Thursday, October 20, 2011

Lowassa- Simuhujumu Kikwete


“SILIKA yangu kama mwanasiasa na mtu mwenye dhamana kubwa kwa watu wa Monduli na kwa Taifa langu, haiwezi kamwe kunituma nianze kupanga mikakati ya kumhujumu kiongozi wetu mkuu au chama ambacho kimenilea na nikakitumikia kwa uadilifu na kwa juhudi kubwa,
pengine kuliko ilivyo kwa hao wazushi.”

Ni kauli ya Waziri Mkuu wa zamani, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kwa waandishi
wa habari jimboni mwake jana, alipozungumzia tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake na
wapinzani wake kupitia vyombo vya habari.

“Ndugu wana habari, nitakuwa mtu wa mwisho kufikiria au kupanga kumhujumu Mwenyekiti wetu wa Chama na Rais (Jakaya Kikwete) ambaye nimemwunga mkono kwa dhati kwa muda mrefu na kushirikiana naye katika harakati nyingi za kifikra na za kiuongozi, katika ngazi mbalimbali na kwa miaka mingi. Nilipata kulisema hili na leo nalirudia. Mimi na Rais Kikwete
hatukukutana barabarani,” aliongeza Lowassa kwa hisia kali.

Alifikia kutoa kauli hiyo baada ya kueleza kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie
madarakani kuna kundi la watu limekuwa likifanya juhudi kubwa kumgombanisha na Rais, likitumia kila aina ya hoja za kupikwa.

Alisema kundi hilo ambalo sasa limekuja na uzushi mpya, ndilo ambalo mwaka juzi lilipenyeza ndani ya chama na katika jamii, hoja kwamba alikuwa amejipanga kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, na kwamba alikuwa na malengo ya kumpinga Rais Kikwete ambaye wakati huo alikuwa ndiyo kwanza anaelekea kukamilisha ngwe yake ya kwanza madarakani.

“Katika kuthibitisha kwamba watu hao walikuwa na hila, nilipohojiwa na waandishi wa
habari Dar es Salaam miezi kadhaa kabla ya Uchaguzi Mkuu, nilijibu kwa kifupi nikisema,
hatukukutana na Rais Kikwete barabarani.

“Nayasema haya na kurejea baadhi ya mambo huku nikiwa na imani ya dhati kabisa, kwamba
viongozi wenzangu ndani ya CCM na walio na nia njema na chama chetu na Taifa hili, akiwapo Mwenyekiti wetu wa Taifa, Kikwete, hawawezi kamwe kuamini au kushawishiwa na propaganda chafu zinazoendeshwa na kikundi kidogo chawanasiasa hao, kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, ambao malengo yao ya kisiasa yako wazi na yanayojulikana,” alisema bila kuwataja wanasiasa hao.

Lowassa aliingia katika matatizo mwaka 2008 baada ya kuibuka kashfa ya kampuni ya kufua
umeme wa dharura ya Richmond, ambapo alilazimika kujiuzulu baada ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza suala hilo, hasa utoaji zabuni, kumtaja kuwa alishinikiza kampuni hiyo kupewa zabuni.

Hata alipoulizwa swali kuhusu Richmond na malipo ya Dowans, Lowassa alisema kwa sasa
hawezi kulizungumzia hilo, lakini utafika muda atalizungumzia kwa mapana na marefu.
Madhambi ya JK

Alishangaa pia kusikia kuwa amejipanga katika mkutano ujao wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya CCM, kuwasilisha orodha ya madhambi yaliyofanywa na Mwenyekiti Kikwete.

“Kuhusu hili napenda kusema kwa uwazi, kwamba mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria
hata mara moja kuhusu hicho wanachokiita mabaya au madhambi ya Rais, sina na wala siijui
hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete,” alisema.

Aliwataka viongozi wa chama na wa Serikali kumsaidia Rais na CCM kwa kutimiza ipasavyo
wajibu wao, badala ya baadhi yao tena wakiwamo wenye dhamana nyeti, kuwa vinara wa kutunga mambo ya kufikirika.

