Saturday, October 15, 2011

Vigogo wa Richmond wamhujumu Kikwete


Mwandishi Wetu

Toleo na 207
  • UVCCM Arusha yatumika kuasi
HUKU mambo yakiwa si shwari ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, wiki hii Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, ametoboa siri kwamba tangu Rais Jakaya Kikwete akubali kuvunjwa Baraza la Mawaziri mwaka 2008 kutokana na kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, amekuwa akihujumiwa.

Akizungumza katika mahojiano mahsusi na Raia Mwema mwishoni mwa wiki iliyopita, Membe alisema Rais Kikwete amekuwa akipigwa vita ya wazi wazi na ya chini kwa chini na watu aliowaamini na ambao wamepata kuwa marafiki zake.
Membe, hata hivyo amesema kwamba hujuma hizo hazijafanikiwa kumfanya Rais Kikwete apoteze malengo yake ya kiuongozi.

Katika mahojiano hayo maalumu na Raia Mwema, yatakayochapishwa katika gazeti hili siku zijazo, Membe amezungumzia pia masuala mbalimbali, ikiwamo namna nchi za Afrika zilivyosambaratika kimsimamo juu ya kulitambua Baraza la Mpito laTaifa la Libya (NTC).
Kati ya maswali aliyoulizwa ni pamoja na Rais Kikwete ambaye anatajwa kuwa rafiki wake wa karibu, kuwa na kile kinachotajwa ni huruma ambayo inamfanya kushindwa kufanya uamuzi mgumu kwa haraka ili kukidhi matakwa ya wakati.

Akijibu Membe alisema: “Unajua ili uweze kujibu swali hili lazima uangalie matukio ya mwaka 2008. Mwaka 2008, Rais alivunja Baraza la Mawaziri, hadi Waziri Mkuu akaondolewa. Hakuna huruma hapo. Ameondoa mawaziri na Waziri Mkuu.
“Na baada ya hapo akaanza kupigwa vita kutokana na hatua hiyo ya kishujaa. Alipigwa vita ya wazi wazi na vita ya ndani na watu aliowaamini na marafiki zake. Hili ni vema Watanzania wakalijua, halafu jiweke wewe kwenye nafasi yake.

“Ni kiongozi ambaye hajapoteza focus ( malengo) yake ya kuongoza nchi lakini huku akiongoza nchi ana kazi kubwa ya kuhimili vishindo, mapigo kwenye vyombo vya habari, kwenye simu, kutoka midomoni na kwa watu ambao wakati mwingine usingetarajia wafanye hivyo,” alisema Membe.
Lakini katika mahojiano hayo Membe amelieleza Raia Mwema ya kuwa juhudi za kumpiga vita Kikwete hazitawafikisha popote wahusika kwa kuwa nchi haiendeshwi kwa kutegemea msaada wa marafiki bali vyombo vya dola.

Membe ambaye pia amekuwa akitajwa kuwa rafiki wa karibu wa Rais Kikwete alisema; “Rais haendeshi nchi kwa kutegemea urafiki; kuna ushauri wa vyombo rasmi vya dola.
“Rais anao Usalama wa Taifa, Takukuru (Taasisi ya kuzuia na Kupabana na Rushwa), Jeshi la Polisi, Baraza la Mawaziri; anaweza kupata ushauri kutoka Kamati Kuu ya CCM na taasisi nyingine. Hategemei ushauri wa marafiki...hakuna.”
Uhasama ndani ya CCM ulijitokeza na kupata nguvu zaidi mara baada ya kashfa ya Richmond, iliyochunguzwa na Bunge, kupitia Kamati Teule iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrisson Mwakyembe, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi, akisaidiwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Kamati hiyo ilitoa mapendekezo kadhaa ikiwamo kuwawajibisha waliokuwa mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, ambao ni Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha. Mawaziri hao waliongoza wizara hiyo wakati wa mchakato wa zabuni ya kufua umeme iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond.
Pamoja na kupendekeza Karamagi na Dk. Msabaha wawajibishwe, ripoti hiyo ilimtaka Waziri Mkuu (wakati huo) Edward Lowassa, kupima uzito wa kashfa hiyo na kuchukua hatua kwa jinsi alivyopima na akaishia katika kujiuzulu.

Mwingine aliyetajwa katika ripoti hiyo ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga Rostam Aziz ambaye taarifa za awali zilionyesha kuwa alihusika katika kuiingiza nchini Richmond ambayo baadaye ilirithiwa na Dowans, ambayo nayo miezi kadhaa iliyopita, iliuza mitambo yake ya kufua umeme kwa kampuni ya Symbion ya Marekani.

Baada ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa, yaliibuka makundi mawili makubwa bungeni, moja likijitambulisha na aliyekuwa Spika Samuel Sitta na jingine likiegemea kwa waziri mkuu aliyekuwa anejiuzulu Lowassa na Rostam, ambao kwa miaka mingi walikuwa ni watu wa karibu sana na Jakaya Kikwete.

