WAKATI mabaki ya miili ya watu 12 walioteketea kwa moto katika ajali ya basi la Deluxe yakizikwa jana, mmoja wa abiria waliokufa katika ajali hiyo, Salome Benjamin (24) alitoa simu yake itumike kutoa taarifa kwa ndugu zake.
Salome, mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma, ameelezwa kuwa aliwapa mashuhuda hao simu hiyo na kuwataka wawasiliane na ndugu zake kwamba imeshindikana kwake kuokolewa hivyo wasihangaike.
Akisimulia jana jinsi mwanawe alivyokufa, baba mdogo wa Salome, Michael Isamuhyo alisema shuhuda aliyetumia simu ya mwanawe aliwaeleza kuwa, Salome kabla ya kufa, aliwataka wasihangaike.
Isamuhyo aliyezungumza na gazeti hili, alisema shuhuda huyo aliwaeleza kuwa Salome kabla ya kufa alitokea dirishani upande wa kulia na kupiga kelele ya kuomba msaada.
Shuhuda huyo kwa mujibu wa Isamuhyo, alisema walikwenda kumsaidia lakini walishindwa kwa kuwa alinasa sehemu ya miguu ndani ya basi hilo.
“Shuhuda alituambia kuwa, wakati wanamvuta, walibaini kuwa hawataweza kumuokoa kwa kuwa sehemu ya miguu ilinasa na alipoona hawezi kuokolewa, alirusha simu nje kwa shuhuda huyo.
“Baada ya kutoa simu hiyo, alimtaka atueleze sisi ndugu zake kuwa ameshindikana kuokolewa ili tusihangaike,” alieleza kwa uchungu Isamuhyo.
Baba wa Salome, Benjamin Magige akizungumzia msiba huo alisema; “Nimempoteza mtoto wangu wa pekee wa kike, nimebaki na mdogo wake wa kiume tu, walikuwa wawili pekee, nina uchungu sana.
“(Salome) alikuwa amalize chuo keshokutwa tu, ni maumivu makubwa kwa familia, mama yake kaja lakini hawezi kuzungumza, huu si wakati wa Serikali kufumbia macho ajali hizi, tuumie wote na tuhakikishe zinakoma,” alisema Magige huku akilia.
Maiti hao walizikwa katika makaburi yaliyochimbwa kwa kuambatana katika eneo la Air Msae walipozikwa abiria 25 waliokufa katika ajali ya basi ya Air Msae mwaka 1999, umbali wa kilometa takribani 10 kutoka ilipotokea ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment