Saturday, October 22, 2011

Tanzania yashitushwa

SERIKALI imeshitushwa na jinsi kifo cha aliyekuwa Rais wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, kilivyofanyika na ina wasiwasi na hatima ya nchi hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania kwa Wizara yake ya Mambo ya Nje na Ushirikinao wa Kimataifa, Waziri Bernard Membe alisema:
“Kifo cha Gaddafi ni suala linalotuhusu na limetokea wakati tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru … Serikali ya Tanzania hatuna tabia wala utamaduni wa kusherehekea kifo hata kama ni adui amekufa, hivyo kifo cha Gaddafi kimetushtua sana.”

Alisema Tanzania haiwezi kufurahia kifo chicho na ina wasiwasi kwamba yawezekana kikawa chanzo wa machafuko na umwagaji damu Libya.

Membe alisema kuuawa kwa Gaddafi hakumaanishi kwamba ndiko kupatikana kwa amani ya kudumu Libya na huenda kukawa na machafuko zaidi yatakayosababisha vifo vya wananchi wengi.

“Tuna wasiwasi mkubwa, kwamba huenda kifo cha Gaddafi kikawa chanzo cha mapigano makali na machafuko na vifo vya watu wengi zaidi … lakini pia tunaamini Libya itajengwa na Walibya wenyewe.

“Tunaomba makundi yanayopigana yaunde Serikali ya Mpito, itakayotambuliwa na wote ili iandae uchaguzi wa kidemokrasia na kupata kiongozi kwa njia ya amani na utulivu”.

Alisema Februari Umoja wa Afrika (AU), uliruhusu Umoja wa Mataifa (OAU) kwenda Libya kuhakikisha amani inalindwa, lakini Aprili mwaka huu, AU ilishituka baada ya kuona nguvu kubwa imeelekezwa katika kubadilisha uongozi wa Libya.

Alisema kutokana na hilo jopo la nchi tano likiongozwa na Afrika Kusini ambapo ulifanyika mkutano na ajenda kubwa ikiwa ni kujadili namna Libya itakavyosaidiwa kuhakikisha pande
zote tatu zinakaa na kujadiliana.

Akizungumza mapema kupitia Radio Clouds, Membe alisema kuuawa Gaddafi ni kujichukulia sheria mkononi na kuwa huo utakuwa mwanzo wa kukosekana amani.

“Alikuwa Rais wa mstari wa mbele kuijenga Afrika, kusaidia viongozi wa Afrika na kuifanya Afrika kuwa na serikali moja. Nitashangazwa sana kama nchi yoyote ya Afrika itafurahia
kifo chake.

“Mauaji hayo si ushindi wa Baraza la Mpito la Libya (NTC) kwani ni mwanzo wa visasi kutokana na vifo vya watu zaidi ya 30,000 na hakuna kabila ambalo litawashinda wengine,”
alisema Membe.

Akijibu swali kama Ubalozi wa Libya nchini utapeperusha bendera nusu mlingoti, alisema: “Hatukusema kama Gaddafi akifa tutaruhusu bendera ipeperushwe, hatulazimishwi kuitambua nchi, tutaitambua nchi kama itafuata vigezo.

Tanzania ni nchi huru, hatulazimishwi na wala hatukurupuki tunaamua tunachotaka.”
Alisema ni vema NTC wakaunda serikali ya mpito itakayojumuisha makabila na wapinzani wote ili kuelekea kwenye demokrasia na kutekeleza mtihani uliopo wa kujenga na kulinda amani katika nchi yao.

Maziko yake
Serikali ya Libya inapanga kufanya maziko ya faragha ya Gaddafi, BBC imeelezwa kutoka Tripoli.

Hata hivyo, inaonekana kana kwamba kutakuwa na uchelewaji wa maziko hayo, ambayo chini ya taratibu za Kiislamu hutakiwa kufanyika mapema iwezekanavyo.

Waziri wa Mafuta, Ali Tarhouni, aliiambia Reuters jana, kwamba mwili wa Gaddafi unaweza “ukahifadhiwa kwa siku chache zijazo.” Nato jana ilitarajiwa kutangaza mwisho wa kampeni
zake nchini.

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, alisema kifo cha Gaddafi kinamaanisha kwamba uvamizi wa kijeshi wa Nato nchini hapa umefikia mwisho wake.

“Ni dhahiri kwamba operesheni hiyo imefikia mwisho,” aliwaambia waandishi wa habari. Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain Juppe, alisema operesheni ya Nato ingemalizika “ili kujiandaa kuchukua hatua kuhusu utawala wa mpito wiki moja ijayo.”

Kwa sasa Serikali iliyopo iko njiapanda ya nini cha kuufanyia mwili wa Gaddafi, ambao uko Misrata ambako Alhamisi ulipitishwa mitaani.

Kunaonekana kutofautiana juu ya nini kifanywe na mwili huo. Chini ya sheria za kiislamu, Gaddafi alipaswa kuzikwa ndani ya saa 24 baada ya kifo.

