Saturday, October 8, 2011

Vituko Nishati na Madini

  • David Jairo aondoka na funguo za ofisi
  • Wengine wahoji miaka 20 ni ya dharura gani?
  • Vigogo wahaha Symbion ipewe mkataba wa miaka 20
HUKU Bunge likichunguza madai ya kuwapo fedha zilizogawiwa kwa Wabunge kutoka Wizara ya Nishati na Madini, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayehusishwa na sakata hilo, David Jairo, ameifunga ofisi aliyokuwa akitumia na anayekaimu nafasi yake anatumia moja ya ofisi za makamishina, imefahamka.

Habari zilizothibitishwa na maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini, zimeeleza kwamba ofisi hiyo kwa sasa haitumiwi na Kaimu Katibu Mkuu, Eliakim Chacha Maswi kwa maelezo kwamba bado ina vitu vya Jairo.
Maswi anatumia ofisi za aliyekuwa Kamishna wa Madini Dk. Peter Kafumu, ambaye sasa ni Mbunge wa Igunga aliyeshinda uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo, Jumapili iliyopita.
 
Raia Mwema lilipofika katika ofisi za Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Jengo la Tanesco, mtaa wa Samora, Dar es Salaam ghorofa ya tano lilimkuta katibu muhtasi, huku ikionekana kwamba ofisi za Katibu Mkuu zimefungwa na katibu huyo akaelekeza kwamba Kaimu Katibu Mkuu anapatikana ghorofa ya nne.
Mwandishi wa Raia Mwema alipofika ghorofa ya nne kwa Kaimu Katibu Mkuu Maswi, alimkuta akiwa katika ofisi za ‘Kafumu’, lakini akakataa kuzungumzia sababu za yeye kufanyia kazi katika ofisi hizo akidai haoni tatizo lolote kwa vile anapata ushirikiano wote anaohitaji katika utendaji wake wa kazi za kila siku tokea apangiwe kazi katika wizara hiyo.

“Mimi sina la kusema kwa kuwa nimepangiwa hapa na nilipofika nimepewa hii ofisi ambayo kama unavyoiona inanitosha na naendelea na kazi zangu kama kawaida,” alisema Maswi kwa ufupi.
Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Nishati na Madini, Theresia Mghanga aliliambia Raia Mwema wiki hii kwamba, katika ofisi za Katibu Mkuu kuna vitu vya Jairo ambavyo hakuna mtu anayeweza kuvivuruga kwa maelezo kwamba kwa sasa Jairo yuko likizo na bado ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.

Mghanga alipoulizwa kwanini ofisi za Katibu Mkuu zimefungwa na Kaimu Katibu Mkuu anatumia ofisi nyingine, alisema; “Kwani ulielekezwa wapi na walinzi? Kama walikuelekeza ghorofa ya tano walikosea. Kaimu yuko ghorofa ya nne, ndipo anapopatikana. Kule (Kwa Katibu Mkuu) kuna vitu vya watu ambavyo vimekaa vibaya na mwenyewe yuko likizo.”

Alipoelezwa kwamba hiyo ni ofisi ya umma na inatakiwa kutumiwa na yeyote na kwamba kuna taarifa kwamba Jairo ameondoka na funguo, alisema; “nani kakwambia…. Kwanza hayo mambo yana faida gani? Sisi tuna utaratibu wetu wa kufanya kazi.”
Mtumishi mmoja wa Wizara ya Nishati na Madini, ambaye amekuwapo katika wizara hiyo kwa zaidi ya miaka 15, ameliambia Raia Mwema wiki hii kwamba ilipata kutokea katika ofisi za wizara hiyo za zamani zilizokuwa Mtaa wa Mkwepu, ofisa mmoja kugomea kutoa funguo za ofisi kabla ya uongozi wa juu wa wizara kuamuru kuvunjwa kwa mlango.

“Nakumbuka tulipokuwa Mkwepu kuna ofisa aligoma kutoa ufunguo wa ofisi na nina wasiwasi alikuwa ni Jairo wakati huo, kabla ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Patrick Rutabanzibwa kuamuru mlango uvunjwe na kitasa kibadilishwe ili ofisa anayehamia aweze kufanya kazi. Nadhani kama kweli mtu hayupo aachie ofisi za Serikali,” alisema mtumishi huyo ambaye ni wa ngazi ya chini.
Taarifa zaidi ambazo Raia Mwema limepata zinasema suala hilo la funguo za ofisi huenda likawa limefikishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambako inadaiwa kasi ya kulishughulikia si nzuri.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Mbunge wa Tunduru (CCM) Ramo Makani, Luhanjo na Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja ni kati ya watakaohojiwa katika sakata hilo la Jairo.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, kazi hiyo inaelekea kukamilka ili ripoti ya kamati iandaliwe na kisha iwasilishwe bungeni mwezi ujao.

Taarifa zaidi zilizotufikia zinaeleza kuwa miongoni mwa kundi hilo la viongozi 20 waliohojiwa wamo baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa baadhi ya taasisi za umma.
Mbali na Luhanjo, Ngeleja na Jairo mwenyewe, wengine waliotarajiwa kuhojiwa ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh ambaye ripoti yake ndiyo iliyotumiwa na Luhanjo kumsafisha Jairo kabla ya hatua ya Rais Jakaya Kikwete kumsimamisha tena.

Awali Luhanjo kwa mamlaka yake alimsimamisha kazi Jairo baada ya sakata hilo kuibuka bungeni na akamwagiza Utouh kuchunguza.

Kamati hiyo Teule ya Bunge iliundwa kutokana na Azimio la Bunge la Agosti 24, mwaka 2011. Azimio hilo lilitaka kuundwa kwa kamati hiyo ili kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini, kuchangisha fedha kwa ajili ya “kupitisha bajeti”.

Mbali na hilo, azimio pia lilitaka Kamati ichunguze kama kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi, kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizokuwa zikichangishwa na wizara hiyo, kimeingilia na kuathiri madaraka ya Bunge.

Kamati hiyo teule ya Bunge imeundwa kwa mujibu wa kanuni ya 2(2) na 117(4) ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007, ikiwa na hadidu rejea mahsusi ambazo ni:
Kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.

Kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni, iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.

Kupitia taarifa ya CAG kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Katibu Mkuu Kiongozi juu ya Jairo kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ili kufanikisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara Bungeni.
Kuchunguza mfumo wa Serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kuarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.

Hadidu nyingine ni:
Kuchunguza kwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Katibu Mkuu Kiongozi katika suala la Jairo na kubaini iwapo utaratibu huo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge.
Kuangalia nafasi ya Mamlaka ya Uteuzi kwa ngazi za makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua. Nyingine ni kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na uchunguzi huo.

Wakati hayo yakiendelea, kuna taarifa za kutatanisha kuhusu shinikizo kubwa la kutaka kampuni ya kufua umeme wa mafuta ya Kimarekani ya Symbion Power ipewe mkataba wa miaka 20 wa kufua umeme na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kwamba shinikizo hilo la kisiasa limekumbana na vizingiti kutoka kwa baadhi ya wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco ambao wanasema hakuna dharura ya miaka 20.
Ofisa mmoja wa Tanesco amesema kwamba anachofahamu ni kuwapo kwa mkataba wa mwaka mmoja hadi miwili na si miaka 20, lakini akatahadharisha kwamba “lolote linawezekana, tusipokuwa makini.”
 Imeelezwa kwamba kuwapo kwa shinikizo hilo kunatokana na nguvu kubwa ya wanasiasa kuzidi kujipanga kutafuta fedha zitakazowawezesha kufanikisha malengo yao ya kisiasa mwaka 2015.

Katika maelezo yake bungeni wakati wa Bunge la Bajeti lililomalizika karibuni, Waziri Ngeleja aliahidi kwamba kutakuwa na uzalishahji wa megawati 112 za umeme mwishoni mwa mwezi Agosti kwa kuzingatia mkataba kati ya Serikali na kampuni ya Symbion Power.

Lakini kabla ya uzalishaji huo kutimia sasa vigogo, taarifa zinasema, wanaandaa mpango wa kuipatia Symbion mkataba wa miaka 20 kimsingi ukiwa na maana kwamba nchi itaendelea kutegemea umeme wa mafuta na hivyo kuwa katika mgao kwa kipindi kirefu kijacho badala ya kutumia rasilimali nyingine kama gesi ambayo ni nyingi nchini au mkaa wa mawe.

Symbion inayoongozwa na Wamarekani waliopata kufanya kazi nyingi za serikali yao, ilinunua mitambo iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni tata ya Dowans Tanzania Limited, na ikatangaza kuwa haihusiki na kashfa zozote zilizotokana na kampuni zilizotangulia katika mradi huo.

Kwa mujibu wa Ngeleja, kampuni ya Symbion imesaini mkataba na Serikali ili izalishe megawati 205 za umeme kati ya sasa na Desemba zikiwemo megawati 45 zitakazozalishwa Septemba, 110 Oktoba na megawati 50 Desemba.

Mbali ya Symbion Ngeleja alisema Tanesco na kampuni ya Aggreco International wamesaini mkataba wa kuzalisha megawati 100 za umeme, mitambo imeshaletwa nchini, imeanza kufungwa, na kwamba, wahusika wametakiwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuharakisha utekelezaji.

Serikali imetangaza mpango wa dharura wa kumaliza mgawo wa umeme nchini utakaowezesha kuzalisha megawati 572 za nishati hiyo kati ya Agosti na Desemba mwaka huu kwa gharama za Sh bilioni 523 ambazo Tanesco imekopa fedha hizo kwa kudhaminiwa na Serikali.

Pamoja na mipango hiyo mingi hali haionyeshi kama mgao wa umeme unaotafuna uchumi wa nchi kila kukicha unakaribia kwisha.

No comments:

Post a Comment