Monday, October 24, 2011

Kikwete maji ya shingo


Saed Kubenea's picture
Na Saed Kubenea

RAIS Jakaya Kikwete amebakiwa na njia mbili tu kulinda nafasi yake katika Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ama aachane na mpango wake wa kufukuza anaowaita “magamba,” au afanye maasi ya makusudi na kuwatimua nje ya mpango wake wa awali wa kuwabembeleza kujiondoa.
Wakati watuhumiwa wameonyesha ukaidi na hata kuonyesha kutokusikia anachosema; taarifa zinasema wameanza kutumia Umoja wa Vijana (UV-CCM) kuwatetea kwa njia ya kumshutumu waziwazi Kikwete na hata mtoto wake Ridhiwan.
Wachunguzi wa mambo wanaona njia mbili ambazo Kikwete anaweza kuchangua mojawapo, ni kama ifuatavyo:

Kwanza, kuwaangukia watuhumiwa na kuwataka wajisikie amani katika chama na kuendelea kutafuta uongozi na nafasi nyingine kwa ngazi mbalimbali. Hili, hata hivyo, wachunguzi wanasema linaweza kumgharimu kisiasa.

Pili, kuleta mabadiliko katika mfumo wa katiba ya chama chake ili kupata nafasi ya kuwaengua.
Tayari njia ya kwanza imeelezwa na baadhi ya makada na wazee ndani ya CCM, kuwa ni “kula matapishi,” na kudhoofisha nafasi ya mwenyekiti ambaye pia ni rais wa jamhuri.

Waliohojiwa jijini Dar es Salaam, Jumatatu hii na kukataa kutajwa majina gazetini wamesema, akifanya hivyo atakuwa anakidhalilisha na kukidharaulisha chama.
Njia ya pili ya kukabiliana na watuhumiwa wa ufisadi ndani ya CCM inaweza kulenga kuzuia wabunge wake kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC).

Hili linaweza kufanyika kwa njia mbili: Kuondoa utaratibu wa kuwa na wajumbe wanaotokea mkoani na badala yake watokee wilayani tu.
Njia nyingine ambayo sharti itokane na mabadiliko ya katiba, ni kuzuia wabunge kugombea ujumbe wa NEC wilayani; badala yake wasubiri uteuzi kupitia nafasi za wajumbe ndani ya kamati ya bunge ya CCM.

Kwa miezi sita sasa, viongozi ndani ya CCM, Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz wamekuwa wakishinikizwa, angalau kwa kauli, wajiuzulu uongozi ili “kusafisha” chama, kutokana na wao kutuhumiwa ufisadi katika nyanja mbalimbali.

Ni Rostam peke yake, miongoni mwao aliyehiari au aliyeshinikizwa kwa siri, kujiuzulu ubunge na ujumbe wa NEC. Hata hivyo, Rostam ameonekana waziwazi jimboni Igunga, akimbeba rais mstaafu Benjamin Mkapa kwenye kampeni za uchaguzi mdogo kuziba pengo aliloacha.
“Unajua, CCM inahitaji mabadiliko makubwa ya katiba, ambapo moja ya mapendekezo sharti iwe kuzuia wabunge kugombea ujumbe wa NEC kupitia wilayani,” ameeleza kada mmoja na kuongeza, “…pendekezo hilo likipita, basi Kikwete atakuwa amefanikiwa kuwadondosha kina Lowassa.”
Umuhimu wa mabadiliko haya umeonekana kufuatia taarifa kuwa kuna njama za kumwengua Rais Kikwete kutoka uenyekiti wa chama chake.

Ilikuwa MwanaHALISI ambayo miaka mitatu iliyopita iliripoti taarifa za kumwondoa Kikwete kwenye uongozi. Licha ya gazeti kubezwa na wanachana na viongozi wa chama hicho, lilikemewa pia na msajili wa magazeti nchini na kufungiwa kwa siku 90.

Miezi miwili iliyopita, viongozi wastaafu wa chama hicho mkoani Morogoro, walikariri taarifa hizohizo wakisema kuna wanaopita wilayani na makao makuu ya mikoa wakishawishi Kikwete atoswe.

