SAKATA la malipo ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Dowans limezidi kuchukua sura mpya, baada ya jana viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa shirika hilo kutoka katika matawi 12 ya Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, kutamka kuwa, hawako tayari kuilipa kampuni hiyo.
Wamekwenda mbali zaidi na kudai kuwa, wako tayari kuandamana kwa lengo la kushinikiza Dowans isilipwe kiasi cha Sh bilioni 94 ambacho kimesajiliwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa kikao cha dharura cha viongozi wa vyama vya wafanyakazi ambao walikuwa wakijadili malipo ya Dowans, kauli za ugawanyishwaji wa shirika na gharama za manunuzi ya mafuta ya Kampuni ya IPTL.
Akichokoza mada hizo, mjumbe wa Kamati ya Majadiliano, Hassan Athuman alisema haiwezekani kuilipa Dowans kutokana na kutokuwa na sababu ya kufanya hivyo, kutokuwa na fedha, na sio walioingia mkataba na kuvunja mkataba na hawako tayari kuilipa kampuni hewa.
Alisema: “Hatuna sababu za kulipa fedha hizo, hata tukisema tunailipa, fedha tutatoa wapi? Ili kulipa ni lazima Tanesco isimamishe uzalishaji si chini ya miezi mitatu. Na kama tutasema wafanyakazi walipe kutokana na mishahara basi tunatakiwa tufanye kazi kwa miezi 22 bila kulipwa chochote.
“Hivi inaingia akilini mtu kufanyakazi kwa kujitolea na kisha fedha tumlipe Dowans ambaye Rais (Jakaya Kikwete) na serikali walisema hawafahamu mmiliki wake, hivi hiyo hundi itaandikwa yeyote anayehusika”? Athuman alisema kwa muda mrefu Tanesco imekuwa ikihusishwa na ulipaji wa gharama ambazo haziwahusu na kutolewa mfano malipo ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL ambazo ni Sh bilioni 26 kwa mwezi.
“Kwa muda mrefu wameifanya Tanesco kama mti wa mzambarau ambao kila mwenye kapu anatikisa na kuondoka nazo na hapo wanasema hamzalishi. Sasa hali hii hatuikubali,” alisema. Tanesco ambayo mapato yake ni Sh bilioni 56.8 kwa mwezi, imekuwa ikinunua mafuta yanayotumika katika mitambo ya IPTL kiasi cha lita laki tano kwa siku. Aidha, Athuman aliishangaa Hazina kupitia kauli ya Waziri wa Fedha, na Uchumi, Mustafa Mkullo kujivua katika malipo hayo na kutupa mzigo kwa Tanesco.
“Mkullo (Mustafa) amejivua na kutupa mzigo Tanesco, sasa hapo anatukataa kama sisi si miongoni mwa mali za wizara yake, basi atuletee waraka ambao utaonesha kuwa ni mali ya wafanyakazi. Kamati iliyoingia mikataba ilitoka huko huko serikali,” Akichangia, Eric Mbilinyi alipendekeza kufanyika maandamano ya wafanyakazi wa shirika hilo nchi nzima ikiwa ni njia ya kushinikiza kutolipwa ma malipo hayo.
“Tuitishe maandamano haraka, ikibidi tulale barabarani na tuandae vipeperushi vitakavyoelezea bayana suala hili na kuvisambaza kwa wananchi,” alisema huku akishangiliwa na viongozi wengine na kuungwa mkono na Shukuru Nyuso kutoka Pwani aliyetaka maandamano hayo yafanyike Jumamosi ijayo.
Anacletus Magembe pamoja na kusisitiza kwa Tanesco kutolipa fedha hizo, alitaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kujiuzulu kutokana na kushindwa kutekeleza kile alichokiahidi mbele ya Bunge.
“Tanesco tunagharamia mambo mengi, kununua mafuta ya IPTL, Symbion, Aggreko, pamoja na Waziri kusema serikali itabeba gharama za umeme wa dharura, lakini bado Tanesco ndio wanaolipia gharama hizo badala ya serikali, sasa wakati umefika wa kukataa kubeba gharama hizo na ikibidi Waziri ajiuzulu kwani ameshindwa kuwajibika,” alisema.
Hilda Njovu kutoka Tabata alisema kuwa ni vema waliohusika na tatizo la Dowans kubeba gharama hizo wenyewe na kuwa waendelee na msimamo wao wa mwaka 2002 wa ‘hakuna mtu kuingia, hakuna mtu kutoka’.
Alisema pia kuna haja kwa Serikali kukaa na IPTL na kupitia upya vipengele vya mkataba na kuviondoa vile vilivyopitwa na wakati na kupendekeza Kamati ya Serikali inapopitishwa mikataba basi kuwepo uwakilishi wa Kamati ya Majadiliano ili kuweka mikataba ambayo haiumizi Tanesco na Serikali kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano, Abdul Mkama alisema matatizo ya shirika hilo hayatatuliwa kwa kuligawa, suluhisho ni kuanzishwa vyanzo vingi vya kuzalisha umeme ambayo vitakidhi mahitaji. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesajili tuzo ya Sh. bilioni 94 ya Dowans hivyo itailazimu Tanesco kulipa fedha hizo pamoja na gharama za kuendesha kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment