Friday, October 28, 2011

Zitto Kabwe akutwa na vijidudu 150 vya malaria


















KUPELEKWA INDIA KWA UCHUNGUZI ZAIDI, MBUNGE MWINGINE NAYE ALAZWA
Ramadhan Semtawa

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amebainika kuwa na vijidudu 150 vya malaria ambavyo vimemfanya alazwe Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Wakati Zitto akilazwa ICU ndogo (Min ICU), mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Claradiana Mwatuka, naye amelazwa katika kitengo hicho akisumbuliwa na vidonda vya tumbo.Jana uchunguzi kuhusu Zitto ulibaini kuwa anasumbuliwa na malaria kutokana na kuwa na wadudu hao ambao ni wengi kwa mtu kuweza kuwahimili.Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jana wodini hapo kuhusu hali yake, Zitto alisema kwa kifupi tu, "naendelea vizuri, najisikia vizuri".
Awali, taarifa kutoka hospitalini hapo zilisema Katibu Mkuu Wizara ya Afya alipiga marufuku Zitto kusumbuliwa na kuagiza wote ambao walikuwa wakienda wasimsemeshe kwa muda mrefu wa dakika 20.

Kwa upande wake, Msemaji wa hospitali ya Muhimbili, Jezza Waziri, alisema Zitto baada ya kufanyiwa vipimo tangu alipofika hospitalini hapo amebainika kuwa na vijidudu hivyo 150.Hata hivyo, alisema uchunguzi zaidi kuhusu afya ya Zitto unaendelea na kuongeza kwamba majibu ya vipimo zaidi yataonyesha kama kuna matatizo mengine au la.

Alifafanua kuwa hadi sasa madaktari wamebaini tatizo kubwa linalomsumbua mbunge huyo ni malaria na kuongeza kwamba jitihada na taratibu zaidi za matibabu zimekuwa zikiendelea.

Kumpeleka India
Spika wa Bunge, Anne Makinda jana jioni aliwaambia waandishi wa habari hapo Muhimbili kwamba Zitto alikuwa akiendelea vizuri, lakini tatizo la kichwa kuuma lilikuwa bado linamsumbua.Makinda ambaye alienda kumjulia hali Zitto, alisema kutokana na tatizo hilo kuendelea, Ofisi ya Bunge inafanya taratibu ili apelekwe India kwa uchunguzi zaidi.

Makinda aliwataka Watanzania waendelee kumuombea ili aweze kupona.Taarifa za watu wa karibu na Zitto zinasema kwamba huenda akasafirishwa kwenda India kesho kwa ajili ya uchunguzi huo alioutangaza Spika Makinda.

 Mbunge Mwatuka
Kuhusu hali ya mbunge Mwatuka, Waziri alisema alifikishwa hospitalini hapo juzi saa 4:00 usiku akisumbuliwa na matatizo ya vidonda vya tumbo na kwamba hadi jana alikuwa akiendelea na matibabu.Alifafanua kwamba, mbunge huyo baada ya kufikishwa hospitalini hapo alianza kupatiwa matibabu ambayo alisema yanaendelea vizuri.

Kaka wa Zitto  
Kwa upande wa kaka wa Zitto, Salumu Mohamed alifafanua kwamba kipindi chote ambacho ndugu yake alikuwa Aga Khan haikuweza kubainika mara moja iwapo ana wadudu 150 wa malaria.Hata hivyo, alisema baada ya kufika ICU Muhimbili moja kwa moja alifanyiwa vipimo vya awali ambavyo vilivyoonyesha kwamba alikuwa na kiasi hicho cha vijidudu.

"Baada ya kufika hapa juzi alipelekwa moja kwa moja ICU na kuchukuliwa vipimo. Matokeo ya awali, yanaonyesha ana malaria 150, hawa ni wadudu wengi sana," alifafanua Kabwe.Alisema bado uchunguzi zaidi kuhusu afya ya mdogo wake unaendelea kwani bado anasumbuliwa na tatizo la kuumwa na kichwa.
Salum alisema kama kutakuwa na umuhimu wa tatizo hilo kwenda kutibiwa nje itafahamika na itafanyika hivyo.

Wodini alikolazwa
Isipokuwa watu maalumu tu, watu wengine hawakuwa wakiruhusiwa kuingia alikolazwa mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwani hata waandishi wa habari waliofika hosipitalini hapo walizuiwa kuingia wodini hapo.

Kulikuwa na utaratibu maalamu kwani hata kwa wale walioruhusiwa walikuwa wakihojiwa kwanza, kwamba unatoka wapi na unamfahamu vipi mbunge huyo ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Wabunge mbalimbali wakiwamo Dk Hamis Kigangwallah wa Nzega na Dk Maua Daftari wakiwa na wafanyakazi wengine wa Ofisi ya Bunge, walikuwa miongoni mwa waliofika wodini hapo jana.

No comments:

Post a Comment