Tuesday, October 4, 2011

Igunga kwachafuka


CCM WATUMIA MAPANGA KUWATIMUA WAFUASI CHADEMA, MABOMU YA MACHOZI YATUMIKA

Waandishi Wetu, Igunga
MJI wa Igunga jana uligeuka uwanja wa mapambano kati ya wafuasi wa Chadema na Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambao walilazimika kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya.Milio ya mabomu yaliyofyatuliwa nje ya ofisi za msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na ving’ora vya polisi vilitikisa mji huo kiasi cha kuzifanya kutanda moshi mweupe.
Vijana hao wa Chadema, wanawake kwa wanaume, walijibu mashambulizi hayo ya polisi kwa kuwarushia mawe na fimbo huku wakiwasha moto uliounguza sehemu kubwa ya nyasi nje ya ofisi hizo.

Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wakisubiri kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika juzi lakini walikosa uvumilivu kadri muda ulivyokuwa ukienda ndipo walipoanza kupiga kelele za kutaka matokeo hayo kutagazwa, hali iliyowalazimisha polisi kutoa amri iliyowataka kuondoka katika eneo hilo, amri ambayo waliikaidi hivyo kurushiwa maji ya kuwasha na baadaye mabomu ya machozi.

Kutokana na vurugu hizo, baadhi ya maduka, migahawa na shughuli nyingine za uzalishaji mali, vilisimama huku wengi wa wakazi wakijifungia majumbani kukwepa kukamatwa na polisi.

Kadhalika, vurumai hizo zilishuhudia kundi la wafuasi wa Chadema lililokuwa likipita kwenye mitaa ya Mji wa Igunga likitawanywa na walinzi wa CCM maarufu kwa jina la Green Guard kwa kutumia mapanga, mishale na mawe katika tukio lililotokea majira ya saa mbili asubuhi.

Polisi walifika katika eneo la makazi ya muda ya CCM yaliyo katika Hoteli ya Peak na kuizingira kwa takriban saa mbili hivi, huku askari wengine wakiingia ndani kufanya upekuzi wa silaha zilizokuwa zikitumiwa na walinzi hao. Baadhi ya vijana hao walikamatwa na kupelekwa polisi.

Ilikuwaje?
Baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba CCM kilikuwa kimepata ushindi, gari la matangazo la chama hicho lilianza kupita mitaani likipiga muziki wa hamasa kwa wanachama na wafuasi wake.

Kitendo hicho kiliwaamsha Chadema ambao nao waliingiza gari lao la matangazo barabarani, huku wakitoa matangazo kwamba matokeo yalikuwa hayajatangazwa rasmi na kwamba CCM kilikuwa kikiwahadaa wananchi kwa kufanya vitendo vinavyoashiria kwamba ni washindi.

Gari hilo la Chadema likisindikizwa na wafuasi wake waliokuwa wakipeperusha bendera za chama hicho, lilifika usawa wa Hoteli ya Peak, Barabara ya Mwanzugi ilipokuwa kambi ya CCM na kuibua hasira za Green Guard waliamua kuwashambulia.

Katika vurugu hizo, vijana hao wa Chadema walitawanyika kila mmoja na njia yake na baadhi waliokamatwa na Green Guard walipigwa kwa bapa za mapanga.

Kutokana na hali hiyo, shughuli katika Barabara ya Mwanzugi zilisimama kwa muda huku watu waliokuwa karibu na eneo hilo wakitaharuki na kufunga biashara zao. Gari moja la CCM, Land Cruiser Hardtop lililokuwa limeegeshwa nje ya hoteli hiyo lilivujwa vioo.

Takriban dakika 15 tangu kuanza kwa vurugu hizo, polisi waliwasili na kuanza kutuliza ghasia hizo japokuwa walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa makada wa CCM, waliokuwa wakitetea hatua ya vijana wao kutumia silaha za jadi kwa maelezo kwamba walikuwa wakijihami baada ya kuchokozwa na Chadema.
Mmoja wa polisi hao alinusurika kupigwa kwa mawe yaliyorushwa kutoka ndani ya uzio unaozunguka hoteli hiyo ambako ndiko walikokuwa wamefikia viongozi wa CCM wakiwamo Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Wilson Mukama, Mawaziri Dk John Magufuli na Steven Wassira pamoja na makada wengine.

Dakika kama 45 baadaye, idadi ya polisi iliongezwa na kuizingira hoteli hiyo huku wengine wakiingia ndani kufanya upekuzi.

Mratibu wa Polisi katika Uchaguzi wa Igunga, Naibu Kamishna, Isaya Mngulu alisema wangetoa taarifa rasmi kuhusu matukio hayo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Dalili za kuzuka kwa vurugu zilianza jana saa 12:00 asubuhi baada ya wafuasi wa Chadema kuanza kujikusanya nje ya Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi na kadri muda ulivyozidi kusonga mbele, idadi yao iliongezeka.

Ilipotimu saa 12:50 asubuhi, vijana hao walianza kuimba nyimbo mbalimbali na kisha kufunga barabara kwa mawe kuzuia magari yasipite na kupandisha bendera ya Chadema.

Huku wakionekana kuwa na jazba, vijana hao walikuwa wakiimba kwa kupokezana wakisema: “”Wakijivua gamba tunaua nyoka, hesabu gani zinawashinda... kama mabomu tumeyazoea.”

Baada ya kuona hivyo, Mkuu wa FFU nchini, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Telesfory Anaclet aliwafuata na kuwasihi watulie na wasubiri kutangazwa kwa matokeo hayo.

Vijana hao walitulia na ilipotimu saa 2:10, gari la matangazo la Chadema lilipita mitaani likiwahamasisha wafuasi wa Chadema kwenda Ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi likidai kuwa kuna mipango ya kuchakachua kura.

Matangazo hayo yalionekana kama kuchochea moto kwa petroli kwani muda mfupi tu baadaye, makundi ya vijana yakitokea kila kona yalianza kumiminika katika ofisi hizo.

Ilipotimu saa 2:20, vijana hao wa Chadema tayari walikuwa wamefurika eneo lote la barabara inayoelekea katika ofisi hizo hadi lango kuu ndipo gari la polisi lenye maji ya kuwasha lilipowasili.

Kadri muda ulivyosonga mbele ndivyo hali ilivyozidi kuwa tete katika eneo hilo ndipo SACP Anaclet alipoagiza kuongezwa kwa FFU ambao waliwasili muda mfupi baadaye.

Mfuasi wa Chadema, Husna Amir alimweleza SACP Anaclet kuwa kitendo cha kutotangaza matokeo wakati viongozi wao wamewaarifu kuwa wameshinda, kinaashiria kuwa CCM kinataka kuchakachua matokeo hayo.

Hata hivyo, uvumilivu uliwashinda wafuasi hao kwani ilipotimu saa 3:50 walibadilika na kuanza kuimba: “Tunawapa dakika 10 vinginevyo tunakuja...” na baada ya muda wakasema: “Zimebaki dakika tano kuingia na geti.”

Ilionekana kama utani vile, lakini ni muda huo ulipotimu, vijana hao walianza kukata matawi ya miti na kuanza kuokota mawe huku wakihamasishana kuanza kusonga mbele kuelekea lilipokuwa gari lenye maji ya kuwasha.

Polisi wa FFU wakiwa wamebeba bendera nyekundu yenye maandishi yanayowaamuru kutawanyika walisogea mbele hatua chache huku ofisa mmoja akitoa matangazo kwa kipaza sauti akiwataka kutawanyika.

Wafuasi hao walikaidi amri hiyo na kuanza kurusha mawe kuelekea alipokuwa SACP Anaclet na polisi wengine na ndipo ilipotolewa amri ya wafuasi hao kumwagiwa maji ya kuwasha na mabomu ya machozi.

Milio ya mabomu hayo iliendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Igunga hususan karibu na Stendi Kuu na barabara ya kuelekea katikati ya mji kutokana na vijana hao kujikusanya upya kutaka kupambana na polisi.

Nje ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, polisi walikusanya baiskeli zaidi ya 10, viatu, kandambili, kanga na vitenge ambavyo viliachwa na wafuasi wanaoaminika kuwa ni wa Chadema waliotimua mbio baada ya kutawanywa.

SACP Telesfory aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kilichowasukuma polisi kutumia nguvu ni kitendo cha wafuasi hao kuanza kuwashambulia polisi.

“Tulikuwa hatuna jinsi zaidi ya kutumia nguvu na nyinyi waandishi ni mashahidi mmeona tulivyoshambuliwa hapa na hata nyinyi mlikimbia kuokoa maisha yenu lakini sasa hali ni shwari,” alisema.

No comments:

Post a Comment