Thursday, October 6, 2011
Mgombea CUF Igunga akumbwa na tuhuma
Waandishi Wetu
SIKU chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, inadaiwa kuwa aliyekuwa mgombea wa CUF, Leopold Mahona alitoa taarifa katika fomu ya uteuzi wake zinazopingana na zile alizotoa alipowania nafasi hiyo mwaka jana.Taarifa hizo zinazokinzana zinadaiwa kuandikwa na Mahona katika fomu za uteuzi wake zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambazo humtaka mgombea kueleza mambo mbalimbali.
Fomu inayoelezwa kujazwa tofauti na Mahona ni namba 8B ambayo hujazwa na wagombea wakiomba kuteuliwa kuwania ubunge chini ya Kanuni ya 31 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge ya mwaka 2010, ambayo huambatanishwa na tamko la kisheria la mgombea ambalo huthibitishwa na hakimu kwa mujibu wa sheria.
Katika fomu zake za mwaka huu, Mahona ametoa taarifa za kuzaliwa kwake akisema kwamba alizaliwa katika Halmashauri ya Igunga, Tabora, Tanzania Julai 4, 1981 maelezo ambayo yanatofautiana na yale yaliyoko katika fomu ya mwaka jana ambayo yanaeleza kwamba alizaliwa siku, mwezi na mwaka huohuo, lakini huko Kibondo, Kigoma Tanzania.
Katika fomu ya mwaka 2010, Mahona anadaiwa kujaza anwani ya posta anayotumia kuwa ni Sanduku la Posta 453, Bongomela Kigoma wakati fomu ya mwaka huu pia inaonyesha kuwa anwani yake ni 453, lakini mahali pakiwa ni Simbo, Tabora.
Mgombea huyo ambaye katika uchaguzi wa mwaka jana alipata kura 11,000 pia alijaza fomu B ya tamko la mgombea akithibitsha kwamba maelezo aliyatoa ni ya kweli kwa kadri ya ufahamu wake.
Fomu B inasomeka: “Mimi Leopord Lucas Mahona, aliyedhaminiwa kuwa mgombea wa Jimbo la Igunga, nathibitisha kwamba nipo tayari na ninazo sifa za kugombea ubunge na kwamba maelezo niliyoyatoa kwa kadri ya ufahamu wangu ni ya kweli.”
Mahona alisaini fomu za mwaka huu kugombea nafasi hiyo Septemba 5 na zile za mwaka jana alisaini Agosti 9. Fomu zote zilithibitishwa na Katibu wa CUF Wilaya ya Igunga, Marco Maganga Katamija na kugongwa muhuri wa chama hicho Agosti 11 kwa ile ya mwaka jana na Septamba 5, kwa fomu ya mwaka huu.
Katika fomu hizo, Mahona amejaza fomu ya tamko la kisheria ambalo pamoja na mambo mengine, linathibitisha uraia wake, umri unaomruhusu kugombea ubunge, uwezo wa lugha, uanachama wa chama cha siasa na kwamba hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai.
Fomu ya mwaka huu ilisainiwa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Igunga, Sarah Nyamonge Septemba 5, wakati ile ya mwaka jana ilithibitishwa na Hakimu huyo Agosti 13 na zote zikigongwa muhuri wa Mahakama.
Fomu zote pia zimethibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Igunga. Fomu ya mwaka huu ilisainiwa na Protase Magayane aliyesaini fomu ya mwaka huu, Septemba 6 na alipokea ada ya Sh50,000 na kumpatia mgombea huyo risiti namba 0062770.
Katika uchaguzi wa mwaka jana, fomu hiyo ilisainiwa na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi, Richard Daudi Kalele, Agosti 19 na kumpatia Mahona risiti yenye namba 0060157 baada ya kuwa amepokea ada ya Sh50,000.
Mahona achachamaa
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo jana, Mahona alisema anachojua ni kwamba yeye mzaliwa wa Igunga katika eneo la Simbo na hayo mambo mengine: “Ni siasa tu.”
Akizungumza kwa hasira Mahona alisisitiza: “Mimi ni mzaliwa wa Simbo, Igunga sawa? Na nyie waandishi mfanye kazi yenu vizuri.”
Alikwenda mbali na kulituhumu gazeti hili akidai kuwa limekuwa likiandika taarifa zake visivyo na kumtaka mwandishi wa habari hii akome kumfuatafuata.
“Mwananchi (gazeti) mmekuwa mkiniandika vibaya na kama habari hii nitaiona kesho (leo), bwana ..., itakuwa ndiyo mwisho wako wa kuandika kwenye magazeti.”
Muda mfupi baada ya mazungumzo hayo, Mahona alituma ujumbe wa simu kwa mwandishi akisema: “Sijui nini unatafuta kwangu, wala sijui lini ulianza kufanya kazi Uhamiaji . Sijui kunijua huku mno kunatoka wapi? Sijui lini tumeanza tabia ya kutoa form (fomu) za wagombea kwa kina ...(jina la mwandishi), tafadhali kuwa makini na ukome kufuatilia mtoto wa mwenzako, usiyemjua.”
Maelezo ya CUF
Msemaji wa CUF, Mbarara Maharagande alisema alishapokea taarifa kuhusu suala hilo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Julius Mtatiro lakini akasisitiza kwamba kadri wanavyofahamu Mahona alizaliwa mkoani Tabora.
"Mgombea wetu (Mahona), alizaliwa hapahapa Igunga katika Kijiji cha Simbo na Kata hiyohiyo ya Simbo, huo ndiyo ukweli na hata ndugu zake, dada zake wote wamezaliwa hapa.”
Hata hivyo, Maharagande alisema CUF hawana kumbukumbu za taarifa alizotoa mgombea wao mwaka jana na kwamba hata walipozungumza naye alisema kwamba hakumbuki iwapo aliandika kwamba yeye ni mzaliwa wa Kigoma.
Msimamizi wa Uchaguzi
Akizungumzia suala hilo, Magayane alisema: “Siamini kama mtu anaweza kuwa na vyeti viwili vya kuzaliwa, hilo kweli siliamini, pengine inaweza kuwa miujiza.”
Hata hivyo, Magayane ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, alisema asingeweza kutafuta fomu ya mgombea ya mwaka jana na kuilinganisha na ile ya mwaka huu kwa sababu ya kutingwa na shughuli nyingi za uchaguzi.
Alisema ikiwa tuhuma hizo ni za kweli, mgombea huyo angeweza kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho kama angewekewa pingamizi na wagombea wenzake wakati wa hatua hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment