MWIVI MVIVU
Mwizi mmoja nchini Marekani amekamatwa, baada ya kupitiwa na usingizi ndani ya nyumba aliyoingia kufanya wizi wake.
Hata hivyo, baada ya kuoga na kujitupa kitandani alipiiwa na usingizi mzito, hadi alipokutwa na wenye nyumba.
Luteni Steve Kenney wa idara ya polisi ya Wichita amesema, mwizi huyo alikutwa akiwa amezungukwa na vitu alivyopanga kuviiba pembeni mwa kitanda alichokuwa amelalia.
"Baada ya kukusanya vitu alivyotaka kuviiba, alienda bafuni kuoga na kuingia kitandani kulala" amesema Luteni Steve. Mwizi huyo alikurupushwa na wenye nyumba, waliokuwa na mshangao baada ya kukuta mtu wasiyemfahamu akiwa kalala kitandani mwao.
USIOGOPE SIMU
Serikali ya Nigeria imetoa tangazo kuwahakikishia wananchi wake kuwa hawawezi kufa kwa kupokea simu.
Tume ya mawasiliano ya Nigeria imesema "ni jambo lisiloweza kufikirika kuwa mtu atakufa kwa kupokea simu".
Msemaji wa tume hiyo Rueben Muoka amesema "Ni watu wanaodanganywa kirahisi ndio wanaweza kuamini uvumi huu."
MTOTO KWA MAMA HAKUI?
Bwana mmoja na mkewe nchini Italia wametafuta msaada wa kisheria ili kumshawishi mtoto wao mwenye umri wa miaka 41 kuhama na kutafuta makazi yake mwenyewe.Wazazi hao ambao hawakutajwa majina, wamesema mtoto wao wa kiume ambaye anafanya kazi amegoma katakata kuhama nyumbani kwa wazazi wake, na bado anataka kufuliwa nguo zake na kupikiwa chakula na wazazi wake. Wazazi hao sasa wametafuta ushauri wa kisheria.
Mwanasheria Andrea Camp amesema wametuma barua kwa mtoto huyo na kumtaka ahame katika kipindi cha siku sita, la sivyo atakabiliwa na hatua za kisheria. Iwapo atagoma kuhama, wanasheria wataomba mahakama mjini Venice kutoa amri ya kuwalinda wazazi hao dhidi ya mtoto wao.
"Tumechoka, na mambo haya" amekaririwa baba wa bwana huyo.
"Yaani ana kazi nzuri lakini hataki kuhama na kuanza maisha yake" amesema mzee huyo. Mzee huyo amesema mtoto wao huwataka wafue nguo zake, na kuzipiga pasi na pia kumtayarishia chakula.
"Nadhani hana nia ya kuhama" amesema baba wa mtoto huyo mwenye miaka arobaini. Hata hivyo wanasheria wamesema familia nyingi nchini himo zinakabiliwa na tatizo hilo.
MAPENZI KIZUNGUZUNGU
Mwanamama mmoja nchini Brazil alituma mtu akamuue mwanamke aliyekuwa akitembea na mume wake, lakini kwa bahati mbaya au nzuri muuaji huyo akajikuta akipendana na mtu anayetakiwa kumuua.
Mwanamama huyo alihisi kuna mwanamke anayemchukulia mume wake, na hivyo kutafuta mtu atakayemuua mwanamke huyo.
Mke huyo mwenye wasiwasi alitafuta mtu wa kazi, lakini bwana huyo aliyepewa jukumu la kuua, alipendana ghafla na mwanamke anayetakiwa kumuua.
Ili kumaliza sakata hilo bwana huyo aliamua kumpaka rangi nyekudu iliyofanana na damu na kumpiga picha mwanamke huyo na kuituma kwa mwanamama aliyemtuma. Bwana huyo alimwambia tayari amekamilisha kazi.
Hata hivyo mwanamama aliyeagiza mauaji kufanywa aliwafuma mitaani na kwenda kushtaki polisi. Polisi wamewakamata watatu hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
RAIA WA DUNIA
Mwanamama mmoja wa Ufilipino amejifungua mtoto wake ndani ya ndege ikiwa angani kutoka Ufilipino kwenda Marekani.Mwanamama huyo Aida Alamillo aliyekuwa amebakiza siku nane kabla ya tarehe yake ya kujifungua, aliruhusiwa na dakrtari wake kusafiri, lakini alipatwa na uchungu ndege ilipofika angani.
Baada ya kuanza kusikia uchungu, aliwaita wafanyakazi wa ndani ya ndege ambao kwa kushirikiana na baadhi ya abiria wenye uzoefu wa ukunga, wakamsaidia kujifungua mtoto wa kiume.
Hata hivyo suala la uraia wa mtoto huyo ndio limezua utata, kwani mtoto huyo amezaliwa katika anga la kimataifa, ambalo halimilikiwi na nchi yoyote duniani.
Sheria nyingi duniani zinasema popote mtoto atakapozaliwa, atapewa uraia wa nchi alikozaliwa. Mwana huyu kazaliwa ndani ya ndege...
SHINDA BUNDUKI
Watoto nchini Somalia wamekuwa wakipewa zawadi za bunduki na fedha taslimu katika mashindano kupitia radio yaliyoandaliwa na kundi la Al Shabaab.
Taarifa zinasema mshindi wa kwanza katika shidnao hilo amezawadiwa bunduki aina ya AK47 na fedha taslimi dola mia saba.
Mshindi wa pili naye amepatiwa AK 47 na dola mia tano huku watoto waloshika nafasi ya tatu wamezawadiwa mabomu mawili mawili na dola mia nne.
Washindi wengine wamepatiwa vitabu vya kidini. "Vijana hawana budi kutumia mkono mmoja kwa ajili ay elimu na mwingine kutumia bunduki" amesema afisa wa ngazi ya juu wa Kundi la Al Shabaab, Mukhtar Robow, mjini Mogadishu.
Mwandishi wa BBC mjini humo amesema huu ni mwaka wa tatu mashindani kama haya yanafanyika.
No comments:
Post a Comment