Wednesday, October 5, 2011

JWTZ wanasa maharamia 7 waliotaka kuiteka meli


JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewakamata maharamia saba baada ya jaribio lao la utekaji meli kaskazini mashariki mwa Kisiwa cha Mafia kushindikana.

Maharamia hao wanasadikiwa kuwa ni wa Somalia.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe, alisema maharamia hao walikamatwa juzi saa 3 usiku, umbali wa kilometa 40 mwa visiwa hivyo vya Mafia mkoani Pwani.

Alisema maharamia hao wakiwa na silaha waliivamia meli hiyo iitwayo Sam-S-Allgood, inayofanya utafiti wa mafuta katika eneo hilo kwa lengo la kuiteka, lakini walishindwa kufikia kusudio hilo baada ya meli zingine mbili zinazofanya shughuli hiyo kuwahi kutoa msaada.

Kanali Mgawe alisema baada ya kuona kuwa wamevamiwa, walitoa ishara ya kuashiria kuwa wamepatwa na tatizo, na meli mbili zilizokuwa katika eneo la jirani huku zikiwa na wanajeshi ndani yake, zilikwenda na kutoa msaada.

“Meli hizi moja iitwayo Froshibre na nyingine Monck, zikiwa na vikundi vya wanajeshi, zilifika na kuwasha taa kubwa katika meli iliyotekwa na kuwaona maharamia hao wakitembea nje ya meli hiyo ambapo walirusha risasi hewani ili kuashiria wajisalimishe,” alisema Mgawe.

Alisema baada ya kuona hali hiyo, maharamia hao nao walianza kuwarushia risasi, jambo lililowafanya wanajeshi kujibu mapigo na kwamba baada ya dakika chache, maharamia walitupa bunduki zao baharini na kusalimu amri kwa kunyoosha mikono juu.

Alisema baada ya hapo, wanajeshi waliisogelea meli hiyo kwa karibu na kuwafunga kamba maharamia hao, huku mmoja akiwa amejeruhiwa paja la kulia.

Aidha, Kanali Mgawe amewataka wananchi kutambua kuwa JWTZ ipo imara kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi unalindwa kikamilifu.

Pia wamewaagiza askari waliopo katika mazoezi na meli ya Sas Drakensburg, kufanya doria katika maeneo ya bahari ili kuibaini boti waliokuwa wakiitumia maharamia hao ambayo inadaiwa kuwa waliiacha majini.

Kanali Mgawe alisema maharamia hao walitarajiwa kufikishwa jijini Dar es Salaam jana kutoka Mafia.

Kumekuwapo na matukio mbalimbali ya utekaji nyara katika Bahari ya Hindi maeneo ya kuanzia Ghuba ya Aden kunakofanywa na wapiganaji wa Kisomali wa kundi la Al Shabaab na kusababisha mauaji na utekaji nyara, na pia kusababisha gharama za maisha kuwa juu.

Katika hatua nyingine, Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), zimetakiwa kuendelea kujenga mshikamano wa pamoja katika mapambano dhidi ya maharamia ili kuziwezesha kukua kiuchumi.

Mwito huo umetolewa jana na Kiongozi wa Mazoezi ya Kijeshi, Meja Jenerali Karl Wiesner kutoka Afrika Kusini, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu mazoezi kwa wanajeshi kutoka nchi wanachama wa SADC.

Meja Jenerali Wiesner ambaye pia ni kiongozi wa meli ya SAS Drakensburg inayoongoza mafunzo hayo, alisema lengo la mazoezi hayo ni kuwawezesha wanajeshi wa Sadc kukabili uharamia unaoendelea katika Bahari ya Hindi.

Alisema nchi za Sadc ili ziweze kukabiliana na vikwazo vya ukuaji kiuchumi, hazina budi kuhakikisha kuwa zinaendelea kujenga ushirikiano katika nyanja zote ikiwamo ya ulinzi baharini ili kupambana na uharifu unaofanywa na maharamia katika maeneo hayo.

“Huwezi ukafanya biashara kwa kupitia bahari kama kuna maharamia, kwa sababu hiyo uchumi wa nchi hizi hauwezi kukua, kama tunataka haya yote kufanyika maeneo ya bahari yetu ni lazima yawe salama,” alisema.

Alisema kama ushirikiano hautafanyika katika kuwadhibiti maharamia kwa kushindwa kuyaweka salama maeneo ya bahari, biashara zinazofanyika kwa kutumia bahari, hazitoweza kufanikishwa hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya nchi wanachama.

Alisema maeneo ya bahari yamekuwa ni kivutio kikubwa kwa maharamia pasi na kutaka kujua kuwa linamilikiwa na nchi ipi, kwa hiyo ni vyema nchi husika zikajipanga kuhakikisha zinalinda kwa pamoja maeneo hayo ili kuondokana na hatari ya maharamia hao.

Akiyazungumzia mazoezi, Weisner alisema yanafanywa na wanajeshi wapatao 500 na yatakuwa ya muda wa siku tano.

No comments:

Post a Comment