Monday, October 10, 2011

Dk Mwakyembe akimbizwa India

Rais Jakaya Kikwete akimjulia hali Naibu Waziri wa Ujenzi Dkt.Harrison Mwakyembe wakati alipomtembelea nyumbani kwake Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam juzi.Picha na Ikulu
ALIONDOKA JANA SAA SITA NA NDEGE YA QATAR
Ramadhan Semtawa na Raymond Kaminyonge
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe amekimbizwa India kwa matibabu zaidi baada ya hali yake ya afya kuzidi kuzorota.Taarifa za kuumwa kwa Dk Mwakyembe zilisambaa zaidi mwishoni mwa wiki, baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya na juzi Rais Jakaya Kikwete, alimtembelea nyumbani kwake Kunduchi  Beach, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, jana baada ya hali ya naibu waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Kyela kuzidi kuwa mbaya, Serikali ililazimika kumkimbiza India kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya Appolo.Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, alithibitisha Dk Mwakyembe kupelekwa India.Hata hivyo, Nyoni alisema haikuwa sahihi kuzungumzia kwa undani safari hiyo ikiwamo ujumbe wa watu aliondoka nao.

"Siyo vizuri sana kuanza kusema aliondoka saa ngapi na aliondoka na nani. Lakini, zipo taratibu kama mtu ni mgonjwa mahututi kuna utaratibu wa kumsafirisha na kama hayuko mahututi pia upo utaratibu mwingine," alifafanya Nyoni.

Alisema mara nyingi mtu ambaye anaweza kuzungumza hali hali halisi ya mgonjwa ni daktari."Jambo la msingi tumuombee  Mungu ili afike salama na apate matibabu, lakini akiwa huko pia atasema jamani nimefika  salama," aliongeza Nyoni.  

Juzi Dk Mwakyembe aliliambia gazeti la Mwananchi kwamba alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya mwili kuvimba. “ Ni kweli naumwa nipo nyumbani, hata sura yangu imebadilika. Sasa hivi nasubiri daktari wangu, nilisikia natakiwa kupelekwa India kwa matibabu,” alisema.

Akizungumzia ugonjwa unaomsumbua Dk Mwakyembe, mkewe Linah alisema kwamba mumewe alianza kusumbuliwa na ugonjwa huo miezi mitatu iliyopita.

“Alianza kuugua muda mrefu kidogo kama miezi mitatu iliyopita, hali hiyo ilikuwa inatokea na kupotea hadi sasa ambapo hali imekuwa mbaya,” alisema.

Washirika wake wa karibu
Hata  hivyo, vyanzo vilivyo karibu na  Dk Mwakyembe, jana vililiambia gazeti hili kwamba naibu waziri huyo aliondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Qatar.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo,  Dk Mwakyembe alilazimika kuondoka na ndege ya Qatar badala ya ile ya Emirates kwani angechelewa.

"Ameondoka leo (jana) saa sita mchana na ndege ya Qatar. Hali yake siyo nzuri hata kidogo," kilisema chanzo kimoja cha habari .

Chanzo hicho kiliongeza kwamba, Dk Mwakyembe anatarajiwa kuwasili India leo na moja kwa moja atapelekwa hospitalini kupatiwa matibabu.

Taarifa mkanyangiko
Wakati taarifa za baadhi ya madaktari zikionyesha Dk Mwakyembe, anasumbuliwa na kisukari, baadhi ya watu wake wa karibu  wanaamini maradhi hayo ni sumu.

Kwa mujibu wa washirika hao wa karibu wa  Dk Mwakyembe, uthibitisho wa sumu ulitolewa na mmoja wa madaktari maarufu nchini ambaye alimweleza bayana kwamba alikuwa na sumu mwilini.

Vyanzo hivyo vilisema kwamba, Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipata matibabu, alielezwa kusumbuliwa na sukari.


"Mtu akishika ngozi inapepetuka na kutoa unga, akishika nywele zina nyonyoka, sasa hii ni hatari," alifafanua mmoja ya watu walio karibu naye.

Alianza kuumwa taratibu    
Vyanzo vya habari vinasema kuwa Dk Mwakyembe alikuwa akiumwa taratibu na wakati mwingine alilazimika kumeza vidonge hali hiyo inapomjia.

"Alikuwa anaumwa taratibu, sasa wakati mwingine hali hii inapomjia alikuwa akilazimika kumeza vidoge ili kutuliza," vyanzo hivyo vilidokeza.

Aliongeza kwamba, awali, hali hiyo ilipokuwa ikimjia mwili wake ulikuwa ukikakamaa na baada ya kunywa vidonge hutulia.

Nyumbani kwa Dk Mwakyembe

Jana, asubuhi mwandishi na mpigapicha wa gazeti hili walifika  nyumbani kwa  Dk Mwakyembe.

Hata hivyo, akizungumza nyumbani hapo, dada wa Dk Mwakyembe, Grace Mwakyembe aliwaeleza waandishi kwamba hali ya kaka yake inaendelea vizuri.

“ Yupo ndani anapumzika, sisi ndugu tumeamua kwamba apumzike hivyo hamuwezi kumwona,” alisema Grace.

Aliongeza, “tunafahamu kwa jinsi alivyo angewaona, angependa kuzungumza na nyie, lakini sisi ndugu tumeona ni vizuri akipumzike. Tunasubiri uchunguzi wa daktari, kama atatoa taarifa zinazotaka akatibiwe nje ya nchi tutafanya hivyo,”.

1 comment:

  1. NINAOMBA NDUGU WA KARIBU WA DR MWAKYEMBE WAFANYE WAWEZAVYO WAFIKE LAGOS NIGERIA KWA NABII T.B.JOSHUA MWENYE KANISA LIITWALO "SYNAGOGUE CHURCH OF ALL NATIONS" AKAPEWE ANNOINTING WATER ILI ANYWE NA KUPULIZIWA KWENYE NGOZI.ANY EVIL SICKNESS,TOXCIC SUBSTANCES WILL BE FLUSHED OUT BY THE BLOOD OF JESUS AND THE FIRE OF THE HOLYSPIRIT. AMINI,ATAPONA KWA KUFANYA HIVYO.HOSPITALI ITAMTESA!HIYO NI SUMU ILIYOCHANGANYIKANA NA EVIL SPIRITS.NI MUNGU PEKE YAKE KWA MAOMBI ATAPONA.

    ReplyDelete