Alisema kwa nafasi alizopata kuwa na nazo na alizonazo sasa, anatambua na kuiheshimu kwa
dhati kazi kubwa inayofanywa kwa weledi mkubwa na taasisi za Dola zenye wajibu wa
kuhakikisha ulinzi na usalama wa viongozi na Taifa kwa jumla.

Alisema tofauti na nchi alizopata kutembelea hivi karibuni, kinachofanywa nchini hasa na
wanahabari na wanasiasa ni kutumia muda mwingi kujadili watu na propaganda za kisiasa zisizo na tija, wakati wakitambua kwamba, Taifa linakabiliwa na changamoto nyingi.

Alizitaja baadhi yao kuwa ni pamoja na za kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi,
kuimarisha mifumo ya utawala bora, kuporomoka kwa thamani ya shilingi kila kukicha, mdororo wa uchumi, tatizo kubwa la ajira kwa vijana, kushuka kwa kiwango cha elimu na ugumu wa maisha kwa jumla.

Hivi karibuni katika Mkutano wa Bunge la Bajeti, Dodoma, Lowassa aliwanyooshea vidole
viongozi wa kitaifa, akiwaambia kwamba wanashindwa kuchukua uamuzi mgumu wa
kuwatatulia wananchi matatizo yao.

Aliwatuhumu wanasiasa wanaotumia jina lake kama ajenda ya uzushi wa kila namna, kuanza
sasa kumhusisha hata na matukio ya kisiasa kama yaliyotokea hivi karibuni jijini Arusha, yakimhusisha Mwenyekiti wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) mkoa wa Arusha, James ole Millya.

Hivi karibuni, Mwenyekiti huyo wa UVCCM alidai kwamba kuna mtoto wa kigogo (bila kumtaja jina), aliyeingilia mambo yao Arusha na hivyo kufanya Polisi kuzuia maandamano yao.

Lowassa alisema viongozi wa UVCCM Arusha kama wamevunja sheria wanapaswa
kuchukuliwa hatua kali na kama wanachodai kina msingi pia wanapaswa kusikilizwa na si
kupuuzwa.

Alikumbusha kuwa UVCCM ni jumuiya ya vijana wengi wenye damu changa na wanaweza
kuwa na mawazo mazuri ama mabaya, lakini viongozi wa juu wa chama wanapaswa kuwasikiliza na kuona mawazo yao kama yana busara au la, na si kuwapuuza.

‘’Suala hapa si kuwapuuza bali ni kuwasikiliza ndani ya vikao na kusutana humo humo na hiyo ndio njia pekee ya kutatua matatizo ya jumuiya za chama,‘’ alisema.

“Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua kuanza kuchukua hatua za kisiasa na kisheria, ambazo naamini zitatoa majibu sahihi dhidi ya walio nyuma ya ajenda hizi chafu, kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawa ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya Watanzania, ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi na wakati mwingine ya hatari dhidi yangu,” alisema Lowassa.

Alisema amepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka husika, zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza la Habari Tanzania.

Akizungumzia harakati za kuwania urais mwaka 2015, Lowassa alisema kwa sasa anachojua ni kwamba bado kuna miaka minne mbele.

Mbali na miaka hiyo, Lowassa pia alisema kuna rais yuko madarakani na kamwe hawezi
kuzungumzia hilo kwa sasa, kwani ni ukiukwaji mkubwa wa utaratibu kichama.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alizungumzia pia afya yake na kusema yuko imara na hajapooza kama watu wanavyozusha.

Alisema taarifa kuwa yeye ni mgonjwa, amepooza mwili na hawezi kutembea ni uzushi
unaopaswa kupuuzwa kwa nguvu zote na kuongeza kuwa anamshukuru Mungu kwa kuwa
na hali nzuri kiafya na salama.

Lowassa amekuwa akitajwa mara kwa mara na baadhi ya vyombo vya habari wakiwamo viongozi wa chama chake, kwamba ni mmoja wa viongozi wanaopaswa kukaa pembeni chini ya falsafa yao ya kujivua gamba.

No comments:

Post a Comment