Monday, October 3, 2011

Matokeo moto Igunga

UPIGAJI kura katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Igunga jana ulimalizika kwa amani na matokeo ya awali wakati tukienda mitamboni yalionesha mchuano mkali kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ilipofika saa mbili usiku jana, CCM ilikuwa ikiongoza katika kata 9 kati ya 26 za Jimbo la Igunga ikiwa na kura 8,421 dhidi ya kura 6,197 za Chadema.

Kata hizo ni Ntobo, CCM 730, Chadema 302; Nguvu Moja CCM 694, Chadema 284; Nkinga ambako Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alifunga mkutano wa kampeni wa CCM Jumamosi, chama hicho kimepata kura 1,479 na Chadema ikipata kura 1,085.

Nyingine ni Itumba CCM 1,079, Chadema 590; Nanga, CCM 897, Chadema 645; Igulubi CCM 925, Chadema 592 wakati katika Kata ya Mwisi anakotoka Mbunge aliyejiuzulu Rostam Aziz, CCM imeanguka kwa kupata kura 926 dhidi ya 992 za Chadema.

Rostam alijiuzulu wadhifa wake huo alioushikilia kwa miaka 17, akidai amefanya hivyo kutokana na siasa uchwara ndani ya chama hicho tawala.

CCM imeanguka pia katika Kata ya Mbutu ambako imepata kura 1,186 dhidi ya 1,426 za Chadema wakati katika Kata ya Kinungu imeongoza CCM kwa kura 505 dhidi ya kura 263 za Chadema.

Aidha, hadi kufikia saa mbili usiku, katika vituo 53 vya Kata ya Igunga Mjini, tayari vituo 22 vilikuwa matokeo yake yako tayari na CCM ilikuwa ikiongoza kwa kura 1,388 dhidi ya kura 1,287 za Chadema. Jimbo zima lina vituo vya kupigia kura 427.

Kutokana na Chadema kuongoza katika baadhi ya vituo vya mjini, vijana na mashabiki wa chama hicho walikuwa wakishangilia na kuandamana kukisifu chama hicho.

Matokeo ya mjini yalionesha kuwa kwenye Kituo cha Shule ya Msingi Igunga, kituo kidogo cha kwanza Chadema ilipata kura 216, CCM
(201) na CUF (3).

Katika Kituo cha Chipukizi, kituo kidogo cha kwanza Chadema ilipata 98, CCM (87) na CUF (7). Kituo kidogo cha pili Chadema 108, CCM 71 na CUF 4.

Kituo cha Tarafani Chadema 88, CCM (61), CUF (6), kituo kidogo cha pili Chadema (73), CCM (71) na CUF (4). Kituo kidogo cha tatu, Chadema (90), CCM (83) na CUF (7).

Katika kituo cha Stoo ya Pamba, kituo kidogo cha kwanza Chadema (69), CCM (81), CUF (2), kituo kidogo cha pili, Chadema (91), CCM (70), CUF (2)., kituo kidogo cha tatu, Chadema (82), CCM (86), CUF (3).

Kituo kidogo cha nne katika kituo cha Stoo ya Pamba, Chadema (72), CCM (76), CUF (2), kituo kidogo cha tano Chadema (84), CCM (79) na CUF (1).

Katika kituo cha Chipukizi, Chadema (98), CCM (84), CUF (7) kituo kidogo cha pili katika kituo hicho, Chadema (106), CCM (71) na CUF (4).

Awali, shughuli ya upigaji kura katika uchaguzi huo wa kujaza nafasi ya Rostam aliyejiuzulu Julai mwaka huu, ilianza na kumalizika kwa utulivu ambapo wakazi wa jimbo hilo walijitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura huku kukijitokeza kasoro chache.

Baadhi ya kasoro hizo ni pamoja na mpigakura kubadilisha picha ya kitambulisho chake cha kupiga kura kwa madai kuwa haikumpendeza na kuweka iliyompendeza ya rangi.

Pia ipo dosari ya baadhi ya wasio na vitambulisho vya kupiga kura kuruhusiwa kupiga kura katika baadhi ya vituo, huku vingine wapigakura wenye kasoro hiyo wakizuiliwa. Pia kulijitokeza kukosekana kwa majina ya baadhi ya wapigakura katika orodha ya wapigakura.

