Tuesday, October 18, 2011

Kikosi maalumu kuchunguza mauaji ya Mchina

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inakusudia kuunda kikosi maalumu kwa ajili ya kuwasaka waliomuua mke wa Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kichina nchini, Han Bing (38).

Uamuzi huo umetangazwa jana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova wakati wa kuaga mwili wa Han karibu na Chuo cha Diplomasia Kurasini, sehemu yalipotokea mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Kova Polisi wamefikia hatua nzuri ya kuwanasa waliomuua mama huyo.

Han ambaye ni mke wa Zhu Jin Fenj, alivamiwa na kuuawa na majambazi kwa risasi Oktoba 11, mwaka huu ambapo pia walimpora Sh milioni 30 alizokuwa nazo kwenye gari.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliahidi kuwa vyombo vya sheria vitahakikisha vinawakamata na kuwachukulia hatua wahusika wa mauaji hayo.

Membe aliwahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ni nchi salama kwao na siyo tabia ya Watanzania katika kufanya mauaji kama hayo.

Alisisitiza kuwa mauaji hayo si ya kudhamiria kwa raia wa China au kwa wageni waliopo nchini, bali ni mauaji ya watu wenye tamaa ambao hufanya kwa yeyote ili kupata fedha bila kujali utaifa, rangi wala dini ya mtu.

Aliwashauri wafanyabiashara kuwa makini katika ubebaji wa kiasi kikubwa cha fedha kwa kutumia kampuni binafsi za ulinzi kama Suma JKT ili kulinda usalama wao na fedha zao.

“Ni vema kutumia kampuni hizo hususani katika kutuma na kupokea fedha kutoka benki, Serikali kwa upande wake iko tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha vitendo kama hivi havitokei na wahusika wanatiwa nguvuni,” alisema Membe.

Naye mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete alitoa pole kwa jamii hiyo na kuwataka vijana kufanya kazi halali kwa kuwa kazi hizo zinawaletea heshima na utu. Pia aliwashauri vijana walioajiriwa sehemu mbalimbali kuwa waaminifu kwa waajiri wao pamoja na kuheshimu kazi zao.

Alisema Han wakati wa uhai wake alikuwa mdau mkubwa katika maendeleo ya wanawake nchini kupitia WAMA na kutaka vyombo vya sheria kutowafumbia macho wauaji hao wanaorudisha nyuma maendeleo ya wanawake nchini.

Alisema jamii ya Wachina wamekuwa mstari wa mbele kusaidia Tanzania tangu kwa waasisi wa mataifa hayo hivyo kifo cha mwanamke huyu ni changamoto kwa nchi zinazoendelea. Alisema taasisi yake pamoja na wanawake wote wanathamini mchango wa maendeleo wa mwanamke huyo kwao.

Naye Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alishiriki maziko ya Han, katika eneo linalotumika kuchomea moto maiti za watu wenye imani hiyo, Kijitonyama.

Ngeleja alitoa pole kwa Balozi wa China nchini, Liu Xinsheng kwa niaba ya Wachina wote na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua.

Alisema anaamini Zhu na Han ni wajasiriamali waliokuwa na lengo la kusaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kutoa ajira kwa vijana katika kampuni yake iliyopo Dar es Salaam.

Alisema Wizara yake imekuwa ikipokea misaada mingi kutoka China katika kipindi cha miaka 50 kutoka nchi ipate Uhuru na kutumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya China kwa misaada wanayoitoa.

No comments:

Post a Comment