Hivi karibuni, waziri wa mambo ya nje, Benard Membe alikaririwa akisema wateule wa Kikwete wanamsaliti; akifuatiwa na katibu wa uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliyekaririwa akisema kuna njama za kumng’oa Kikwete.

Kinachoelezwa na wapinzani wa Kikwete ni kwamba amekifanya chama kudhoofika na kuwa kwenye wakati mgumu hadi kuonekana kuwa hakiwezi kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Habari zinasema baadhi ya wanachama wanaotaka Kikwete ang’oke kwenye uongozi tayari wamejiadaa kuwasilisha hoja hiyo kwenye mkutano wa NEC uliopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.
Hata hivyo, MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake kwamba mkakati wa kutaka wajumbe wa NEC watoke wilayani umeanza kukigawa chama hicho.

Habari zinasema wapo wanaoona hatua hiyo ya kupeleka nafasi za NEC wilayani imelenga kuwaengua watuhumiwa wawili wa ufisadi ambao hawajaamua kuchukua njia ya Rostam.
Kwa njia hii na kama mapendekezo ya mabadiliko ya katiba yatapitishwa, Lowassa na Chenge waweza kushindwa kuingia NEC kwa kuwa uchaguzi wa nafasi hiyo kupitia kamati ya Bunge ya CCM, tayari umefanyika. Uchaguzi mwingine utafanyika baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hoja ya kuzuia wabunge kugombea wilayani inaondoa uwezekano wa kukuta NEC yote ikiongozwa na wabunge ambapo, kwa vyovyote vile, wanachama wa kawaida hawawezi kushindana nao,” anasema kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya CCM.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa CCM kufanya mabadiliko ambayo yanauma kwa baadhi ya wanachama wake. Iliwahi kutengeneza kanuni ya kuondoa utaratibu wa kupiga kura tatu kumpata mgombea urais mwaka 2005. Iliwahi pia kuweka sharti la kuwa na digrii ili ugombee urais.

Wakati hayo yakitendeka, mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), mkoa wa Arusha, James Millya ameendelea kumshindilia Kikwete kwa kukaa kimya kuhusu kauli ya Baraza la Vijana mkoa wa Pwani, kuwa rais ajaye hawezi kuwa “mtu kutoka Kaskazini” mwa nchi hii.
Sehemu ya uongozi wa UV-CCM hivi sasa inadai kuwa, kwa vile mtoto wa rais, Ridhiwan alikuwa kwenye baraza hilo, basi anajua vema chanzo cha kauli hiyo.

Katika waraka wake ambao alipanga kuusoma kwa wananchi, juzi Jumatatu, mjini Arusha (haukusomwa), Millya anatuhumu UV-CCM mkoa wa Pwani kwa kupanga “safu ya uongozi ndani ya nchi” kabla ya uchaguzi.

“Mapema mwaka huu, baraza la vijana mkoa wa Pwani walitamka wazi kwamba, ‘rais wa 2015 kamwe hawezi kutokea kanda ya Kaskazini na anayemjua Rais wa 2015, ni Rais Jakaya M. Kikwete…’ ” amelalamika Millya.

Amesema, “Mbali na kwamba hili ni tusi kubwa kwa watu wa Kaskazini wenye haki yao kikatiba kuwania nafasi ya uongozi wa juu wa nchi yetu, ni tusi pia kwa wapiga kura wa Tanzania…ni dhahiri kuwa rais ameshapangwa na kikundi kidogo cha watu na upigaji kura wa 2015 utakuwa ni usanii mtupu.”

Millya anaituhumu ikulu kushindwa kukanusha kwamba Rais Kikwete hayumo “au hatarajii kushinikiza kwa mabavu mtu wa kuongoza taifa hili baada ya kumaliza kipindi chake cha urais” Novemba 2015.
Ameandika katika waraka wake na kuuliza, kama rais ameshapatikana, demokrasia iko wapi?

No comments:

Post a Comment