Uongozi wa muda unataka yafanyike maziko ya faragha, lakini hakuna uamuzi uliokwishafikiwa wa ni wapi azikwe – Misrata, Sirte au katika jangwa la Libya.

Ofisa mmoja wa utawala huo, aliiambia BBC, kwamba wapiganaji kutoka Misrata waliomkamata kiongozi huyo, hawako tayari kuuachia mwili huo kwa sasa.

Habari za BBC zinasema mamlaka husika hivi sasa zinatakiwa kuamua jinsi ya kushughulikia kifo hicho na hasa maziko yake.

Kaburi baharini Tayari mamlaka hiyo imeshasema inaandaa maziko ya faragha na kuna
uvumi kwamba huenda ikajaribu kumzika baharini, kama ilivyofanyika kwa kiongozi wa al Qaeda, Osama bin Laden, ili kuzuia kaburi kuonekana kama sehemu takatifu.

Hata hivyo, habari zaidi kutoka Misrata zilisema mwili wa Gaddafi hautatolewa mapema kwa ajili ya maziko hayo.

“Nimewaambia wauweke kwenye friji kwa siku chache … kuhakikisha kwamba kila mtu anajua kuwa amekufa,” Tarhouni alisema. Alipoulizwa kuhusu mipango ya mazishi, alisema:
“Hakujatolewa uamuzi bado.”

Reuters pia ilimkariri ofisa ambaye hakutajwa jina, akisema kuna kutofautiana ndani ya Baraza la Taifa la Utawala (NTC) juu ya nini kifanyike kwa mwili huo.

Maswali pia yanaibuliwa kuhusu nini kilifanyika katika saa za mwisho za maisha ya Gaddafi baada ya kukamatwa.

Maofisa wanakana kwamba aliuawa. Kuna mikanda miwili ya video, mmoja ukimwonesha akiwa hai na mwingine amekufa na kuna mingine minne au mitano yenye matukio tofauti ya nini kilifanyika kati ya video hizo mbili. Hii inazua shaka kubwa.

Mpiganaji wa NTC aliiambia BBC, kwamba alimkuta kiongozi huyo wa zamani amejificha ndani ya mtaro wa majitaka na alimwomba asimwue.

Mpiganaji huyo aliwaonesha waandishi wa habari bastola ya dhahabu akisema aliichukua kwa Gaddafi.

Mjumbe mwandamizi wa NTC, Mohammed Sayeh, aliiambia BBC, kwamba ana wasiwasi kwamba Gaddafi aliuawa kwa makusudi, lakini akaongeza: “Hata kama aliuawa kwa makusudi, nadhani alistahili.”

Aliongeza: “Kama walimwua hata mara 1,000, nadhani haitatosha kuwalipa Walibya alichowafanyia. Tumepoteza zaidi ya watu wetu 70,000 kutokana na ukatili wake.”

Haki za binadamu
Jana, Kamishna wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Navi Pillay, alisema kunapaswa kufanyika uchunguzi wa kina juu ya jinsi alivyouawa Gaddafi.

Msemaji wake, Rupert Colville, aliiambia BBC, kwamba kifo cha Gaddafi yawezekana kikawa haramu.

“Kuna video mbili pale, moja ikimwonesha akiwa hai na nyingine akiwa amekufa na zipo nyingine nne au tano zenye matukio tofauti ya kilichotokea kati ya video hizo mbili zilizopigwa
kwa simu ya mkononi.

Hiyo ni dhahiri inaibua shaka kubwa sana sana,” alisema. “Watu wanauawa vitani na hiyo
inatambulika waziwazi katika sheria ya kimataifa. Kwa upande mwingine, ni wazi pia chini ya sheria ya kimataifa kwamba mauaji ya kikatili, yasiyotokana na hukumu za mahakama, yote ni haramu.”

Taasisi ya Haki za Binadamu ya Uingereza ya Amnesty International imetoa mwito wa kufanyika kwa uchunguzi huria wa mazingira ya kifo cha Gaddafi.

Rais wa Venezuela, Hugo Chavez, ambaye ni mshirika na rafiki wa Gaddafi, amekiita kifo hicho kuwa cha kusikitisha. “Wamemwua,” Chavez aliwaambia waandishi wa habari jana.

Hata hivyo, habari zinasema Walibya wachache wana shaka juu ya jinsi kiongozi huyo wa zamani alivyokumbana na mauti kidhalili, ingawa wamefurahi kuwa ameondoka.

Marekani, Nato washangilia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, akizungumza akiwa Pakistani jijini Islamabad, alisema kifo cha Gaddafi kinaashiria mwanzo wa enzi mpya kwa watu wa Libya.

NTC inatarajiwa leo kutangaza rasmi ukombozi wa nchi kutoka Benghazi. Katibu Mkuu wa Nato, Anders Fogh Rasmussen, alisema kwa kifo cha Gaddafi, mwisho wa ushirika huo kujihusisha na masuala ya nchi hii “umeshakaribia sana.”

No comments:

Post a Comment