Huku mvutano wa makundi hayo mawili ukiwa wazi bungeni, na mara kadhaa ukitishia utendaji serikalini, ulimsukuma Rais Kikwete, kama Mwenyekiti wa CCM, kuunda Kamati Maalumu kutibu kile kilichotajwa kuwa ni mpasuko miongoni mwa wabunge wa CCM. Kamati hiyo iliongozwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na spika mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki, Kanali (mstaafu) Abdulrahman Kinana.

Kamati hiyo ilishuhudia mashambulizi ya wazi miongoni mwa kambi hizo ilipokutana na wabunge wa CCM mjini Dodoma na kwa hakika bado makundi hayo hayajapatanishwa ipasavyo.

Wakati huo huo, hali ya kisiasa ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) ni tete ikibainika kuwa Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Benno Malisa, ameanza kucheza hadharani siasa uasi zinazoendeshwa na kambi inayotajwa kuwa ni ya kigogo mmoja wa CCM mkoani humo.
Malisa sasa anahusishwa na tukio la hivi karibuni linalohusisha na ufunguzi wa mashina ya chama hicho Arusha mjini, unaotajwa kuratibiwa kinyemela bila viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa kutoa kufahamishwa na kwamba, sehemu ya waratibu wa tukio hilo ni vijana waliosafirishwa kutoka wilayani Monduli.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa tukio hilo halikushirikisha viongozi wa UVCCM mjini Arusha na viongozi wengine wa chama hicho.
“Mipango yote kwa kiasi kikubwa imeratibiwa na watu wa kutoka wilayani Monduli. Inasemekana kuwa hii ni sehemu ya mkakati wa maandalizi ya watu hao kumhami Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa endapo atabanwa kwenye mkakati wa kujivua gamba wa CCM, basi wajifanye kushusha bendera za CCM kwenye mashina hayo ili kuuonyesha umma kuwa anakubalika sana ndani ya chama,” anasema mmoja wa watoa taarifa wetu ambao ni vijana waliohusika kuratibu mpango huo.

Hali kama hiyo ya kujiandaa kwa ajili ya mchakato wa kujivua gamba ilijitokeza wakati aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz pale alipotangaza kujiuzulu baadhi ya vijana waliandaa mabango yenye ujumbe unaomtaka ajisiuluzu na wengine wakihoji hatua hiyo huku taarifa zikisema mabango hayo yaliandaliwa muda gani wakati alikuwa bado kutangaza kujiuzulu.

Kiongozi mmoja wa UVCCM Arusha anaeleza; “UVCCM Arusha mjini walikataa utekelezaji wa mkakati huo haramu kupitia kikao chake cha Kamati ya Utekelezaji kilichoketi Oktoba 7, mwaka huu, kwa kumwandikia barua Katibu wa Vijana CCM mkoani Arusha.”

Inaelezwa kuwa barua hiyo ilimjulisha kiongozi huyo kuwa wao kama wilaya hawajapata taarifa rasmi za uzinduzi wa mashina hayo ya wakereketwa na hivyo kwa muda uliobaki wasingeweza kufanya maandalizi mazuri ikizingatiwa wao ndio wenye jukumu la kuandaa mashina hayo na si Wilaya ya Monduli.
“CCM Mkoa baada ya kupata nakala ya barua hiyo waliamua kuitisha kikao cha sekretariati ya mkoa pamoja na kamati ya utekelezaji ya vijana Mkoa wa Arusha na Wilaya Arusha mjini, Oktoba 8, 2011.
“Katika kikao hicho maazimio yalikuwa ni kusitisha zoezi hilo hadi hapo taratibu za chama zitakapofuatwa. Chama Mkoa walimwandikia barua hiyo Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha ili aweze kuwataarifu na viongozi wengine pamoja na wanachama wa umoja wa vijana wa CCM.
“Baada ya kupata barua hiyo Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya, alifanya kikao cha faragha na Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige na Benno Malisa. Baada ya kikao chao hicho, waliamua kufanya shughuli hiyo iendelee kama walivyokusudia pamoja na chama kukataza.
“Jumatatu, Oktoba 10, 2011 walianza kushughulikia kibali cha maandamo na uzinduaji mashina hayo. Hadi saa nne asubuhi polisi waliwanyima kibali cha kazi hiyo,” alisema mtoa habari wetu mwingine ambaye naye amekataa kutajwa jina lake gazetini.

Inaelezwa kuwa mkutano huo wa kufungua mashina uliofanyika 10/10/2011, ulihudhuriwa na vijana kutoka Monduli na vijana wengine wa vyama mbalimbali vya siasa.
Katika shughuli hiyo, Benno Malisa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alishambulia wazi wazi chama chake akitetea Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema) chini ya mwavuli wa demokrasia na utawala bora.

Katika hotuba yake hiyo, Benno Malisa amekejeli hata kauli ya viongozi wenzake wa CCM wanaoonyesha kwamba CCM ni chama tawala na kuonya dola kuingilia mambo ya siasa, hali inayozidi kuashiria mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho tawala.

No comments:

Post a Comment