Katika baadhi ya vituo ambavyo gazeti hili lilitembelea ikiwemo Shule ya Msingi Chipukizi Igunga Mjini, lilishuhudia wasiokuwa na vitambulisho wakishiriki kupiga kura kwa kujaza fomu namba 17 kama uthibitisho.

Hata hivyo, katika kituo cha Stoo ya Pamba nacho cha Igunga mjini, wananchi waliopoteza vitambulisho waliwagomea kupiga kura.

Hali hiyo imezua mtafaruku na kuwavuta viongozi wa vyama katika vituo hivyo huku wakitolea mfano vituo vingine vilivyowaruhusu wasiokuwa na vitambulisho
vya kupigia kura kupiga kura.

Kasimu Mussa Selemani alikuwa ni mmoja wa watu waliokumbana na adha ya kutokuwa na kitambulisho, lakini jina lake lipo katika orodha ya wapigakura
kwenye kituo cha Ujenzi na alikataliwa kupiga kura.

“Tumetangaziwa kuwa hata usipokuwa na kitambulisho unaweza kupiga kura na ndio maana nimekuja hapa tangu asubuhi na nimeshuhudia wenzangu wakiendelea
na uchaguzi, lakini mimi nimekataliwa,” alisema Selemani.

Alisema kitambulisho chake hakufika nacho katika kituo cha kupiga kura kwa kuwa kimechanika vipande vipande. Hata hivyo, aliruhusiwa kupiga kura mara baada ya kupeleka vipande vya kitambulisho cha kupigia kura.

Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Protace Magayane, alisema mtu yeyote ambaye hana kitambulisho haruhusiwi kupiga kura na hiyo ni kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi.

Alisema masharti ya mpigakura yalibandikwa katika vituo vyote na kuongeza kuwa fomu namba 17 si tamko kwa ajili ya mtu aliyekosa vitambulisho vya wapigakura.

Kuhusu changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi huo, alisema kutokana na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo jimboni humo hasa Kata ya Igurubi,
magari yalikwama na kusababisha vifaa kuchelewa kufika vituoni na kusababisha watumie baiskeli kuvibeba.

Kuhusu hali ya usalama katika uchaguzi magari ya Polisi yalionekana kila kona ya jimbo hilo huku yakiwa yamefungwa vitambaa vyekundu na mengine kuegeshwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ambako ndiko matokeo ya uchaguzi huo yatakapotangazwa.

Katika Kituo cha Shule ya Msingi Chipukizi, Mzee Rashid Sultan aliyekuwa na kitambulisho cha kupiga kura, alizuiwa baada ya jina lake kukosekana katika orodha ya wapigakura wa kituo hicho.

Hata hivyo, Sultan alipozungumza na gazeti hili alisema yeye tangu 2007 alihamia Nzega na hakuwahi kufanya mabadiliko ya kitambulisho chake hata huko Nzega.

Sultan alisema alikwenda kupiga kura kwa kuwa ameshiriki katika uhamasishaji wa kupiga kura na yeye kuhamasika lakini anahisi aliondolewa katika daftari
hilo labda kwa dhana kuwa alishakufa kumbe yuko hai.

Mzee Salum Mteka (86), alisifu utaratibu wa kuwapa kipaumbele wazee ili wasipange foleni kama vijana na kuongeza kuwa utaratibu huo umemsaidia kupata haki yake.

Hata hivyo baada ya kuzungumza na gazeti hili, alidhani kuwa ni kama wakati wa kupiga kura na kutaka mwandishi ampe sehemu ya kusaini baada ya kumhoji.

Katika Kituo cha Stoo ya Pamba nako, mmoja wa wapiga kura alizuiwa kupiga kura baada ya kubadilisha picha ya kitambulisho chake iliyokuwa haina rangi
na kuweka picha ya rangi inayomuonesha vizuri.

Mkuu wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Polisi Makao Makuu, Isaya Mngulu, alisema mpigakura huyo, Zakaria Reuben alizuiwa kupiga kura baada ya kuharibu kitambulisho chake cha mwaka 2009 kwa kuondoa picha inayodhaniwa haikumpendeza na kuweka aliyodhani imempendeza.

Mgombea wa CCM, Dk. Dalaly Kafumu alipiga kura yake katika Kituo cha Lugubu, Kata ya Itumba saa nne asubuhi huku mgombea wa Chadema, Mwalimu Joseph
Kashindye akipiga kura katika Shule ya Msingi Chipukizi Kata ya Igunga Mjini saa mbili asubuhi.

No comments:

Post a Comment