Wednesday, October 26, 2011
Sitta:Sigombei urais uchaguzi 2015
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema hana ndoto ya kuwania urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.Kauli hiyo ya kwanza ya Sitta ambaye pia ni kada wa CCM, imekuja wakati ambao kuna mpasuko mkubwa ndani ya chama chake hicho ambao unahusishwa na mbio za urais wa 2015, huku yeye akitajwa kuwa mmoja wa wenye nia ya kushiriki mbio hizo.
Kauli yake imeingia katika orodha ya kauli za makada wengine kadhaa ambazo zimetikisa siasa za CCM huku nyingi zikiwa na sura ya mvutano tena zikitolea nje ya vikao rasmi vya chama hicho tawala nchini.
Hata hivyo, juzi usiku akijibu swali kama ana ndoto ya kuwania urais au la, Sitta alisema: "Hapana! Sina ndoto ya kuwania urais kwa sasa, wapo vijana watajitokeza, wapo wazuri, tutawaunga mkono tu".
Sitta alifafanua kwamba matumaini yake mwaka 2015 watakuwapo wagombea wenye uwezo wakiwemo vijana, na kuongeza, "wale wazalendo wenye maadili wataungwa mkono".
Ingawa, Sitta amesema hana ndoto ya kuwania urais kwa sasa, lakini amekuwa akitajwa kama mmoja wa watu wanaoutaka baada ya Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015, kutokana na nguvu zake kubwa alizojijengea kwa umma.
Sitta aliweza kujipatia umaarufu mkubwa kisiasa baada ya kuongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa ambalo alikuwa na kauli mbiu yake ya Bunge la Kasi na Viwango.
Kuhusu chuki ya watu aliowaita mafisadi, Sitta alisema watuhumiwa hao walifanya mbinu mbalimbali kuhakikisha hafanikiwa katika malengo ya kurejea kwenye uspika wa Bunge la Kumi kwani waliendesha hujumu nzito dhidi yake.
Sitta aliwatuhumu watu hao akisema: "Mafisadi hawanitaki, wananichukia wako tayari hata kuniua".
Mwelekeo wa CCM
Akizungumzia mustakabali wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, Sitta alisema CCM kitaweza kushinda kutokana na mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa katika vikao vijavyo vya chama hicho baadaye mwaka huu, pamoja na uchaguzi wake mkuu wa mwakani.
Sitta aliongeza:, "Uchaguzi Mkuu ndani ya CCM wa mwaka 2012, utatuonyesha sura ya chama. Nina imani watapatikana wanaofuata maadili yale aliyosimamia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere".
Hata hivyo, Sitta alionya kwamba chama hicho kinahitaji timu ya ushindi na kwamba hakiwezi kufanya hivyo ikiwa kitaendelea kuwa na watu wanaojitajirisha kwa nafasi zao za uongozi.
"CCM inastahili kufanya mabadiliko, inahitaji timu ya ushindi ili kuweza kufanya hivyo, lakini hakiwezi kufanya hivyo kama itaendelea kuwa na watu wanaojitajirisha kupitia fursa za uongozi. 2012 CCM iwe safi zaidi, tusiache watu wanunuane," alionya Sitta.
Alisema mwaka 2012, CCM itashuhudiwa ikirejea katika mstari wake, kupitia vikao vyake na falsafa ya kujivua gamba ambayo itashuhudiwa ikiwashughulikia wanaopinga kurejesha maadili na kuzaliwa upya.
Lakini, alisema katika hilo wapo wanaopinga kurejeshwa kwa maadili hayo kwa kutumia fedha zao kununua wapambe aliowaita wenye roho za kuku ambao watakuwa wakitumika kuzuia mpango huo kwa malengo ya kisiasa.
"Katika hilo wapo wenye roho ya kuku, wakionyeshwa pesa tu, basi wanabadilika. Wanaosema hawataki dhana ya kujivua gamba hawataki CCM izaliwe upya,"alisema.
Malipo ya Dowans
Sitta alirerejea msimamo wake kuhusu malipo kwa kampuni hiyo, huku akisema kuwa anaridhishwa na hatua ya kukata rufaa na kusisitiza umuhimu wa vijana kuwa na uzalendo wa kufanya maandamano kupinga mambo yasiyo ya msingi.
"Sisi zamani tulikuwa mstari wa mbele katika maslahi ya taifa. Ila kwa sasa naona vijana wako nyuma sana hawaandamani kupinga vitendo vya kifisadi katika Serikali yao, maandamano ya kizalendo yenye kuonesha hisia zao juu kupinga ufisadi huu,’’alisema Sitta.
Alisema angefurahi siku kuona kama vijana wa CCM na wengine wenye maadili wakiandamana kwa pamoja kupinga vitendo vya kifisadi, ikiwemlo kuilipa Dowans, lakini kwa sasa akasema suala hilo linashughulikiwa kisheria.
Sitta ambaye alikuwa akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha luninga cha ITV, alisema Sh 110 bilioni za kuilipa Dowans zina uwezo wa kujenga shule za kisasa 300 mbazo kila moja ingegarimu Sh300 milioni.
Sitta alisema huo ni ulafi na kuongeza kwamba yeye kama angekuwa na fedha nyingi au sehemu angekuwa tayari mafisadi wangemchafua.
“Mimi kama ni ngekuwa hata na tuhuma ya shilingi moja ni lazima wangeniumbua maana wananitafuta sana na kama vitisho nimevipata sana kwenye simu ndiyo maana nabadilisha sana namba ya simu,’’ alisema.
Alisema stahiki anazolipwa na Serikali kama nyumba na magari si ufahari, kwani kama ni benzi aliyokuwa akitumia kipindi akiwa mbunge si lake.
Waziri Sitta alisema gari kama hilo alinunuliwa pia Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na hata Gavana wa Benki Kuu (BoT) na kuhoji, "sasa kwanini nitajwe mimi tu?"
Kauli za makada CCM
Wiki iliyopita Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa naye alivunja ukimya kwa kuzungumzia tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake, huku akisisitiza kuwa amechoka kukashifiwa na sasa kamwe hatawavumilia wanaomzulia mambo.
Lowassa ambaye pia amekuwa akitajwa kuwa na mpango wa kuwania urais wa 2015 alisema ni jambo lisiloingia akilini kumhusisha yeye na kile kinachodaiwa mkakati wa kumhujumu Rais Kikwete au CCM, wakati yeye ni mbunge anayetokana na chama hicho.
Siku moja kabla ya Lowassa kuzungumza na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya aliingia katika malumbano yanayoendelea miongoni mwa makada wa chama hicho pale aliposema “watoto wa viongozi wa CCM na Serikali wamejitwika madaraka ya wazazi wao kinyume cha sheria za nchi”.Kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa, pia Millya alimshambulia Katibu wa Itikadi na Uenenzi wa chama hicho, Nape Nnauye kwamba amekuwa akikivuruga chama.
Nape anatuhumiwa na kundi mojawapo ndani ya CCM kutokana na jinsi anavyosimamia utekelezaji wa maazimio ya NEC ya CCM hasa falsafa ya kujivua gamba, na hilo limekuwa likihusishwa na mbio za urais wa 2015.
Hata hivyo, Nape aliwahi kuliambai gazeti hili kwamba anashamgazwa na wale wanaopotosha utekelezaji wa maazimio hayo ya NEC kwa kuhusisha utekelezaji wake na Uchaguzi Mkuu ujao, wakati muda wa uchaguzi wenyewe bado haujafika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment