi wa Taiwan wameliambia shirika la habari la AFP.

Polisi wamesema mwanamke mwenye umri wa miaka thelathini aliyejulikana kwa jina moja tu la Pan, alikata karibu nusu ya uume wa mume wake.
Polisi hao wamesema tukio hilo limetokea katika mji wa Tainan, wakati mwanaume huyo akiwa amelala fo fo fo.

Bi Pan alijisalimisha mwenyewe kwa polisi na sasa anshtakiwa kwa makosa ya kujeruhi. Mwanamke huyo amesema aliutupa uume wa mume wake mtoni ili kulipiza kisasi. Hata hivyo polisi hawakusema mwanaume huyo anaendelea vipi.

Mwizi choka mbaya

Mwizi
Mwizi.. (lakini sio huyu)
Mwizi mmoja aliyejaribu mara kadhaa kufanya wizi na kushindwa kufanikiwa na jitihada zake hizo, aliamua kujisalimisha kwa polisi.

Polisi nchini Canada wamesema mtu huyo alijaribu mara tatu katika kipindi cha dakika kumi na tano kufanya wizi, lakini hakufanikiwa hata mara moja.

Polisi wamesema akiwa ameshika bastola aliingia katika duka moja katika kitongoji cha Peterbrough, mashariki wa jiji la Toronto na kutaka apewe fedha, lakini akaambulia patupu.

Dakika nane baadaye mwivi huyo aliingia katika duka jingine, ambapo wafanyakazi wa duka hilo walipoona ameshika bunduki, wote walijificha na hivyo akatoka bila chochote tena. Dakika tano baadaye, bwana huyo akamsimamisha mtu barabarani na kumuonesha bunduki na kumlazimisha ampe pesa na simu yake.

Hata hivyo polisi wamesema mtu huyo aliyesimamishwa aligoma kumpa chochote mwizi huyo. Mwizi huyo Derrell Kenneth kuona hivyo akaamua mwenyewe kwenda polisi na kujisalimisha. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kwa kosa na kutaka kufanya wizi kwa kutumia silaha.

Droo ya kwanza baada ya mechi 70

Ball
Mpira si mchezo
Timu moja ya vijana ya soka hapa Uingereza imepata pointi moja, na ya kwanza baada ya kucheza misimu minne bila kushinda mchezo hata mmoja.

Timu hiyo ya vijana chini ya umri wa miaka kumi na nne ilitoka sare ya mabao matatu kwa matatu na kuambulia pointi hiyo ya kwanza kabisa.

Gazeti la Telegraph limeripoti kuwa timu hiyo imepoteza mechi zake 70 na kufungwa magoli mia tano katika kipindi hicho. "Tunaona kama tumeshinda kombe la dunia" amesema Paul Chadwick, meneja wa timu hiyo.
Timu hiyo iitwayo Huncoat United inayocheza ligi ya vijana ya Accrington and District impoteza kila mchezo kwa wastani wa kufungwa magoli kumi na tano. Mchezo iliyochemsha zaidi ilifungwa mabao 25 kwa sifuri.
Mechi ambapo ilikuwa na nafuu ilikuwa kufungwa mbili bila. Licha ya kumaliza mkiani kila msimu katika ligi yao, meneja Paul amewapongeza wachezaji wake wa sare hii muhimu walioipata.

Na kwa taarifa yako.....
Takriban asilimia sabini ya dunia ni maji --- Ni asilimia moja tu ya maji hayo yananyweka.
Tukutane wiki ijayo....... Panapo Majaaliwa..

No comments:

Post a Comment